Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed O. Mchengerwa,akizungumza na watumishi wa ofisi yake iliyopo Mtumba jijini Dodoma wakati wa kikao kazi chake na watumishi hao chenye lengo la kujitambulisha na kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi hao.
Watumishi wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed O. Mchengerwa (hayupo pichani) wakati wa kikao kazi cha Waziri huyo na watumishi hao chenye lengo la kujitambulisha na kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi hao.
Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Dkt. Laurean Ndumbaro akitoa neno la utangulizi wakati wa kikao kazi cha Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa na watumishi wa ofisi yake chenye lengo la kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi wa ofisi hiyo.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed O. Mchengerwa (kushoto) akipokea Taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya ofisi yake toka kwa Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi, mara baada ya waziri huyo kuzungumza na watumishi wa ofisi yake wakati wa kikao kazi cha kuhimiza uwajibikaji.
…………………………………………………………………………..
Na.Alex Sonna,Dodoma
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi na Utawala Bora, Mohammed Mchengerwa amewataka Wakuu wa Mikoa na Wilaya kuacha kutumia vibaya mamlaka zao kuwaweka ndani kinyume na sheria watu wanaotenda makosa huku akiwataka kuzingatia Utawala wa haki na sheria.
Hayo ameyasema jijini Dodoma wakati akizungumza na watumishi wa Wizara yake ikiwa ni siku kadhaa tangu ateuliwe na Rais Suluhu Hassan kushika nafasi hiyo akichukua nafasi ya Kepteni George Mkuchika ambaye ameteuliwa kuwa Waziri asiye na wizara.
Mhe.Mchengerwa amesema Wakuu wengi wa Mikoa na Wilaya wamekua wakitumia vibaya mamlaka yao waliyopewa kikatiba ya kuwaweka ndani masaa 24 hadi 48 watu waliofanya makosa huku akisisitiza viongozi hao kutambua kuwa Serikali ya Rais Samia inazingatia haki na utawala bora.
Waziri Mchengerwa pia ameitaka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa kuondoa kesi zote zilizopo mahakamani ambazo wanaona kwamba serikali haina uelekeo wa kushinda.
” Kumekua na mfulululizo wa kesi nyingi ambazo TAKUKURU inazipeleka mahakamani lakini haina ushahidi wa kutosha, niwaombe kuziondoa kesi zote ambazo hatuna uhakika wa kushinda, ni kupoteza fedha na muda kuendesha kesi ambazo mwisho wake wenyewe tunaona hatutoshinda.
Maelekezo mengine ni kwamba TAKUKURU iharakishe uchunguzi ambao Rais Samia aliagiza ufanyike kwenye Mamlaka ya Bandari nchini TPA, lakini pia iongeze juhudi za haraka kufikisha kesi za rushwa mahakamani kwa sababu hakuna kesi nyingi zilizopelekwa mahakamani badala yake kumekuepo na majadiliano nje ya mahakama,” Amesema Mchengerwa.
Ametoa pia onyo kwa maafisa utumishi wote nchini kuhakikisha wanasimamia na kutatua changamoto za watumishi nchi na yeyote ambaye atashindwa kutekeleza majukumu yake ipasavyo hatosita kumuagiza Katibu Mkuu Utumishi kumuondoa kwenye nafasi hiyo.
” Haiwezekani watumishi wapate changamoto kwenye nafasi zao halafu kuna Maafisa Utumishi, niwatake maafisa utumishi wote kushughulika na changamoto za watumishi nchini na atakayeshindwa tutamuondoa kwenye nafasi hiyo,” Amesema Mchengerwa.
Kwa upande wake, Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi amesema kuwa, ofisi inaendelea na mchakato wa kuanzisha huduma ya CALL CENTRE itakayotoa fursa kwa watumishi na wananchi kupiga simu na kutuma ujumbe ili kutatuliwa kero na malalamiko yao ya kiutumishi.
Mhe. Ndejembi ameahidi kuwa, atashirikiana na Idara ya TEHAMA Serikalini kuandaa mfumo rafiki utakaowawezesha watumishi wa umma nchini kuwasilisha kero na malalamiko yao ili yafanyiwe kazi kwa wakati.