**********************************
NA NAMNYAK KIVUYO, ARUSHA.
Aliyekuwa mkurugenzi wa Taasisi ya kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Tanzania Dkt Eduward Hosea amepita katika kinyang’anyiro cha urais wa chama cha wanasheria Tanganyika(TLS) 2021/2022 kwa kura 292.
Akitangaza matokeo mwenyekiti wa kamati ya uchaguzi huo Charles Rwechungura alisema kuwa Dkt Hosea ameibuka kidedea baada ya mchuano mkali baina yake na wanasheria wanne ambao ni Flaviana Charles aliyepata kura 223,Shehzada Walli aliyepata kura 192, Albert Msando aliyepata kura 69, pamoja na Fransis Stola aliyepata kura 17.
Rwechungura alisema kuwa idadi ya wapiga kura ni 5286 kura zilizopigwa 802 ambapo pia alitangaza nafasi nyigine zilizokuwa zikigombewa ikiwemo ya makamu wa rais wa chama hicho ambapo Gloria Kalabamu aliibuka kidedea kwa kura 395 dhidi wa mgombea mwenzie Gidion Mandes aliyepata kura 324 huku kura 77 zikiharibika.
Kwa upande wake Dkt Eduward Hosea alisema uchaguzi huo umekuwa wa haki na huru na ni uchaguzi wa kuigwa ambapo mtazamo wake kusimamia utawala wa sheria kwa kuwa na mahakama zilizo huru na TLS huru.
“Tutasimamia utawala sheria katika maeneo moja ikiwemo ni kila mtu kuwa huru na haki katika macho ya sheria pamaja na mahakama kuwa huru ikiwa ni pamoja na kuishauri serikali na kufanya nayo kazi kwa karibu,”Alisema Hosea.
Pia aliwataka watanzania wategemea TLS itaendelea kuwa wazi, itawajibika na kuwatetea bila kujali rangi wala sura na watapigania sheria na haki kwa lugha yao ya utu.
Naye mgombea mwenza aliyeshika nafasi ya pili Flaviana Charles alisema uchaguzi kuwa uchaguzi ulikuwa mzuri na haukuwa na vurugu zozote na umesha salama sasa wanakitumikia chama na taifa la Tanzania katika maeneo mbalimbali.
Aidha kwa suala la upigaji kura aliwataka wanasheria kuwa mfano kwa jamii katika kujitokeza kupiga kura kwani ni haki yao na sio kubaki kushabikia tu ambapo aliyasema hayo kutoka na idadi ndogo ya wapiga kura waliojitokeza kulinganisha na idadi ya waliojiandikisha ya 5286.
Sambamba na hayo pia aliwataka wanawake kutokata tamaa kugombea nafasi mbalimbali kwani wanawake wana nguvu kubwa katika jamii japo kuna changamoto ila wasizipe nafasi.