Mratibu wa Jinsia na Lishe kutoka Asasi kilele ya sekta binafsi inayojihusisha na kuendeleza tasnia ya horticulture hapa nchini ijulikanayo kama TAHA, Salome Stephen, akitoa mafunzo ya lishe bora kwa wanawake na baadhi ya wanaume wa kijiji cha Mnang’ana Kata ya Sepuka wilayani Ikungi mkoani Singida juzi.
Wanawake na baadhi ya Wanaume wa Kata ya Kipumbwiko wilayani Ikungi mkoani Singida wakiwa katika picha ya pamoja baada ya kupatiwa juzi mafunzo ya lishe bora kwa watoto wao kutoka Asasi kilele ya sekta binafsi inayojihusisha na kuendeleza tasnia ya horticulture hapa nchini ijulikanayo kama TAHA.
Wanawake na baadhi ya Wanaume wa Kijiji cha Mnang’ana Kata za Sepuka wilayani Ikungi mkoani Singida wakiwa katika picha ya pamoja baada ya kupatiwa mafunzo ya lishe bora kwa watoto wao kutoka Asasi kilele ya sekta binafsi inayojihusisha na kuendeleza tasnia ya horticulture hapa nchini ijulikanayo kama TAHA.
Na Dotto Mwaibale, Singida
WANAWAKE zaidi ya 300 wa Kata za Sepuka, Irisya na Kipumbwiko wilayani Ikungi mkoani Singida wamepata mafunzo ya lishe bora kwa watoto kutoka Asasi kilele ya sekta binafsi inayojihusisha na kuendeleza tasnia ya horticulture hapa nchini ijulikanayo kama TAHA.
Mafunzo hayo yametolewa na Asasi hiyo kwa ufadhili wa UN WOMEN pamoja na Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi lengo likiwa kuwaepusha watoto na udumavu unaosababishwa na ukosefu wa lishe bora.
Akizungumza kwa nyakati tofauti na wanawake hao wakati akitoa mafunzo hayo Mratibu wa Jinsia na Lishe kutoka TAHA, Salome Stephen alisema lishe bora kwa watoto ni muhimu sana kwa ukuaji wao tangu wakiwa tumboni mwa mama zao.
Stephen alisema mafunzo hayo yalilenga kuangalia mambo mawili moja likiwa ni ulishaji bora wa watoto na pili ni namna bora ya utayarishaji wa mbogamboga na umuhimu wa ulaji wake.
Akizungumzia msingi wa lishe bora alisema unapatikana kutoka katika makundi matano ya chakula la kwanza likiwa ni vyakula vinavyo tokana na nafaka, mizizi pamoja na ndizi za kupika.
Alitaja kundi la pili kuwa ni la vyakula asili ya wanyama, samaki na jamii ya mikundekunde ambayo ni maharagwe, mbaazi, choroko, njugu, dengu na njegere.
Alitaja kundi la tatu kuwa ni la mbogamboga na la nne ni la matunda ya aina mbalimbali.
Stephen alitaja kundi la tano kuwa ni la vyakula vya mafuta, sukari na asali ambapo kwenye mafuta ni zile mbegu zote kama karanga, alizeti na za maboga.
Akizungumzia namna bora ya kuwalisha watoto kuanzia chini ya miezi sita, Stephen alisema chakula pekee kinachotakiwa ni maziwa ya mama.
” Maziwa ya mama ndio chakula sahihi kinachofaa kwa mtoto chini ya miezi sita kwa ajili ya ukuaji bora kwa mwili na akili” alisema Stephen.
Alitaja sababu nyingine ya mtoto kupata maziwa ya mama yake ndani ya miezi hiyo kuwa yanamsaidia kupata kinga ya mwili na kwamba mama anaweza kumnyonyesha mtoto wake kwa muda huo pasipo kumpa kitu chochote.
Alisema changamoto kubwa waliyonayo wakina mama ni kukosa ufahamu wa namna gani ya kunyonyesha na wale vyakula gani ili maziwa yaendelee kutoka.
” Ili maziwa ya mama yaendelee kutoka anapaswa kunyonyesha mara nyingi zaidi kwani mwili wa binadamu unavichocheo vya kutengeneza maziwa.” alisema Stephen.
Alitaja changamoto nyingine kuwa ni wakina mama kunyonyesha watoto wao haraka haraka na hawana muda wa kutosha wa kunyonyesha kwani mtoto anapaswa kunyonya ziwa moja si chini ya nusu saa au anyonye mpaka atakapo shiba.Na ziwa lingine atanyonya wakati mwingine atakaposikia njaa.
Alisema hakuna mahali ambapo pameelekeza lazima mtoto anyonye maziwa yote mawili kwa wakati mmoja na kuwa mtoto hasipo nyonya kwa muda mrefu maziwa yanatabia ya kujitenga, atakapo anza kunyonyeshwa huanza kutoka maziwa ya maji ambayo utuliza kiu ya mtoto na kufuaata maziwa mazito ambayo umfanya mtoto ashibe, hapo hapo mama bila ya kusubiri kidogo ili yaanze kutoka maziwa mazito yenye virutubisho anamwamishia katika ziwa jingine.
Asasi ya TAHA yenye makao yake makuu jijini Arusha imekuwa ikitoa mafunzo kama hayo katika mikoa 25 ya Tanzania ikiwemo Arusha, Mwanza, Manyara, Kilimanjaro,Tanga, Dodoma, Morogoro, Iringa, Njombe, Pwani, Dar es salaam, Lindi, Mtwara, Mara, Simiyu, Mbeya, Songwe, Unguja
( Unguja Kaskazini, Unguja Kusini na mjini Magharibi ) na Pemba ( Pemba Kaskazini na Pemba Kusini ) ,Ikungi-Singida na Shinyanga.