Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Ummy Mwalimu,akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) leo April 9,2021 jijini Dodoma wakati akitoa maelezo kuhusu ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), iliyotolewa juzi kwa umma ikionesha Halmashauri nane zilipata hati chafu huku 53 zikipata hati zenye mashaka.
…………………………………………………………………………………….
Na.Alex Sonna,Dodoma
Kutokana baadhi ya halmashauri kupata hati chafu na nyingine kupata hati isiyoridhisha katika ripoti ya mkaguzi na mdhibiti wa hesabu za Serikali CAG, Waziri ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mhe. Ummy Mwalimu ametoa maelekezo 10 kwa mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa.
Waziri Ummy ametoa maagizo hayo Leo April 9,2021 Jijini Dodoma wakati akizungumza na waandishi wa habari ambapo amezitaja Halmashauri nane zilizopata hati mbaya kuwa ni Halmashauri za Wilaya za Itigi, Singida, Shinyanga, Momba, Igunga, Sikonge, Urambo na Manispaa ya Tabora.
Waziri Ummy amesema kutokana na Wakurugenzi kuwa na wajibu wa kuhakikisha kuwa taarifa za hesabu za mwisho zinaandaliwa kwa usahihi, ameshauri Mamlaka ya uteuzi wao kuchukua hatua stahiki kadiri ya itakavyoona inafaa.
“Ofisi za Wakuu wa Mikoa na Mamlaka za Nidhamu zihakikishe kuwa hatua stahiki zinachukuliwa kwa Wakuu wa Vitengo vya Ukaguzi wa Ndani wa Halmashauri 54 ambao hawakukagua taarifa za hesabu za mwisho kabla ya kuziwasilisha kwa CAG,”amesema Waziri Ummy.
Amesema Wakuu wa Mikoa wahakikishe Wanashiriki Mikutano Maalum ya Mabaraza ya Madiwani katika Halmashauri kujadili taarifa za CAG na kusimamia utekelezaji wa mapendekezo yote ya CAG pamoja na kuratibu kufanyika kwa uhakiki wa majibu ya hoja zote za ukaguzi na Ofisi yake ipate taarifa za utekelezaji na mpango kazi kabla ya Mei 31, mwaka huu.
“Halmashauri zilizopata hati mbaya na hati zenye shaka ziwabainishe, Wataalam wa Fedha wenye CPA (T) ambao walisaini taarifa za hesabu za mwisho kuthibitisha kwamba taarifa hizo ni sahihi na hazina makosa wafikishwe bodi ya Wahasibu na Wakaguzi (NBAA) ili wachukuliwe,” amesema.
Pia ameagiza kupitiwa upya mfumo wa kielektroniki wa ukusanyaji wa mapato ya Halmashauri kwa lengo la kufanyia kazi dosari zote zilizobainishwa na CAG kuhusu mfumo huo na pia vituo vyote vya kutolea Huduma za Afya vinavyojengwa sasa, vihusishe uwekaji wa mfumo wa kielektroniki wa GoTHOMIS.
Waziri Ummy pia amebainisha kuwa anakusudia kuandaa mikataba ya ufanisi kwa Wakuu wa Mikoa ili kuongeza uwajibikaji katika maeneo yao ya kazi.
Kuhusu kutorejeshwa kwa mikopo inayotolewa kwa Vikundi vya Wanawake, Vijana na Watu wenye Ulemavu, Waziri huyo ameagiza Halmashauri kusimamia utekelezaji wa kanuni za utoaji na usimamizi wa mikopo za mwaka 2019 na kuchukua hatua stahiki kwa kikundi kitakachoshindwa kurejesha mkopo.