Home Biashara JKT YAJIVUNIA MAFANIKIO YALIYOANZA KUPATIKANA KATIKA KILIMO MKAKATI

JKT YAJIVUNIA MAFANIKIO YALIYOANZA KUPATIKANA KATIKA KILIMO MKAKATI

0

Katibu wa Kamati ya Kimakakati ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi JKT, Luteni Kanali Peter Lushika,,akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kumaliza ziara yake ya kukagua miradi mbalimbali inayotekelezwa na Jeshi hilo  katika kikosi cha 842KJ Mlale JKT kilichopo Songea Mkoani Ruvuma Leo April 19,2021.

Kaimu Kamanda Kikosi cha 842 KJ Mlale JKT Songea, Mkoani Ruvuma,Godwin Mapunda,akielezea kwa waandishi wa habari leo April 19,2021 jinsi walivyotekeleza kilimo cha kimkakati kwa kulima ekari 1000 za mahindi ili kujitosheleza kwa chakula.

Mtafiti kutoka Taasisi ya Utafiti wa Kilimo nchini(TARI), Frank Reuben,akizungumzia taasisi hiyo inavyofanya utafiti maeneo mbalimbali ya vikosi vya JKT na kushauri mazao yanayopaswa kulimwa Leo April 19,2021.

Muonekano wa Shamba la Mahindi lenye ekari 1000 linalolimwa katika Kikosi cha 842 KJ kilichopo Mlale JKT Songea Mkoani Ruvuma.

Mtambo wa Kuchakata Mahindi uliopo katika Kikosi cha 842 KJ Mlale JKT Songea Mkoani Ruvuma.

……………………………………………………………………………………………

Na Alex Sonna, Ruvuma

Katibu wa Kamati ya Kimakakati ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi, JKT,  Luteni Kanali Peter Lushika, amesema,mpango wa Jeshi hilo wa Kilimo Mkakati umeanza kuonyesha mafanikio kutokana na baadhi ya mambo ikiwemo kununuliwa kwa zana za kilimo za kisasa kabla ya muda uliopangwa.

Akizungumza Leo April 19,2021 wakati wa ziara yake katika kikosi cha 842KJ Mlale JKT Songea Mkoani Ruvuma Luteni Kanali Lushika amesema,katika mpango huo Jeshi hilo pamoja na mambo mengine lilipanga kununua zana bora za kilimo yakiwemo matrekta makubwa 30 kabla ya kufikia mwaka 2024/2025 tayari mpaka sasa wameshanunua matrekta makubwa 15.

Akitaja malengo ya kuanzisha kilimo hicho, Luteni Kanali Lushika, amesema Mkuu wa JKT Meja Jenerali, Charles Mbuge baada ya kuteuliwa kuliongoza jeshi hilo Novemba 2019 aliunda kamati maalum ya kilimo mkakati lengo lilikuwa kuzalisha mazao ya kimkakati na kujitosheleza kwa chakula.

“Lengo jingine ni kujitosheleza kwa chakula, na kufundisha vijana stadi za kazi kutokana na vijana wengi wanaokuja JKT lengo lao ni kuajiriwa na vyombo vya ulinzi na usalama hivyo tunalenga kubadili fikra za vijana kutoka kutegemea ajira rasmi na kujiajiri kupitia kilimo,”amesema

Pia, amesema lengo ni kutekeleza agizo la serikali la uchumi wa viwanda kwa kuwa viwanda vingi vinaanzishwa na malighafi nyingi ni mazao ya kilimo.

“Tukaona tuanzishe kamati ya kimkakati na kutoa wataalam kutoka taasisi za kilimo na pia haya mashamba yanatumika kama mashamba darasa kwa vijana wanaosomea kwenye kilimo na uvuvi wawe wajifunze na kusaidia wananchi wanaotuzunguka wanakuja kujifunza kilimo bora,”amesema.

“Ununuzi wa matrekta haya ni moja ya mafanikio kwani mpango mkakati huu tumeanza kuutekeleza mwaka 2019/20 ambao unaishia mwaka 2024/2025,lakini mpaka sasa tumeshanunua matrekta makubwa 15,haya kwetu ni mafanikio kwani yatawezesha sasa kulima kisasa na kwa tija.”alisema Luteni Kanali Lushika

Aidha Luteni Kanali Lushika  amesema kuwa mpango huo ulianza kwa kulima ekari 2200 za Mahindi, Mpunga na Maharage lakini mpaka kufikia katika msimu huu wa kilimo wamelima ekari 6,600.

“Mwaka 2020/21 tumelima ekari 6600 ambapo ekari 3500 ni za mahindi, ekari 2500 mapunga na ekari 600 za maharage na ifikapo mwaka 2024/25 tutafikia ekari zaidi ya 28,000 na tutalima kitaalam,”amesema.

Ameeleza kuwa kilimo hicho kinaangalia mazingira na hali ya hewa ili mazao hayo kustawi

Awali Kaimu Kamanda Kikosi cha 842 KJ Mlale JKT Songea, Mkoani Ruvuma,Godwin Mapunda amesema katika msimu huu wa kilimo, kikosi hicho  kimetekeleza kilimo cha kimkakati kwa kulima ekari 1000 za mahindi ili kujitosheleza kwa chakula.

“Tulianza maandalizi mwezi Novemba mwaka jana na sasa tupo kwenye hatua ya kusubiri mavuno, tulipatiwa vifaa vyote muhimu kama pembejeo, matrekta na mbolea ili kufikia lengo,”amesema

Ameeleza kuwa katika ekari hizo wanatarajia kuvuna kwa kila ekari wastani wa gunia 16 hadi 20.

Aidha, amesema katika kikosi hicho tayari kuna kiwanda cha kuchakata mahindi hayo.

“Tunatarajia kufika mwaka 2024 angalau tufikie ekari 1200 hadi 1500 za mahindi,”amesema.

Naye, Mtafiti kutoka Taasisi ya Utafiti wa Kilimo nchini(TARI), Frank Reuben,amesema taasisi hiyo imefanya utafiti maeneo mbalimbali ya vikosi vya JKT na kushauri mazao yanayopaswa kulimwa.

“Lengo ni kuifanya JKT ichangie katika uzalishaji wa mahindi nchini, ambapo Tanzania inashika nafasi ya 25 duniani kati ya nchi 170 zinazolima mahindi,”amesema