Waziri wa mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula akipokea nakala ya hati za utambulisho za Balozi Mteule wa Uturuki Dkt Mehmet Gulluoglu.
…………………………………………………………………………….
Tanzania imeahidi kuendeleza mahusiano yake na Uturuki katika Nyanja za miundombinu,utalii,biashara na uwekezaji hasa baada ya kampuni zinazotoka nchini humo kuonesha uwezo katika ujenzi wa reli ya kisasa (SGR) unaoendelea.
Kauli hiyo imetolewa na waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula wakati akipokea nakala ya hati za utambulisho kutoka kwa Balozi Mteule Dkt Mehmet Gulluoglu na kumhakikishia kuwa Tanzania itaendelea kuwatumia wataalamu wa Uturuki katika miradi mbalimbali ya maendeleo
Balozi Mulamula amemuomba Balozi Mehmet kuhamasisha Makampuni na taasisi kutoka Uturuki kuja kuwekeza hapa nchini kutokana na mazingira bora ya biashara na uwekezaji yaliyopo Tanzania hususani katika maeneo ya utalii,biashara,miundombinu,elimu pamoja na afya.
Kwa upande wake Balozi Mteule wa Uturuki Dkt Mehmet Gulluoglu amempa pole Balozi Mulamula kwa niaba ya watanzania kutokana na kifo cha aliyekuwa Rais wa awamu ya tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Hayati Dkt. John Pombe Magufuli na kwamba msiba huo umeigusa kipekee Uturuki kwa kuwa Hayati Dkt. Magufuli alikuwa mshiriki na mdau muhimu wa mahusiano ya kimaendeleo kati ya Tanzania na Uturuki.
Dkt. Mehmet ameongeza kuwa Uturuki na Tanzania ina masuala mengi ya pamoja ya kushirikiana kupitia sekta mbalimbali za kiuchumi,kijamii n ahata kiutamaduni na kwamba yuko hapa nchini kuhakikisha kuwa hayo yote yanatekelezeka kwa maslahi ya pande zote mbili.
Hii ni shughuli rasmi ya kwanza kwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula kuitekeleza mara baada ya kukabidhiwa rasmi ofisi kutoka kwa mtangulizi wake Prof. Palamagamba John Kabudi ambaye kwa sasa ni Waziri wa Katiba na Sheria.