************************************
Na Masanja Mabula,PEMBA.
MAHAKAMA ya Mkoa wa Kaskazini Pemba imewapeleka chuo cha mafunzo kwa kipindi cha miaka 35 watu wawili baada ya kutiwa hatiani kwa makosa ya udhalilishaji.
Katika mahakama hiyo mtuhumiwa wa kwanza kutiwa hatiani ni Mahmoud Hafidh Khamis 21 mkaazi wa Uwondwe shehia ya Shumba Vyamboni ambaye ametiwa hatiani kwa makosa mawili ya kuwaigilia kinyume na maumbile watoto wawili wa kike mmoja akiwa na umri wa miaka 7 na mwengine miaka 5.
Awali kijana huyo alikuwa anakabiliwa na makosa manne ikiwemo mawili ya kubaka na mawili ya kuingilia watoto wawili kinyume na maumbile.
Akisoma hukumu , hakimu wa mahakama ya Mkoa wa Kaskazini Pemba Abdalla Yahya alimuachia huru mtuhumiwa kwa makosa mawili ya kubaka baada ya maelezo ya upande mashahidi kupingana na maelezo ya waathirika.
“Maelezo ya mashahidi umepingana na maelezo ya waathirika , kwamba upande wa mashahidi walisema watoto hao walibakwa, lakini waathirika wenyewe walikana kubakwa , bali walisema waliingiliwa kinyume na maumbile”alisema.
“Hivyo kutokana na maelezo hayo kutofautiana , Mahakama inamuachia huru mtuhumiwa kutokana na makosa mawili ya kubaka”alifahamisha.
Hata hivyo mahakama hiyo imemwamuru kutumikia chuo cha mafunzo kwa kipindi cha miaka 14, kwa kosa la kumuingilia kinyume na maumbile mtoto wa kwanza na kosa la kumuingilia mtoto wa pili nalo atatumikia chuo cha mafunzo kwa kipindi cha miaka 14.
“Mahakama inamtia hatia mtuhumiwa kwa makosa mawili ya kuwaingilia kinyume na maumbile watoto hao, ambapo kosa la kwanza atatumikia chuo cha mafunzo miaka 14, halikadhalika na kosa la mtoto wa pili, hivyo adhabu hizo zitaenda sambamba”alifahamisha.
Aidha katika mahakama hiyo Seif Said Seif amepelekkwa chuo cha Mafunzo kwa kipindi cha Miaka 7 , baada ya kupatikana na kosa la kumbaka mtoto wa kike mwenye umri wa miaka 10.
Kesi hiyo namba 36/2018 ilitokea tarehe isiyojulikana mwezi wa 10/2007, ambapo akiwa chumbani kwake , Seif Said Seif alimbaka mtoto huyo na kumsababishia maumivu sehemu zake za siri.
“Mahakama iimekutia hatiani baada ya kukubaliana bila ya wingu la shaka juu ya ushahidi uliotolewa na upande wa mashitaka , hivyo utatumikia chuo cha mafunzo miaka saba pamoja na kulipa fidia kwa mwathirika ya shilingi million moja”alisema.
Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Pemba Salama Mbarouk Khatib alipongeza wananchi waliokwenda kutoa ushahidi wa kesi hiyo, na kuwataka kuendelea kutoa ushahidi wakati wanapohitajika.
“Serikali ya Mkoa itaendelea kutoa elimu kwa wananchi kupitia kwa masheha, hivyo tunawaomba wajitokeze kwenye mikutano hiyo, na waipokee elimu inayotolewa na kuifanyiakazi’alisisitiza.