Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Singida, Adili Elinipenda (kushoto) akitoa taarifa kwa waandishi wa habari kuhusu kesi mbalimbali zinazohusu matukio ya rushwa. Kulia ni Kaimu Mkuu wa Taasisi hiyo Mkoa wa Singida, Mzalendo Widege.
Na Dotto Mwaibale, Singida
TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Singida imemfikisha mahakamani Halima Mpita aliyekuwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Iramba kwa kipindi cha mwaka 2013 hadi Mei 2015 pamoja na watumishi wengine kwa makosa ya kuisababishia hasara Serikali kiasi cha sh.Milioni thelathini na tatu laki moja (33,100,000) kwa kufanya malipo ya mbao hewa kwa shule za sekondari katika wilaya hiyo.
Watumishi wengine waliofikishwa mahakamani kwa kosa hilo ni Stephen Pundile, aliyekuwa Afisa Mipango na Zakia Ituja aliyekuwa Afisa Takwimu wakishirikiana na Nicholaus Maro ambaye ni Mkurugenzi wa Kampuni binafsi ya Nicholaus Maro & General Supplies.
Akitoa taarifa hiyo kwa waandishi wa habari Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Singida, Adili Elinipenda alisema kesi iliyofunguliwa dhidi ya watuhumiwa hao ni namba ECC.02/2021.
Elinipenda alitaja kesi nyingine kuwa ni namba ECC. 08/2021 ambayo inawahusu waliokuwa watumishi wa Shirika la Bima la Taifa mkoani hapa ambao ni Costa Massi na Raymond Msangi ambao wanatuhumiwa kwa kutengeneza nyaraka za bima ya gari yenye maelezo ya uongo.
” Kesi namba hii ECC.01/2021 inawahusu waliokuwa watumishi katika Mahakama ya Mkoa wa Singida ambao ni Joshua Chonya aliyekuwa mtendaji wa mahakama hiyo na Innocent Haonga aliyekuwa Afisa Tawala. Watuhumiwa hawa wamesomewa mashtaka ya kuzifanyia ubadhirifu fedha kiasi cha Tshs. 500,000 zilizokuwa zimetolewa kwa ajili ya kuwalipa mashahidi wanaofika mahakamani hapo kwa ajili ya kutoa ushahidi.” alisema Elinipenda.
Elinipenda alitaja kesi nyingine kuwa ni namba CC.01.2021 ambayo ilifunguliwa mahakamani dhidi ya Sarafia Singa ambaye ni Katibu wa Baraza la Ardhi la Kata ya Mkiwa lililopo wilayani Ikungi pamoja na Mwenyekiti wa baraza hilo Rehema Mwanja na wajumbe wawili wa baraza hilo ambao ni Josephaly Mwandi na Jofrey Nkuwi kwa kuomba rushwa ya sh. 100,000 na kupokea sh.60,000 ili wasimchukulie hatua mtoa taarifa kwa kushindwa kutii maagizo ya baraza.
Alitaja kesi nyingine kuwa ni namba CC.01.2021 iliyofunguliwa dhidi ya Said Suswi ambaye ni mwenyekiti wa Kitongoji cha Bunku kilichopo wilaya Ikungi kwa kupokea rushwa ya sh.50,000 ili aweze kumruhusu mtoa taarifa kulima kwenye eneo lisiloruhusiwa.
Katika kesi namba CC.27.2021 ilifunguliwa Iramba dhidi ya Simion Shango na Joseph Shani kwa kujihusisha na vitendo vya rushwa sh. 1,025,000 asimpeleke mahakamani kijana aliyekuwa na mahusiano na binti yake ambae ni mwanafunzi wa kidato cha nne na kesi namba CC.31.2021 ilifunguliwa Iramba dhidi ya Joseph Shani kwa kujihusisha na vitendo vya rushwa sh. 1,025,000 ili kijana wake asipelekwe mahakamani kwa kosa la kuwa na mahusiano na mwanafunzi .
Elinipenda alisema jumla ya kesi tano zilitolewa hukumu ambazo ni namba CC.01/2020 watuhumiwa ni Joseph Kweka aliyekuwa Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Lighwa na Yassin Shelukindo ambao walifikishwa mahakamani kwa tuhuma ya kumsajili mwanafunzi kufanya mtihani wa darasa la saba kwa mara ya pili na kwa kutumia jina ambalo siyo lake na kuwa wote wawili waliachiwa huru.
