Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa TAKUKURU Mkoa wa Dodoma Bw. Sosthenes Kibwengo,akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) Leo April 10,2021 jijini Dodoma wakati akitoa taarifa ya kumshikilia Luka Nkini (38) mkazi wa Airpot jijini Dodoma kwa tuhuma za utapeli na kujipatia manufaa kinyume na sheria za nchi.
………………………………………………………………………..
Na.Alex Sonna,Dodoma
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa TAKUKURU Mkoa wa Dodoma inamshikilia Bw. Luka Nkini (38) mkazi wa Airpot jijini Dodoma kwa tuhuma za utapeli na kujipatia manufaa kinyume na sheria za nchi.
Pia TAKUKURU imefanikiwa kuokoa zaidi ya shilingi milioni mia saba nan ne (704) nyumba pamoja na kiwanja kimoja mali ambazo zilichepushwa kinyume na makusudio.
Akizungumza na waandishi wa Habari Leo April 10,2021 Ofisi kwake Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Dodoma Bw. Sosthenes Kibwengo, amesema walipokea taarifa kuwa mtuhumiwa alikuwa akijifanya mganga wa kienyeji na mjukuu wa babu miti mingi kutoka Kigoma na kujipatia mali kutoka kwa wananchi.
“Uchunguzi wetu wa awali umeonyesha kwamba mtuhumiwa amejipatia manufaa asiyostahili kutoka kwa akina mama 10 kuwa anauwezo wa kuongeza mara dufu fedha na vitu walivyo mpa” amesema Kibwengo.
Aidha Kibwengo amebainisha kuwa mtuhumiwa mara amekuwa akitumia sharti la ngono kwa baadhi ya akina mama ili kuwafanikishia wanayohitaji na amekuwa akifanya uhalifu huo katika Mikoa ya Dodoma, Arusha na Kilimanjaro.
Ameongeza kuwa “ hadi sasa tumepata ushahidi kuwa mtuhumiwa amejipatia zaidi ya shilingi milioni mia moja na tano (105), viwanja viwili, mashamba mawili, vifaa vya kielectroniki na fanicha mbalimbali na amekiri kuhusika” amesema.
Amesema mtuhumiwa amewataja washiriki wenzake kuwa ni Husain Mvungi (44) mkazi wa himo Kilimanjaro ambaye amekamatwa na amekiri kuhusika, na bw. Gaburiel Munuo, mkazi wa Sanya juu Siha ambaye bado hajakamatwa na kutaka ajisalimishe haraka kwenye ofisi yoyote ya TAKUKURU.
Amesema katika robo ya kwanza ya Januari hadi March 2021 wamefamikiwa kuokoa zaidi ya shilingi 704, nyumba moja na kiwanja kimoja zikiwa ni mali zilizochepushwa kinyume na makusudio ikiwa ni malipo ya tozo za halmashauri yaliyokuwa mikononi mwa watendaji, malipo zidifu yasiyostahili fedha zilizokuwa zichepushwe.
Fedha nyingine ni makato ya watumishi ambayo hayakuwasilishwa kwenye mfuko wa taifa wa hifadhi ya jamii(NSSF) kwa mda mrefu, amesema milioni 27 kati ya fedha zilizookolewa zimetokana na ufuatiliaji wa miradi miwili ya maji.
“miradi miwili ya maji ambapo tulibaini malipo batili kufanywa kwa wakandarasi wa miradi ya vijiji vya Goima Wilayani Chemba na Mundemu Wilaya ya Bahi ambapo kazi zilizoainishwa hazikufanyika” amesema.
Kuhusu malipo ya NSSF Bw. Kibwengo amesema “ ufuatiliaji wetu umeonyesha kuwa ni kweli baadhi ya waajiri hawawasilishi aidha sehemu au makato yote yanayopaswa kulipwa NSSF, na kwa kushirikiana na NSSF Mkoa wa Dodoma tumefanikiwa kudhibiti zaidi ya milioni 214 kutoka kwa waajili 30” amesema.
Aidha amebainisha kuwa TAKUKURU Mkoa wa Dodoma wameendelea na kuwa karibu na wananchi ambapo ofisi zao zote za Wilaya zilitenga siku moja ya kutembelea na kusikiliza kero za wananchi( TAKUKURU inayotembea) ambapo walisikiliza kero za wananchi na kuzipatia ufumbuzi.