Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof Joyce Ndalichako akisikiliza taarifa kutoka Operesheni Kamanda wa mradi huo kutoka Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Meja Philemon Komanya kabla ya kuanza kukagua Maendeleo ya ujenzi wa Shule ya Mfano inayojengwa Iyumbu jijini Dodoma iliyofanyika Leo April 10,2021
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof Joyce Ndalichako akipata maelezo kutoka kwa Afisa wa Jeshi, Kapteni Mturi wakati wa ukaguzi wa ujenzi wa Shule ya Mfano inayojengwa Iyumbu jijini Dodoma,leo April 10,2021.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof Joyce Ndalichako akiwa ameongozana na Naibu Waziri wake Mhe. Omary Kipanga na Naibu Katibu Mkuu, Prof Carolyne Nombo wakikagua ujenzi wa Shule ya Mfano inayojengwa Iyumbu jijini Dodoma, wakati wa ziara hiyo ya kukagua maendeleo ya ujenzi huo iliyofanyika Leo April 10,2021
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof Joyce Ndalichako akitoa maelekezo kwa Mkandarasi Mturi wakati wa ziara yake ya kukagua ujenzi wa Shule ya Mfano inayojengwa Iyumbu jijini Dodoma,ziara hiyo imefanyika leo April 10,2021.
Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia,Mhe.Omary Kipanga akipima urefu wa nguzo zilizopo kwenye jengo la Bweni ya Shule ya Mfano inayojengwa Iyumbu jijini Dodoma wakati wa ziara ya kukagua ujenzi wa shule hiyo iliyofanyika leo April 10,2021 .
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof Joyce Ndalichako akiwa na Naibu Waziri wake Mhe. Omary Kipanga wakiendelea na ukaguzi wa ujenzi wa Shule ya Mfano inayojengwa Iyumbu jijini Dodoma, wakati wa ziara hiyo ya kukagua maendeleo ya ujenzi huo iliyofanyika Leo April 10,2021
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof Joyce Ndalichako akimueleza jambo Mhandisi kutoka Ardhi Nicodeus Ngaya wakati wa ziara yake ya kukagua ujenzi wa Shule ya Mfano inayojengwa Iyumbu jijini Dodoma, wakati wa ziara hiyo ya kukagua maendeleo ya ujenzi huo iliyofanyika Leo April 10,2021
Mafundi wakiendelea na shughuli za ujenzi wa Shule ya Mfano inayojengwa Iyumbu jijini Dodoma.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof Joyce Ndalichako,akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kumaliza ziara yake ya kukagua ujenzi wa Shule ya Mfano inayojengwa Iyumbu jijini Dodoma iliyofanyika Leo April 10,2021
…………………………………………………………………………………….
Na.Alex Sonna,Dodoma
WAZIRI wa Elimu Sayansi na Teknolojia, Prof Joyce Ndalichako,amesema kuwa shule mpya ya Sekondari ya Mfano iliyopo Iyumbu Jijini Dodoma itakuwa na uwezo wa kuchukua wanafunzi 1,000 kwa wakati mmoja pindi itakapokamilika wavulana kwa wasichana.
Hayo ameyasema leo April 10,2021 mara baada ya kufanya ziara ya kukagua Maendeleo ya ujenzi wa Shule hiyo inayojengwa na Serikali kwa gharama ya shilingi Bilioni 17.1 ambayo inatarajia kukamilika Februari 22 mwaka 2022.
Waziri Ndalichako amesema maana ya shule hiyo kuwa ya mfano ni kwa sababu itakua na miundombinu yote inayotakiwa huku ikiwa na ubora wa hali ya juu, walimu wa kutosha lakini wanafunzi watakaoletwa hapo ni wale wenye uwezo wa kawaida, lengo ni kutaka kuona namna gani walimu au ubora wa shule unavyoweza kunyanyua uwezo wa mwanafunzi.
” Shule ikikamilika tutawaleta hapo wanafunzi wenye uwezo wa kawaida halafu tutaona kama walimu waliopo hapa ni bora, miundombinu iliyopo ni bora, kutakuwa na sababu yoyote ya wanafunzi kufanya vibaya? Tunataka tuone namna walimu watakavyotumia miundombinu hii bora kukuza kiwango cha ufaulu kwa wanafunzi wao,” Amesema Prof. Ndalichako.
Aidha amesema kuwa lengo la serikali chini ya Rais Samia Suluhu Hassan ni kuhakikisha inasimamia na kukuza kikamilifu kiwango cha ufaulu kwa wanafunzi nchini ili kuweza kuzalisha kundi kubwa la wasomi na watalaamu ambao watakua na tija kwa Taifa.
Hata hivyo Waziri Ndalichako ameitaka Kampuni ya ujenzi ya Suma JKT kuhakikisha inazingatia vigezo na michoro ya ujenzi wa shule hiyo ili kuweza kuifanya kuwa miongoni mwa shule bora na nzuri nchini.
”Niwashukuru Suma JKT kwani tumekuwa na tumekuwa na uhusiano nao kwa muda mrefu naamini kazi hii mtaitekeleza kwa ubora unaotakiwa na mtaifanya kwa uzalendo mkubwa, rai yangu kwenu najua kuna mkataba wa kazi lakini niwaombe mjitahidi kukamilisha Januari ili wanafunzi waanze mwaka wa masomo hapa,,” Amesema Prof Ndalichako.
Aidha Prof.Ndalichako amewataka wahandisi wa wizara hiyo kuwa na utaratibu wa kutembelea eneo la mradi kujionea hali halisi na kutoa ushauri kwa wizara na Mkandarasi pale wanapoona changamoto yoyote na siyo kufanya kazi kwa mazoea bila kuwa msaada kwa serikali.
” Nitoe maelekezo kwa wahandisi wetu kuacha kufanya kazi kwa mazoea, huu mradi unagharimu mabilioni ya fedha za walipa kodi wa kitanzania, ni vema tukatumia fedha hizi kwa uangalifu na kwa umakini ili tuweze kukamilisha mradi huu kwa ubora unaotakiwa.
Awali Kwa Operesheni Kamanda wa mradi huo kutoka Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Meja Philemon Komanya amesema kuwa watatekeleza maelekezo yaliyotolewa kwa ufanisi na wana imani kubwa ya kukamilisha mradi wa shule hiyo katika muda uliopangwa ukiwa na ubora ule ule unaotakiwa.
Meja Komanya amesema mpaka sasa ujenzi wa shule hiyo umefikia asilimia 28 ambapo majengo yanayojengwa ni pamoja na madarasa, mabweni ya wavulana na wasichana, Bwalo la chakula, Maabara, nyumba za walimu.