Alitaja kesi ya pili kuwa ni namba CC.04/2020 iliyo muhusisha John Mbua Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Kinyarumi iliyopo Ikungi ambaye alifikishwa mahakamani kwa kushawishi rushwa ya sh. 150,000 na kupokea shs. 100,000 ili amsaidie fundi aliyekuwa na madai aweze kulipwa ambapo alihukumiwa kulipa faini ya sh.500,000 au kifungo cha miaka mitatu.
Elinipenda alitaja kesi ya tatu kuwa ni namba CC.05/2020 iliyokuwa dhidi ya Tatu Mbua na wenzake Mwenyekiti wa baraza la ardhi Kata ya Puma ambayealifikishwa mahakamani kwa tuhuma za kuomba rushwa ya sh. 100,000 kisha kupokea sh. 50,000 ili kushawishi kutoa hukumu ya kipendeleo kwenye kesi ya mgogoro wa ardhi. Mshtakiwa alitiwa hatiani kwa kifungo cha miaka mitatuau kulipa faini ya sh. 500,000.
Katika kesi ya nne namba CC.27/2021 Simion Shango na mkulima mshtakiwa ambaye ni mzazi wa mwanafunzi wa kidato cha nne ambaye alishawishi rushwa ya sh. 1,025,000 ili asimpeleke mahakamani kijana aliyekuwa na mahusiano na binti yake mshtakiwa alitiwa hatiani kifungo cha miaka mitatu au kulipa faini ya sh 500,000.
Alitaja kesi ya tano kuwa ni namba CC.31/2021 mshitakiwa akiwa ni Joseph Shani ambaye alifikishwa mahakamani kwa kuahidi kutoa rushwa ya Tshs. 1,025,000 ili kijana wake asifikishwe mahakamani kwa kuwa na mahusiano na mwanafunzi. Mshtakiwa alitiwa hatiani kwa kupewa adhabu ya kifungu cha miaka mitatu jela au kulipa faini ya sh. 500,000.
Aidha Elinipenda alisema kuna jumla ya kesi 15 zinaendelea kwenye mahakama za Mkoa wa Singida na kuwa zipo kwenye hatua mbalimbali za uendeshaji.
Akizungumzia fedha zilizookolewa katika kipindi husika TAKUKURU Mkoa wa Singida imefanya operesheni mbalimbali za uokoaji na urejeshaji wa fedha na mali ambazo zilikuwa zichepushwe au kufanyiwa ubadhirifu kinyume na Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Na. 11 ya Mwaka 2007.
Aidha, katika kipindi hicho jumla ya sh. 59,896,707 ziliokolewa ambapo sh. 6,450,000 zilirejeshwa kutoka mikopo umiza, kiasi cha shs. 15,000,000 kutokana na fidia ya maeneo ya wananchi yaliyotwaliwa kuchimba madini huko Wilaya ya Mkalama, sh. 200,000 fedha hizi zimerejeshewa kwa wanafunzi Chuo cha Lake kama Ada ,fedha kiasi cha shs.13,165,109 zimerejeshwa kwa wakurugenzi wa Halmashauri, sh. 5,306,000 fedha hizi zilitokana na dhuluma kwa watu binafsi.
Alitaja fedha kiasi cha 13,475,600 kuwa zimeokolewa kutokana na Saccos na fedha kiasi cha sh. 1,300,000 zimeokolewa na kurejeshwa kwa wananchi waliochukuliwa vifaa vya ujenzi (mawe) na kampuni ya ujenzi wa mradi wa umeme (Backbone).
Akizungumzia kuhusu uelimishaji alisema katika kuiwezesha jamii kushiriki kikamilifu katika mapambano dhidi ya Rushwa TAKUKURU kupitia Idara ya Elimu kwa Umma hutumia mbinu mbalimbali kuwaelimisha na kuwashirikisha wanajamii wa makundi mbalimbali ikiwa ni pamoja na vijana wa shule za msingi, sekondari na vyuo .
Alisema ili kuwafikia na kuwaelimisha walengwa TAKUKURU inashirikiana na wadau wengine wa mapambano dhidi ya Rushwa ambao ni pamoja na Taasisi za dini, mashirika ya Umma, mashirika yasiyo ya Serikali, asasi za kiraia na sekta binafsi.
