Picha na Muhidin Amri
…………………………………………………………………
Na Muhidin Amri,Mbinga
NAIBU Waziri wa maji Mhandisi Maryprisca Mahundi amesema,serikali itaendelea kutoa fedha kwa ajili ya kujenga miradi ya maji ili kuwaondolea kero wananchi ya kutembea umbali mrefu kutafuta maji kwa matumizi yao ya kila siku.
Naibu Waziri Mahundi ametoa kauli hiyo leo(jana) baada ya kukagua mradi wa maji katika kijiji hicho unaotekelezwa na wakala wa maji vijijini (Ruwasa) na kujengwa na Mamlaka ya maji safi na usafi wa mazingira manispaa ya Songea (Souwasa) .
Naibu Waziri, ameridhishwa na kazi nzuri yenye viwango na ubora wa hali ya juu iliyofanywa na Souwasa katika ujenzi wa mradi huo na kuipongeza Ruwasa kwa matumizi mazuri ya fedha zinazoletwa kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maji katika mkoa wa Ruvuma.
Kwa mujibu wake,kukamilika kwa mradi huo na miradi mingine inayoendelea kutekelezwa na Serikali kupitia wizara ya maji,kutawawezesha wananchi wa kata hiyo na maeneo mengine ya mkoa wa Ruvuma kupata maji ya uhakika na kuondokana na kero ya kutembea umbali mrefu kwenda kufuata maji mbali na makazi yao.
Alisema, mradi wa maji Kipapa na miradi mingine inayojengwa katika vijiji mbalimbali ni moja kati ya juhudi kubwa za serikali zinazolenga kumtua mama ndoo kichwani na kuchochea kukua kwa uchumi wa mtu mmoja mmoja,wilaya,mkoa na taifa.
Amewataka wananchi,kuhakikisha wanatunza miundombinu na miradi ya maji iliyojengwa na ile inayoendelea kujengwa katika maeneo yao ili iweze kudumu na kuharakisha maendeleo yao.
Meneja ufundi wa Mamlaka ya maji safi na usafi wa mazingira manispaa ya Songea Jafari Yahaya alisema, mradi wa maji Kipapa na Mhilo ulianza kutekelezwa mwezi Januari 2020 na kukamilika mwezi Machi 2021 kwa gharama ya shilingi milioni 772,620,779.67 ambapo wizara ya maji imetoa kiasi cha shilingi milioni 647,472,886.33.
Alisema, mamlaka ya maji safi na usafi wa mazingira Songea(Souwasa) ambayo imejenga mradi huo kama fundi, ilipokea maagizo kutoka Wizara ya maji ya kutekeleza ujenzi wa mradi wa maji Kipapa na Mhilo katika Halmashauri ya wilaya ya Mbinga.
Alisema, mradi huo umewanufaisha wakazi 2,167 wa kijiji cha Kipapa na 1,247 wa kijiji cha Mhilo ambapo utekelezaji wake umefikia asilimia 100 ukiwa umegharimu jumla ya shilingi milioni 574,025,204.26 na kufanya kubakiwa na salio la shilingi milioni 73,447,682.07.
Alisema, Souwasa imetekeleza mradi huo kwa kutumia wataalam wa ndani ambapo iliunda timu mbili ikihusisha timu ya ujenzi pamoja na ya usimamizi ili mradi huo utekelezwe kwa ubora unaotakiwa na muda uliopangwa.
Kwa mujibu wake,kutokana na mradi kuwa na fedha za Utekelezaji, Souwasa imeweza kukamilisha kazi hiyo kwa ufanisi na ubora wa hali ya juu.
Alisema, kujengwa kwa mradi huo kwa kutumia mfumo wa force Akaunti na mafundi wa wadogo kumekuwa na mafanikio mengi ikiwemo kuongeza vituo 10 vya ziada vya kuchotea maji kutoka vituo 23 na kubakiza na fedha kiasi cha shilingi milioni 73.447.