Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Dorothy Gwajima akiongea na kutoa maelekezo kadhaa kwa watumishi wa Wizara hiyo wakati wa hafla ya kuwapokea viongozi wapya jijini Dodoma.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Prof. Abel Makubi akitoa neno la shukrani kwa watumishi wa Wizara ya Afya (Hawapo pichani) wakati akipokelewa katika Wizara hiyo Jijini Dodoma.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Dkt. Abel Makubi akipokea kadi ya kumtakia heri katika majukumu yake mapya kutoka kwa Waziri Dkt. Gwajima na Naibu Waziri Dkt. Mollel katika hafla ya mapokezi jijini Dodoma.
Mganga Mkuu wa Serikali Dkt. Aifello Sichalwe akiongea mbele ya Watumishi wa Wizara ya Afya katika ukumbi mdogo wa Wizara uliopo Area D jijini Dodoma.
******************************
Na WAMJW-Dodoma
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Dorothy Gwajima amewataka watumishi wa Wizara hiyo pamoja na Sekta ya Afya kwa ujumla kukubali mabadiliko ya uongozi na kuangalia namna ya uendeshaji ili kuzidisha uweledi katika maeneo yao ya kazi.
Waziri Gwajima amesema hayo leo wakati wa hafla fupi ya kuwapokea viongozi wapya walioteuliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan na kuapishwa mapema wiki hii.
Viongozi hao ni Katibu Mkuu Prof. Abel Makubi pamoja na Mganga Mkuu wa Serikali Dkt. Aifello Sichwale ambao leo wameripoti rasmi ofisi za Wizara jijini Dodoma.
“Tuimalishe mifumo ya kufanya kazi pamoja kama tulivyoimarisha mifumo ya kufanya na mataifa mengine, tuna makubaliano ya kufanya kazi pamoja katika kutekeleza dira ya afya duniani. Tunashindwaje kuwa na makubaliano ya kufanya kazi pamoja katika kutekeleza sera yetu?”. amehoji Waziri Gwajima.
Waziri Gwajima ameongeza kuwa kuna watu huwa wanaanzisha ajenda ambazo kimsingi Wizara inakua haina haja nazo huku akitoa onyo kwa watumishi wa Wizara ya Afya pamoja na Ofisi ya Rais TAMISEMI kutoandaa vikao ambavyo ajenda zake zinakua siyo za kueleweka.
Aidha, Waziri Gwajima ameagiza wakurugenzi wa idara zilizopo Wizarani kutengeneza vikao vya mashirikiano ili kuwezesha mnyororo wa kutoa huduma za afya kufanyika kwa uweledi na kuepusha malalamiko kutoka kwa wananchi.
Naye Naibu Waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollel amesema ushirikiano baina ya viongozi mbalimbali wa Wizara pamoja na taasisi zake ni chachu kubwa ya kuleta mabadiliko ya kiutendaji na kuongeza kuwa viongozi hao wote ni washauri wa Mhe. Waziri wakiwa na lengo la kuboresha huduma za afya nchini.
Kwa upande wake Katibu Mkuu Prof. Abel Makubi amesema ana imani kubwa kuwa wataalamu waliopo katika Sekta ya Afya wanaweza kufanya kazi nzuri katika kusimamia afya za Watanzania na kuweza kutimiza matarajio ya Rais. Lakini pia Prof. Makubi amewashukuru watumishi wa afya kwa kazi kubwa na hakusita kuomba ushirikiano kutoka kwao ili kuweza kuitekeleza sera ya afya ambayo iliandaliwa na Wizara.
Vilevile Mganga Mkuu wa Serikali Dkt. Aifello Sichwale akitoa Shukrani zake mbele ya Waziri Gwajima amebainisha maeneo yake kadhaa ya utendaji ili kuboresha sekta ya afya.
Ametaja maeneo hayo ni Uongozi, Uwajibikaji na Utawala bora. Eneo la pili ni kuhusu masuala ya fedha, eneo la tatu ni kuhusu bidhaa za afya, Nne ni Rasilimali watu, Tano ni Masuala ya TEHAMA, Sita ni Huduma kwa Mteja, Saba ni kuhusu masuala ya utafiti na la Nane ni Kuhusu ushirikiano na Sekta Binafsi.