Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dkt. Bilinith Mahenge akitoa hotuba ya kufungua mafuzo ya siku mbili kuhusu huduma zinazotolewa na Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) kwa Wakazi wa Dodoma katika Ukumbi wa Mikutano uliopo Makao Makuu ya Jeshi la Zimamoto, Jijini Dodoma leo.
Na Mwandishi Wetu, Dodoma
MKUU wa Mkoa wa Dodoma, Dkt Bilinith Mahenge amewataka wakazi wa mkoa huo kuchangamkia elimu inayotolewa na Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) kwa kuwa ina umuhimu mkubwa katika kujikwamua kiuchumi.
Dkt. Mahenge ameyasema hayo leo wakati akifungua mafunzo ya siku mbili kwa Wakazi wa Dodoma katika Ukumbi wa Mikutano uliopo Makao Makuu ya Jeshi la Zimamoto, Jijini Dodoma.
Akizungumza katika ufunguzi huo Dkt. Mahenge amewaeleza washiriki kwamba, ili kuweza kufanikiwa katika biashara ni vyema biashara au kazi husika kuwa imerasimishwa na kutambulika kisheria.
“Hatua ya kwanza ya kufanikiwa katika biashara ni kuirasimisha biashara na ikwa inatambulika kwa mujibu wa sheria. Na BRELA wapo hapa Dodoma kwa siku mbili kwa hiyo hii ni fursa kubwa na adhimu.”alisema Dkt. Mahenge.
Naye Msimamizi wa Kanda ya kati na Ofisi ya BRELA mkoani Dodoma, Gabriel Girangay alisema kwamba licha ya elimu hii kwa wote inayotolewa kwa siku mbili lakini pia ofisi zipo tayari kwa ajili ya kuwa hudumia.
“Ofisi ya BRELA mkoani Dodoma ipo tayari kuwahudumia na inafanya maandalizi ya kufika katika wilaya zote tisa za Mkoa wa Dodoma kwa ajili ya kutoa elimu kwa wananchi katika maeno yao kuhusu huduma zetu.” alisema Girangay.
Aidha Girangay amewataka wadau wa BRELA walio katika mkoa wa Dodoma na kanda nzima ya kati, wasipate shida ya kwenda ofisi za BRELA jijini Dar es Salaam na badala yake wafike katika Ofisi za BRELA mkoani Dodoma zilizopo katika Jengo la PSSSF eneo la Makole, Ghorofa ya 10.
Msaidizi wa Ofisi Mwandamizi wa Utawala kutoka BRELA, Bi. Saada Kilabula amemshukuru Mkuu wa Mkoa Dkt. Mahenge kwa niaba ya Afisa Mtendaji Mkuu, Godfrey Nyaisa kwa kuthamini uwepo wao ndani ya Dodoma na kuja kufungua mafunzo hayo.
BRELA inaendelea na mpango wa kutoa elimu kwa umma, ambapo kwa awamu ya kwanza mikoa sita itafikiwa ambayo ni Ruvuma, Njombe, Iringa, Singida, Dodoma na Morogoro.