Rais wa Chama cha Walimu Tanzania(CWT) Leah Ulaya,akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) leo April 13,2021 jijini Dodoma juu ya msimamo wao kuhusu uanzishwaji wa Bodi ya Kitaaluma ya walimu.
Makamu wa Rais wa Chama cha Walimu Tanzania(CWT) Dinah Mathaman,akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) leo April 13,2021 jijini Dodoma juu ya msimamo wao kuhusu uanzishwaji wa Bodi ya Kitaaluma ya walimu.
Katibu Mkuu wa Chama cha Walimu Tanzania(CWT) Deus Seif ,akisisitiza jambo kwa waandishi wa habari (hawapo pichani) leo April 13,2021 jijini Dodoma juu ya msimamo wao kuhusu uanzishwaji wa Bodi ya Kitaaluma ya walimu.
Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Walimu Tanzania(CWT) Mwl Japhet Maganga .akielezea msimamo wao kuhusu uanzishwaji wa Bodi ya Kitaaluma ya walimu.
……………………………………………………………………………………
Na.Alex Sonna,Dodoma
Chama cha walimu Tanzania (CWT) kimesema kitaendelea kupinga na kukataa juu ya zoezi la uanzishwaji wa Bodi ya kitaaluma ya Walimu Tanzania kwani bodi hiyo imelenga kumkandamiza Mwalimu badala ya kumsaidia.
Akizungumza na Waandishi wa Habari leo April,13,2021 Rais wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT) Leah Ulaya amesema majukumu yaliyooneshwa kwenye bodi hiyo yanafanana nay ale yanayofanywa na Tume ya Utumishi wa walimu (TSC) iliyopo sasa.
“Mnamo mwaka 2019 ,CWT kilialikwa kutoa maoni kuhusu uanzishwaji wa Bodi hiyo ,kimsingi sisi CWT,tuliikataa kwa nguvu zote baada ya kusoma sheria hiyo tukajiridhisha pasi na shaka kwamba chombo hiki kililenga kumgandamiza mwalimu badala ya kumsaidia ,aidha majukumu yaliyo kwenye bodi hiyo yanafanana na yale yanayofanywa na Tume ya utumishi wa walimu ”amesema Bi.Ulaya
Bi.Ulaya ameelezea kuwa Mnamo Tarehe 12 April,2021 CWT tulialikwa na katibu wa bunge kukutana na kamati ndogo ya Bunge ya sheria juu ya kanuni za uendeshaji wa bodi hiyo ambayo msingi wake ni sheria mama ambayo sisi CWT tulikataa tangu mwanzo,katika kikao hicho cha tarehe 12,April,2021 Chama cha Walimu Tanzania kiliendelea na msimamo wake wa usitishwaji wa chombo hiki na kuimarisha utendaji kazi wa Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC)
Aidha,Rais huyo wa CWT ametaja sababu kadhaa za msimamo kupinga uwepo wa bodi hiyo kuwa ni pamoja na gharama za bodi ambapo uendeshwaji utategemea pesa ya mwalimu mfukoni na ada ni elfu hamsini kwa mwaka pamoja na kupunguza utitiri wa vyombo vinavyomsimamia mwalimu .
“Bodi hii tunaipinga kwa nguvu zote kwa sababu ,uendeshaji wa bodi hii utategemea pesa ya walimu mfukoni kwa ajili ya usajili,leseni na ada kwa mwaka ambayo si chini ya Tsh.50,000/=,gharama za kusikiliza mashauri,gharama za semina ya kila mwaka ambayo ni lazima kuhuisha leseni hiyo ,kushindwa kufanya hivyo mwalimu atanyang’anywa leseni na hivyo kupoteza sifa ya kufundisha na sababu nyinyine ya kuikataa bodi hii ni kupunguza utitiri wa vyombo vinavyomsimamia mwalimu na majukumu yakifanan”amesema.
Kwa upande wake Makamu wa Rais wa Chama hicho Dinah Mathaman amesema kuwa
wanachohitaji walimu kwa sasa ni utulivu na siyo kuwaongezea chombo
ambacho kinaongeza mzigo wa kwa mwalimu.
“Kama tunavyoshuhudia kila mwaka matokeo na taaluma imeendelea kupanda
kutokana na walimu kufanya kazi yao kwa tija,kama ni hizo semina ,mwajiri anapaswa aone umuhimu wa kumnoa mwalimu kwa kumpa semina kutokana na bajeti aliyoiandaa kutoka katika ofisi yake na siyo semina na mafunzo kugharamiwa na mwalimu.”amesema Dinah
Hata hivyo ameiomba Serikali kuendelea kuwaamini kwamba wana taaluma ya kutosha na
wana uwezo mzuri wa kufundisha.
“Walimu tunafanya kazi kwa bidii na ukiangalia ufaulu umekuwa ukiongezeka mwaka hadi mwaka kinachotakiwa ni serikali kuendelea kuamini walimu pamoja na kuwatia moyo “amesema.
Naye Katibu Mkuu wa chama hicho Mwl. Deus Seif amehoji kuwa kuna nini cha ziada anachotakiwa afanye mwalimu wakati ufaulu unaongezeka kila mwaka .
Mwl Seif amesema kuwa,tayari wana TSC ambayo inawasimamia lakini pia inatoa nafasi pana kwa mwalimu kujitetea hata lipotokea tatizo tofauti na bodi ambayo mwalimu akiwa na tatizo itampasa atoke alipo na kuifuata bodi ilipo tena kwa gharama zake.
Aidha Naibu Katibu Mkuu wa CWT Mwl. Japhet Maganga ,amesema hawaikubali
bodi hiyo kwani TSC haijawahi kusema imeshindwa kutekeleza majukumu yake ambayo yanatarajiwa kutekelezwa na Bodi hiyo. pia alisema Bodi hiyo haina manufaa yoyote kwa mwalimu zaidi ya kwenda kumdidimiza mara baada ya kuanza kufanya kazi.