****************************************
Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt. Damas Ndumbaro ametembelea Kitalu cha Uwindaji wa Kitalii cha Lake Natron East kilichopo Wilayani Longido mkoani Arusha kilichokuwa kikimilikiwa na Kampuni ya Uwindaji wa Kitalii ya Green Miles Safari Ltd kwa lengo la kukagua Kambi ya mwekezaji huyo, kusikiliza kero na maoni ya wananchi wa vijiji vinavyozunguka kitalu hicho.
Ziara hiyo ya kikazi inafuatia Kampuni ya Green Mile iliyokuwa ikimiliki kitalu hicho na baadaye kufutiwa leseni mwaka 2019 kuwasilisha ombi la kufanyika kwa mapitio ya uamuzi uliotolewa.
Akiwa katika eneo la kitalu hicho ,Dkt. Ndumbaro amesema lengo la amejionea hali halisi katika eneo hilo na kuwaahidi wananchi kuwa maamuzi kuhusu suala hilo yatafanyika hivi karibuni baada ya kukamilika kwa taratibu za kusikiliza pande zote zenye maslahi na kitalu hicho.
“Nawaahidi wananchi, Serikali imewasikiliza wadau wote wanaohusika na suala hili wakiwemo viongozi wenu katika ngazi zote na wale wa wilaya, tambueni kuwa Serikali inawapenda na inawajali wananchi wake na ndio maana leo nimekuja hapa na Katibu Mkuu Dkt. Allan Kijazi na viongozi wengine ”, amesisitiza Dkt. Ndumbaro
Amewaeleza wananchi hao kuwa katika kufanya maamuzi kuhusu mgogoro uliopo Serikali lazima ifuate Sheria, Taratibu na Kanuni zilizopo kwa kuwa Tanzania inaongozwa kwa Misingi ya kufuata Sheria, hivyo amewataka wananchi hao wawe watulivu kabla ya kufanyika kwa maamuzi.