Mwenyekiti wa kamati ya ujenzi sheikh Yusuph Tutupa akishukuru mara baada ya kukabidhiwa msaada wa fedha za ujenzi wa msikiti.
Sheikh Yusuph Tutupa akimwonyesha maendeleo ya ujenzi mkuu wa mkoa wa Mbeya Albert Chalamila
Injini Haule akitoa maelezo ya kitaalam kwa mkuu wa mkoa wa Mbeya, Albert Chalamila juu ya ujenzi wa msikiti wa Kalumbulu ulioko wilayani Kyela.
………………………………………………………………………………………
NA DENIS MLOWE, KYELA
MKUU wa mkoa wa Mbeya Albert Chalamila amewataka waumini wa dini ya Kiislamu wilaya ya Kyela kufanya kazi kwa ushirikiano ili kukamilisha ujenzi wa msikiti wa Kalumbulu ulioanzwa kujengwa katika kata ya Mikoroshini wilayani humo mkoani Mbeya.
Akizungumza katika ziara aliyofanya wilayani Kyela, Chalamila alisema mtu wa kwanza kuwaza kutoa mchango wa ujenzi wa msikiti wa Kalumbulu alikuwa ni hayati Dk. John Pombe Magufuli ambaye alisema ujenzi wa msikiti huo atausimamia.
Chalamila alisema Mwezi wa tatu baada ya kuhudhuria kusaini mkataba wa Uganda na Tanzania hayati Magufuli aliahidi kuanza ziara katika mkoa wa Mbeya na kuahidi baada ya kukamilika kwa ujenzi wa msikiti huo ni akabidhiwe ili yeye aukabidhi kwa wananchi.
Aliongeza kuwa ni kweli hayati Magufuli amefariki imani yake alikuwa ni mkristo na sasa tunaongonzwa na rais samia suluhu hasani imani yake ni muislamu pindi atakavyoanza kufanya ziara yake hapa wilayani kyela akute msikiti huo umekamilika.
Alisema moja ya ajenda yake ni kutaka msikiti huo ukamilike hivyo amewataka waumini hao kujinyima na kufanya kazi kwa ushirikiano ili kuweza kukamilika haraka kwa ujenzi wa msikiti huo .
Chalamila alisema kuwa kukamilika kwa ujenzi wa msikiti huo ni kumbukizi nzuri ya kumuenzi aliyekuwa rais wa awamu ya tano hayati Dr John Magufuli na kuwashukuru wananchi pamoja na kutoa mchango wa kiasi cha shilingi million moja ili kuchangia ujenzi wa msikiti huo wa Kalumbulu.
Hadi kufikia hatua hiyo Chalamila amekwisha changia kiasi cha shilingi milioni 15 kuweza kukamilisha ujenzi wa msikiti huo ambapo kwa sasa bado wanakabiliwa na changamoto mbalimbali za vifaa vya ujenzi.
Kwa upande wake mkuu wa wilaya ya Kyela, Claudia Kita alisema wao kama viongozi wanaendelea kushirikiana na uongozi wa dini ya Kiislamu na kamati ya ujenzi ili kuweza kukamilisha ujenzi msikiti huo.
Kita amebainisha kuwa licha ya kuondoka kwa aliyekuwa rais wa awamu ya tano hayati Dr John Pombe Magufuli na kuacha ujenzi huo wa msikiti ukiendelea hautasitishwa na badala yake utaendelea kujengwa mpaka kukamilika kwake.
Alisema kuwa licha ya kuwepo kwa changamoto mbalimbali katika kipindi hiki cha mvua lakini hawatakata tamaa na kazi lazima iendelee ili msikiti huo uweze kukamilika.
Hata hivyo mkuu wa wilaya amemshukuru mkuu wa mkoa Albert Chalamila kwa kutoa mchango wa kiasi cha shilingi million moja ili ujenzi wa msikiti huo uweze kukamilika kwa haraka.
Naye Mwenyekiti wa kamati ya ujenzi wa msikiti huo, Sheikhe Yusuph Tutupa licha ya kushukuru msaada uliotolewa na mkuu wa mkoa wa Mbeya alisema kuwa ujenzi wa msikiti huo unatarajia kugharimu zaidi sh milioni 200 ambapo hadi sasa uko kwa asilimia 40 ya ujenzi.
Aidha ametoa wito kwa wadau mbalimbali kusaidia ujenzi wa msikiti huo ili ukamilike kwani ni moja ya nguzo ya kutoa sadaka kwa ajili ya kupata eneo la kuabudia.