***********************
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema katika mwaka 2020/2021 Serikali imetoa jumla ya leseni 4,652 za utafutaji wa madini, uchimbaji mdogo na uchimbaji wa kati, uchenjuaji na uyeyushaji wa madini na leseni za biashara ya madini.
Waziri Mkuu amesema katika mwaka 2021/2022 Serikali itaendelea kuwapa kipaumbele wachimbaji wadogo kwa kuwatengea na kuwapimia maeneo maalumu ya uchimbaji, kuwapatia leseni na kuwezesha upatikanaji wa teknolojia rahisi na rafiki ya uchimbaji na uchenjuaji wa madini.
Waziri Mkuu ameyasema hayo leo (Jumanne, Aprili 13, 2021) wakati akiwasilisha hotuba ya Mapitio na Mwelekeo wa Kazi za Serikali na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na Ofisi ya Bunge kwa mwaka 2021/2022, Bungeni jijini Dodoma.
Amesema Serikali imeimarisha masoko ya madini, kuzuia utoroshaji wa madini na kufanikisha uwekezaji wa kimkakati katika madini ili Taifa liweze kunufaika zaidi na rasilimali hiyo. “Hadi kufikia Februari 2021, kiasi cha sh. bilioni 399.33 zilikusanywa sawa na asilimia 72.91 ya lengo la sh. bilioni 547.74 kwa mwaka”.
“Ili kuimarisha sekta ya uchimbaji mdogo wa madini, Serikali imeendelea kuwawezesha wachimbaji wadogo kufanya shughuli zao kwa tija kwa kuwatengea maeneo, kuwajengea uwezo na kuwapatia leseni za uchimbaji. Mwaka 2019 sekta ya madini imekua kwa asilimia 17.7 na kuongoza kwenye mauzo ya bidhaa nje ya nchi na uingizaji wa mapato ya Serikali”
Amesema moja ya matokeo mazuri ya uwezeshaji wa wachimbaji wadogo ni kupatikana kwa mawe ya Tanzanite kutoka katika mgodi wa Bw. Saniniu Laizer yenye uzito wa kilo 9.27, 5.103 na 6.33 yakiwa na thamani ya sh. bilioni 12.59.
Waziri Mkuu amesema Serikali imeendelea kuimarisha masoko na vituo vya ununuzi wa madini nchini, ambayo yameongezeka kutoka 28 hadi 39 na vituo vya ununuzi wa madini vimeongezeka kutoka 28 hadi 41 katika kipindi cha Januari 2020 hadi Februari 2021.
Amesema masoko na vituo vya ununuzi wa madini vimekuwa chachu ya kuongeza ushindani na uwazi kwenye biashara ya madini, kudhibiti utoroshaji wa madini pamoja na kuwahakikishia ulinzi na usalama wa kutosha wanunuzi na wauzaji wa madini. Hatua hiyo, imewezesha kuinua uchumi wa wachimbaji wadogo na kuongeza mapato ya Serikali.
Vilevile, Mheshimiwa Majaliwa amesema Serikali itaendelea kuimarisha na kusimamia utendaji kazi wa masoko na vituo vya ununuzi wa madini ili kuhakikisha vinafanya kazi kwa ufanisi zaidi na kuliongezea Taifa mapato.
Wakati huo huo, Waziri Mkuu amesema kwa mwaka 2021/2022 Serikali itaendelea kusimamia utekelezaji wa Mpango wa Usambazaji Umeme Vijijini Awamu ya Tatu (REA III) ili kuhakikisha kuwa vijiji 1,974 vilivyosalia vinapata huduma ya umeme.
Kadhalika, Waziri Mkuu amesema Serikali itasimamia miradi ya uzalishaji na usafirishaji wa umeme, sambamba na utekelezaji wa ujenzi wa bomba la kusafirisha mafuta ghafi kutoka Uganda hadi Tanzania.
Amesema miradi hiyo mikubwa na ya kimkakati inalenga kuliwezesha Taifa kuimarisha upatikanaji wa nishati ya umeme kwa gharama nafuu na uhakika kwa ajili ya kujenga uchumi shindani wa viwanda. Amesema hadi kufikia Machi 2021 utekelezaji wa mradi wa Julius Nyerere wa megawati 2,115 wenye thamani ya trilioni 6.55 umefikia asilimia 45.
Vilevile, Waziri Mkuu amesema ajira zaidi ya 7,000 za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja zimetolewa katika mradi huo. Aidha, mradi wa uzalishaji wa umeme wa Rusumo wa megawati 80 katika maporomoko ya maji ya Mto Kagera umefikia asilimia 75.3.
“Utekelezaji wa miradi ya kuzalisha umeme unakwenda sambamba na ujenzi wa njia za kusafirisha umeme ikiwemo njia ya Msongo wa kV 400 kutoka Rufiji – Chalinze – Kinyerezi na Chalinze – Dodoma na njia ya kusafirisha umeme wa Msongo wa kV 220 kwa ajili ya treni ya mwendo kasi.”
“Nitumie fursa hii kuliarifu Bunge lako tukufu kuwa awamu ya kwanza ya mradi wa ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme wa msongo wa kV 220 kwa ajili ya treni ya mwendo kasi (Dar es Salaam – Morogoro) imekamilika kwa asilimia 99.”