Katibu Mkuu, Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Allan Kijazi akizungumza na Maafisa Utalii waliohudhuria Mafunzo ya Usajili wa Huduma za Malazi katika Mfumo wa Accommodation Services in Tanzania –(AserT) yaliyofanyika katika ukumbi wa TANAPA jijini Dodoma leo.
Katibu Mkuu, Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Allan Kijazi akizungumza na Maafisa Utalii waliohudhuria Mafunzo ya Usajili wa Huduma za Malazi katika Mfumo wa Accommodation Services in Tanzania –(AserT) yaliyofanyika katika ukumbi wa TANAPA jijini Dodoma leo.
Baadhi ya Maafisa Utalii wakimsikiliza Katibu Mkuu, Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Allan Kijazi (hayupo pichani) alipokuwa akifunga Mafunzo ya Usajili wa Huduma za Malazi katika Mfumo wa Accommodation Services in Tanzania –(AserT) yaliyofanyika katika ukumbi wa TANAPA jijini Dodoma leo.
Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Utalii, Philip Chitaunga (katikati) akitoa neno la shukrani kwa niaba ya washiriki wa mafunzo ya Usajili wa Huduma za Malazi katika Mfumo wa Accommodation Services in Tanzania –(AserT) baada ya Katibu Mkuu, Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Allan Kijazi (kushoto) kufunga mafunzo hayo yaliyofanyika katika ukumbi wa TANAPA jijini Dodoma leo.
************************************
Na Happiness Shayo – Dodoma
Serikali iko katika mikakati ya kuhakikisha idadi ya watalii inaongezeka kutoka milioni 1.5 kabla ya Covid 19 hadi kufikia watalii milioni 5 ifikapo mwaka 2025 na pia kuongeza mapato yatokanayo na utalii kutoka dola milioni 2.6 hadi kufikia dola milioni 6 mwaka 2015.
Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu, Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Allan Kijazi alipokuwa akifunga mafunzo ya Usajili wa Huduma za Malazi katika Mfumo wa Accommodation Services in Tanzania –(AserT) yaliyofanyika katika ukumbi wa TANAPA jijini Dodoma leo.
Dkt. Kijazi ameiagiza Idara ya Utalii kuwa kinara katika kuongoza shughuli za Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kuhakikisha lengo la Serikali la kuongeza idadi ya watalii na kuongeza mapato yatokanayo na utalii linafikiwa.
“ Mafunzo haya ni moja ya mkakati wa Wizara hii ya kuhakikisha tunafikia lengo la Serikali la kuongeza idadi ya watalii na kuongeza mapato yatokanayo na utalii nchini” Dkt. Kijazi amefafanua.
Aidha, Dkt. Kijazi ameongeza kuwa moja ya changamoto iliyopo ni kutokuwapo kwa takwimu sahihi za idadi ya maeneo yanayotoa huduma za malazi nchini hivyo kupelekea makusanyo ya mapato yatokanayo ya wageni kuwa kidogo kuliko hali halisi.
“Nimepewa taarifa kwamba kumbukumbu za maeneo yenye huduma za malazi zinafikia 1800, lakini kiuhalisia huduma za malazi zinatolewa katika maeneo mengi nchini” Dkt. Kijazi amesisitiza.
Ameongeza kuwa idadi ndogo ya huduma za malazi zilizopo zinazotumiwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kukusanya mapato ni ishara ya Serikali kupoteza mapato katika maeneo mengi ambayo bado hayajaorodheshwa.
Amefafanua kuwa mafunzo ya Usajili wa Huduma za Malazi katika Mfumo wa Accommodation Services in Tanzania –(AserT) ni muhimu kwa sababu yatasaidia katika zoezi la utambuzi na uhakiki wa huduma za malazi kufanyika kwa ufanisi mkubwa ili Serikali iweze kupata matokeo yanayotarajia na pia yatasaidia kuwapo kwa kumbukumbu sahihi za watalii wanaopokelewa katika maeneo mbalimbali nchini.
Dtk. Kijazi amewataka Maafisa watakaoshiriki katika zoezi la utambuzi na uhakiki wa huduma za malazi kuwa na nidhamu, uaminifu na uadilifu wa hali ya juu ili kufanikisha zoezi hilo.
“Hatutegemei mtumie rasilimali za Wizara halafu mje na takwimu ambazo si sahihi. Tusije tukaona kwamba hii ndio fursa ya kwenda kutembea yaani unaenda maeneo mawili halafu unaishia mtaani” Dkt. Kijazi amesema.
Pia ametoa onyo la kuwachukulia hatua za kinidhamu Maafisa watakaobainika kufanya kazi kwa mazoea.
“ Tukigundua kwamba haufanyi kazi yako kwa umakini tutakuchukulia hatua kwa sababu hii ni fursa pekee ya kutuwezesha sisi kupata takwimu sahihi kuhusu maeneo yenye huduma za malazi” Dkt. Kijazi amesema.
Naye, Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Utalii, Philip Chitaunga kwa niaba ya washiriki wa mafunzo hayo, ameahidi kutekeleza maagizo yote ya Katibu Mkuu, Dkt. Kijazi na kwamba kila mshiriki wa zoezi utambuzi na uhakiki wa huduma za malazi atapimwa kwa matokeo kwa sababu ni kazi muhimu sana kwa Wizara na kwa nchi.
Mmoja wa washiriki wa Mafunzo hayo ambaye ni Afisa Utalii Mwandamizi, Franklin Mwenyembegu, amesema kuwa mafunzo hayo yamegawanyika katika sehemu mbili ambapo sehemu ya kwanza iligusia mfumo wa Kieletroniki wa Tathmini ya Upangaji wa Huduma za Malazi na Chakula katika ubora wa Madaraja (Accommodation Services in Tanzania – AserT) utakaotumika na wamiliki wa huduma za malazi kufanya tathmini binafsi (Self-Assessment) ya huduma wanazozitoa kwa mujibu wa vigezo na hivyo kupanga madaraja ya ubora wa nyota wao wenyewe kabla ya kuthibitishwa na wathamini wa Serikali.
Amesema sehemu ya pili ya mafunzo hayo ilihusisha namna bora ya uchukuaji wa taarifa za huduma za malazi nchi nzima zitakazosaidia katika ukusanyaji wa tozo ya maendeleo ya utalii.
Mafunzo hayo yamehudhuriwa na Maafisa Utalii kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii na Maafisa Utalii kutoka Ofisi za Utalii za Kanda ya Dar es Salaam, Arusha, Iringa na Mwanza