” Elimu kwa Umma ilitolewa kwa makundi mbali mbali katika jamii na pia katika kipindi tajwa ofisi iliendelea kuelimisha umma juu ya madhara ya Rushwa ambapo jumla ya mikutano ya Hadhara 23 imefanyika ,Semina 18 zimefanyika, Klabu za wapinga Rushwa 45 ziliimarishwa , maonesho (08) na Makala Sita (08) ziliandaliwa.”alisema Elinipenda.
Akizungumzia kuhusu uzuiaji rushwa alisema katika kudhibiti mianya ya rushwa katika Idara mbalimbali TAKUKURU Mkoa wa Singida imefanya kazi ya kuchambua mifumo yenye mianya ya rushwa kwa kufanya uchambuzi wa mifumo kubaini mapungufu katika maeneo ya uchambuzi wa mfumo wa utoaji wa vibali vya ujenzi kwa Halmashauri ya Manispaa Singida, Halmashauri za Wilaya Manyoni, Iramba, Mkalama na Ikungi.
Alitaja mfumo wa pili kuwa ni uchambuzi wa mfumo wa udhibiti mianya ya Rushwa inayotokana na kodi ya vibanda katika stendi kuu ya Mabasi Misuna- Halmashauri ya Manispaa ya Singida.
Akizungumzia kuhusu miradi ya maendeleo, Elinipenda TAKUKURU imefanya ufuatiliaji wa utekelezaji wa miradi ya maendeleo pamoja na kujenga uelewa wa pamoja kuhusu kiasi cha pesa kilichotengwa kwa ajili ya miradi ya ujenzi, ukarabati wa barabara, afya, elimu, maji n.k iliyopo chini ya Mamlaka za Serikali za mitaa, wakala wa Serikali na Serikali kuu, kufuatilia ili kuona uwiano kati ya matumizi ya fedha za umma na ubora wa huduma zinazotolewa, kuimarisha uwazi na uwajibikaji katika mchakato wa utekelezaji wa bajeti, kuimarisha ufanisi na matokeo mazuri ya matumizi ya fedha za umma na kupata msingi wa kufanya udhibiti na ufuatiliaji wa utekelezaji wa bajeti katika miradi husika.
Aidha katika kipindi cha Januari –Machi 2021 TAKUKURU Singida ilifanya Ufuatiliaji wa utekelezaji wa mfuko wa maendeleo ya Jamii awamu ya tatu (Tasaf III) kwa Halmashauri za Wilaya za Singida, Manyoni, Iramba, Mkalama na Ikungi na pia ufuatiliaji wa baadhi ya miradi ya Elimu.
Akizungumzia kuhusu TAKUKURU inayotembea alisema ni kampeni au utaratibu katika mkoa husika unaosaidia kutatua kero za rushwa kwa wananchi.
Alitaja mkakati wa utendaji kazi kuanzia Aprili – Juni, 2021 TAKUKURU Mkoa wa Singida kwa robo ya nne imejipanga kuendelea kufanya uchunguzi kwa taarifa zote za vitendo vya rushwa zitakazoibuliwa, kufanya uelimishaji kwa jamii kuhusiana na madhara ya rushwa uchaguzi, ufuatiliaji wa kina katika miradi ya maji, na elimu ujenzi wa miundombinu ya Barabara kwa lengo la kuona uwiano wa fedha zilizotolewa na serikali na majengo yanayojengwa au manunuzi ya vifaa.
Elinipenda alitumia nafasi hiyo kutoa rai kwa wananchi wote kwa ujumla mkoani hapa kujiepusha na vitendo vya Rushwa na kushiriki kikamilifu kutoa taarifa za vitendo vya Rushwa kwa kufika Ofisi zetu za TAKUKURU mkoa na wilaya , kupiga simu namba 113 au kumpigia Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Singida kwa Namba 0738150208 na kutoa ushirikiano kwenye uchunguzi na kushiriki kutoa ushahidi Mahakamani pale mnapohitajika kufanya hivyo.
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) ni chombo chenye dhamana ya kusimamia Mapambano Dhidi ya Rushwa Nchini kikiongozwa na Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Na. 11 ya Mwaka 2007.