****************************************
Agizo hilo limetolewa na Mkuu wa wilaya ya Kinondoni Mhe Daniel Chongolo alipozuru Kata ya Kunduchi ikiwa ni mwendelezo wa ziara yake ya kikazi kata kwa kata kusikiliza kero za wananchi.
Amesema wenyeviti wa Serikali za Mitaa wanao wajibu wa kuhakikisha kuwa wananchi wanapatiwa ufumbuzi wa changamoto zinazowakabili katika Mitaa yao kwa wakati na ufanisi mkubwa.
“Wenyeviti wa Mitaa ni watu muhimu sana, mkitimiza wajibu wenu vizuri, kwanza kero zitapungua lakini pia kutawafanya wananchi wajenge Imani nanyi, lakini pia na Serikali inayowaongoza. Fanyeni kazi, wajibikeni, ondoeni kero mitaani mwenu, huo ndio uwajibikaji.”Amesisitiza Chongolo.
Aidha ameeleza kuwa vyeo walivyopatiwa ni kwa ajili ya kuwasaidia wananchi na si kutumika Kama fimbo au nguzo ya kuwazungusha na kuweka urasimu pale wanapohitaji huduma
Naye Diwani wa Kata hiyo Mhe. Michael Urio alipokuwa akizungumza alitoa shukrani zake kwa ujio wa Mkuu wa Wilaya katika Kata anayoiongoza, kwani kumewafanya wananchi kuzungumza kero na Changamoto zinazowakabili hali ilirejesha Imani ya Serikali inayowaongoza.
Katika ziara hiyo Mhe Chongolo amefanikiwa kusikiliza kero zipatazo 32 ambapo katika utatuzi wake amesisitiza kuzingatia maamuzi sahihi hasa zile kubwa na za muda mrefu.
Kero zilizopatiwa ufumbuzi ni Pamoja na migogoro ya uvamizi wa maeneo, Uchakavu wa Barabara, Utiririshaji wa maji taka hasa wakati huu wa mvua pamoja na zoezi la urasimishaji wa makazi.
Imeandaliwa na
Kitengo cha Habari na Uhusiano
Manispaa ya Kinondoni