Katibu Mkuu Wizara ya Katiba na sheria Prof. Sifuni Mchome ,akizungumza wakati akifungua Kikao cha pili cha Baraza la wafanyakazi wa ofisi ya wakili Mkuu wa Serikali unaofanyika Leo April 9,2021 jijini Dodoma,kushoto kwake ni Wakili Mkuu wa Serikali Gabriel Malata na kushoto ni Naibu Wakili Mkuu wa Serikali Bw.Boniphance Luhende.
Wakili Mkuu wa Serikali Gabriel Malata,akitoa utangulizi wa ufunguzi wa Kikao cha pili cha Baraza la wafanyakazi wa ofisi ya wakili Mkuu wa Serikali unaofanyika leo April 9,2021 jijini Dodoma (katikati) ni Katibu Mkuu Wizara ya Katiba na sheria Prof. Sifuni Mchome na kulia ni Naibu Wakili Mkuu wa Serikali Bw.Boniphance Luhende.
Mwenyekiti wa TUGHE Tawi la Wakili Mkuu wa Serikali Bw.Mtani Songorwa ,akitoa neno la shukrani kwa niaba ya washiriki mara baada ya Katibu Mkuu Wizara ya Katiba na sheria Prof. Sifuni Mchome,kufungua Kikao cha pili cha Baraza la wafanyakazi wa ofisi ya wakili Mkuu wa Serikali kilichofanyika Leo April 9,2021 jijini Dodoma.
Baadhi ya washiriki wa kikao hicho wakimsikiliza Katibu Mkuu Wizara ya Katiba na sheria Prof. Sifuni Mchome (hayupo pichani) wakati akifungua Kikao cha pili cha Baraza la wafanyakazi wa ofisi ya wakili Mkuu wa Serikali kilichofanyika Leo April 9,2021 jijini Dodoma.
Katibu Mkuu Wizara ya Katiba na sheria Prof. Sifuni Mchome akiwa katika picha ya pamoja na washiriki mara baada ya kufungua Kikao cha pili cha Baraza la wafanyakazi wa ofisi ya wakili Mkuu wa Serikali kinachofanyika Leo April 9,2021 jijini Dodoma.
…………………………………………………………………………………………….
Na.Alex Sonna,Dodoma
Katibu Mkuu Wizara ya Katiba na sheria Prof. Sifuni Mchome amewataka watumishi wa ofisi ya wakili Mkuu wa Serikali kuzingatia ushirikishwaji katika ngazi zote sambamba na kufanya kazi kwa uwazi, huku wakifuata miiko ya kazi yao.
Prof. mchome ameyasema hayo leo April 9,2021 jijini Dodoma wakati akifungua Kikao cha pili cha Baraza la wafanyakazi wa Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali kilichofanyika Leo April 9,2021 jijini Dodoma amesema kuwa kutokana na unyeti wa ofisi hiyo inahitajika kila mtumishi kufanya kazi wa weredi huku wakilenga kutafuta matokeo.
“mfuate maadili ya kazi yenu maadili yanakusaidia katika kutekeleza majukumu yako kikamilifu, sekta yenu ni muhimu sheria ikisimama na hata nchi itatulia” amesema Prof. Mchome.
Amesema mabaraza ya wafanyakazi ni muhimu sana katika maeneo ya kazi kwa sababu huko ndiko ushirikishwaji utafanyika ni muhimu kila taasisi iwe na mabaraza hayo ambayo yapo kwa mujibu wa sheria.
“Serikali itahakikisha taasisi zake zote zinatekeleza takwa hili la sheria la kuwa na mabaraza ya wafanyakazi huku ndiko kutafanyika ushirikishwaji katika mambo mbalimbali kwa watumishi katika ngazi zote” amesema.
Amesema katika majukumu yao wafanye kazi wakilenga kupata matokeo chanya katika kutafuta ushindi katika kesi mbalimbali ambazo wanazisimamia katika ofisi zao zilizopo katika maeneo mbalimbali hapa nchini.
Amewataka kujenga utaratibu wa kufanya tathmini za mara kwa mara katika kazi wanazozifanya ili kuona namna ya kuboresha kazi zao kwani bila tathmini hawawezi kupata kile walichokusudia katika sekta ya sheria hapa nchini.
Ameongeza kuwa “mkasikilize kero za wananchi tunakofanya ziara huko mikoani malalamiko ni mengi, naamini huko mnaofisi zenu mkashughulikie hayo malalamiko ni mengi sana” amesema.
Aidha amewataka wataalamu hao kwendana na kasi ya sasa na sio kufanyakazi kwa mazoea kwani kwa sasa nchi imeingia katika uchumi wa kati hivyo nao wabadilishe namna ya ufanyaji kazi ili kuendana na kasi ya uchumi wa kati ili kama nchi kupata mafanikio zaidi.
Awali Wakili Mkuu wa Serikali ambaye pia ni mwenyekiti wa baraza hilo bw. Gabriel Malata amesema kikao hicho ni cha pili kwa mwaka wa fedha 2020 -2021, ambao wanakutana kwa ajili ya kujadili mambo mbalimbali yanayohusu ofisi hiyo.
Pia amebainisha kuwa ofisi ya wakili Mkuu wa Serikali ilianzishwa Feb, 12, 2018 na aliyekuwa Rais wa awamu ya tano hayati Dkt John Magufuli na kupewa jukumu la kuendesha, kuratibu, na kusimamia mashauri mbalimbali yanayohusu Serikali na taasisi zake.
Amesema katika kipindi cha mwezi julai 2020, hadi Feb, 2021 ofisi hiyo imeshughulikia jumla ya mashauri 3715, kati ya hayo mashauri ya madai ni 3625 na 90 ni ya usuluhishi, jumla ya mashauri 451 kati ya 3715 yaliendeshwa na kumalizika.
Kati ya mashauri hayo 422 ni ya madai ambayo yanajumuisha mashauri 418 ya madai ya ndani ya nchi yakiwamo 13 ya uchaguzi na mashauri manne (4)ya madai ya nje ya nchi, na kukamilika kwa mashauri hayo kumepelekea kuokoa zaidi ya shilingi bilioni 643.7, ambazo zingelipwa na serikali kama ingeshindwa.
Aidha amesema ofisi hiyo inakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwamo ya kukosa muundo wa uendeshaji wa ofisi hiyo ambapo kwa sasa wanatumia muundo wa ofisi ya mwanasheria mkuu wa serikali.