WAZIRI wa Maji, Mhe.Juma Aweso,akizungumza wakati wa uzinduzi wa Kampeni ya kudhibiti upotevu wa maji nchini hafla iliyofanyika leo April 16,2021 jijini Dodoma.
Mkurugenzi Mwendeshaji wa Benki ya Equity Esther Kitoka,akizungumza jinsi ya benki hiyo ilivyoshirika katika Kampeni ya kudhibiti upotevu wa maji nchini hafla iliyofanyika leo April 16,2021 jijini Dodoma.
Katibu Mkuu Wizara ya Maji Mhandisi Antony Sanga,akizungumza wakati wa uzinduzi wa Kampeni ya kudhibiti upotevu wa maji nchini hafla iliyofanyika leo April 16,2021 jijini Dodoma.
Mwenyekiti wa Bodi ya ATAWAS, Mhandisi Geofrey Hilly,akizungumza wakati wa uzinduzi wa Kampeni ya kudhibiti upotevu wa maji nchini hafla iliyofanyika leo April 16,2021 jijini Dodoma.
Baadhi ya washiriki wa Mkutano wakifatilia Hotuba ya Waziri wa Maji, Mhe.Juma Aweso, wakati wa uzinduzi wa Kampeni ya kudhibiti upotevu wa maji nchini hafla iliyofanyika leo April 16,2021 jijini Dodoma.
Mkuu wa Idara ya Biashara Equity Benki Tanzania Isabela Maganga,akielezea mikakati yao waliyonayo kama benki wakati wa uzinduzi wa Kampeni ya kudhibiti upotevu wa maji nchini hafla iliyofanyika leo April 16,2021 jijini Dodoma.
Mkurugenzi Mwendeshaji wa Benki ya Equity Esther Kitoka,akikabidhi hundi ya shilingi milioni 10 kwa Wizara ya Maji kwa ajili ya kukarabati huduma za maji katika shule ya Makole pamoja na kuanzisha huduma ya mkopo kwa wananchi kwa ajili ya kuunganishiwa huduma za maji mara baada ya uzinduzi wa kampeni ya kudhibiti upotevu wa maji nchini iliyofanyika leo April 16,2021 jijini Dodoma.
…………………………………………………………………………………………
Na.Alex Sonna,Dodoma
WAZIRI wa Maji,Mhe.Juma Aweso,amezindua Kampeni ya kudhibiti upotevu wa maji nchini,huku Benki ya Equity wakitoa shilingi Milioni 10 kwa ajili ya kukarabati huduma za maji katika Shule ya Makole na kuanzisha huduma ya mkopo kwa wananchi kwa ajili ya kuunganishiwa huduma za maji.
Akizungumza leo April 16,2021 jijini Dodoma Mhe.Aweso amesema kumekuwa na upotevu wa maji na kuchangia kupotea kwa mapato kila mwezi kiasi cha shilingi bilioni 9.5.
Waziri Aweso amesema kuwa upotevu wa maji nchini katika Mamlaka mbalimbali za maji imekuwa kero ambayo inasababisha kiasi kikubwa cha mapato kupotea.
“Takribani asilimia 36 ya maji yanapotea kila mwezi lakini pia kiasi cha fedha takribani shilingi bilioni 9.5 zinapotea kila mwezi ambazo tungeweza kuzifanyia mambo mengine ya maendeleo”amesema Aweso
Hata hivyo amesema kuwa kiasi cha maji ambacho kimekuwa kikipotea kila siku ni kikubwa sana ambacho hakitakiwi kuendelea kuvumiliwa bali hatua za haraka zichukuliwe ili kukabilina na tatizo hilo.
Mhe.Aweso amesema kuwa njia ambazo zimekuwa zikichangia kupotea kwa maji ni pamoja na watu kujiunganishia huduma hiyo kinyume na utaratibu.
Aidha, Aweso amewataka wananchi kuwa walinzi wa miradi ya maji ambayo serikali imewekeza kiasi kikubwa cha fedha ili idumu na kutoa huduma kwa muda mrefu kwa wananchi.
Hata hivyo Waziri Aweso amewapongeza Equity Benki kwa kuwa moja wa wadau muhimu watakaokuwa wakitoa elimu kwa wananchi kutunza huduma za maji pamoja na kutoa kiasi hicho cha fedha kwa ajili ya kukarabati huduma za maji katika Shule ya Makole.
”Nawapongeza kwanza kwa kushiriki katika kampeni hiyo ya udhibiti upotevu Maji pamoja na kuanzisha huduma ya mkopo kwa wananchi kwa ajili ya kuunganishiwa huduma za maji,ahadi yetu kama Wizara tutashirikiana kwa kila hatua ili kumaliza tatizo la upotevu wa maji nchini”amesema Aweso
Kwa upande wake Mkurugenzi Mwendeshaji wa Benki ya Equity Esther Kitoka ambao ni wadau wa Kampeni hiyo amesema kuwa wao wameshiriki katika kuanzisha huduma ya mkopo kwa wananchi kwajili ya kuunganishiwa huduma za maji.
Bi.Kitoka, amesema moja ya sababu zinazochanagia upotevu wa maji ni idadi kubwa ya watu kutokuwa na huduma hiyo hivyo watu kutumia njia zisizo rasmi kupata huduma hiyo muhimu.
“Tumeanzisha huduma ya kutoa mikipo kwa wananchi sisi tunalipia fedha za kuunganisha maji mojamoja kwa mamlaka husika na mwananchi anakuwa analipa kwetu mkopo kidokidogo”amesema Bi.Kitoke
Aidha benki hiyo imekabidhi kiasi cha shilingi milioni 10 kwa ajili ya kukarabati miundombinu ya maji katika Shule ya Makole huku wakiahidi kutoa elimu kwa wananchi kuhusu jinsi ya kutunza huduma za maji nchini.
Naye Mwenyekiti wa Bodi ya ATAWAS, Mhandisi Geofrey Hilly amesema kuwa lengo la kampeni hiyo ni kudhibiti upotevu wa maji katika maeneo mbalimbali nchini na kuongeza mapato.
“Katika Kampeni hii tutatumia makundi mbalimbali wakiwemo watu wa Media ili kufikisha ujumbe kwani wanaohusika katika upotevu wa huduma hii ni watu ambao wapo katika mazingira hayohayo”amesema Hilly