Mkuu wa Wilaya ya Magu, Salum Kalli, akizungumza na waganga wa tiba asili zaidi ya 300 kutoka katika vijiji 82 wilayani humo baada ya kujadili kero na changamoto zinazowakabili.
Ramadhan Mela Mayandagila, mmoja wa waganga wa tiba asili wilayani Magu alichangoa jambo kwenye mkutao wao uliofanyika mjini Magu ambapo mgeni rasmi alikuwa Mkuu wa Wilaya hiyo, Salum Kalli.
……………………………………………………………………………….
NA BALTAZAR MASHAKA, Magu
MKUU wa Wilaya ya Magu, Salum Kalli, amewataka Waganga Tiba asili wilayani humo, wasiwafilisi na kuwasababishia umasikini wateja wao sababu ya tamaa ya fedha bali wawahudumie kwa kuzingatia maadili ya taaluma hiyo.
Pia amewataka waganga hao kuchangia shughuli za maendeleo wilaya hiyo na taifa ili kuunga mkono juhudi za serikali na kuwaasa wasomeshe watoto ili kupata watalaamu mbalimbali wakiwemo wa tiba mbadala.
Kalli,alitoa rai hiyo hivi karibuni alipokutana na wataalamu wa tiba asili kutoka kwenye vijiji 82 vya tarafa za Ndagalu,Sanjo,Kahangara na Itumbili, mjini Magu.
Alisema waganga wa tiba asili wanaisaidia jamii kwa tiba hizo lakini baadhi wasio waaminifu wanawalaghai na kuwafilisi wateja wao na kuwasababishia umasikini kwa tamaa ya kujipatia fedha.
“Mnafanya kazi nzuri ya kuhudumia jamii yenye changamoto ya maradhi na sikuwahi kuamini mtu anavunjika mfupa wa mkono anaponea kwa mganga wa jadi lakini zingatieni maadili ya tiba mnayoitoa na kuwafichia siri wateja wenu,”alisema Kalli.
Aliongeza kuwa wanapowatibu wakapona wasiwatoze gharama kubwa za kuwafanya wafirisike kiuchumi na kuwafanya kuwa masikini bali wakipona warudi kuzalisha mali na kukua kiuchumi.
“Mkitoa huduma nzuri ya tiba kwa kuzingatia maadili ya utaalamu mlionao mtaongeza wateja nao watawapenda hasa wenye gharama nafuu, hivyo msiwasababishe kuwa masikini,” alisema Mkuu huyo wa wilaya.
Aliwapongeza wataalamu hao wa tiba asili kwa namna walivyozuia na kukomesha mauaji yaliyopamba moto Kanda ya Ziwa ya watu wenye ualibino na ya wazee yaliyosababishwa na imani za kishirikina na kuwafanya waishi kwa amani na kusistiza maadili ili wilaya ya Magu iwe ya mfano kwa tiba asili.
Mratibu wa Tiba Asili Wilaya ya Magu, Casteur Kahema Mawe,alisema mtandao wa waganga wa tiba asili wilayani humo ulitengenezwa tangu 2007 ukilenga kudhibiti na kukomesha mauaji ya watu wenye ualibinism.
Pia alisema wameanzisha na kutoa tiba ya mifupa kwa dawa asili nje ya hospitali ya wilaya na wameanza kupata mafunzo ya tiba ya mifupa kwa dawa asili kwa kushirikiana na madaktari wataalamu kutoka Canada ambapo wanatarajia kupata wahadhiri 6 kutoka nchini humo wenye ujuzi zaidi.
Aidha waganga hao walitumia fursa hiyo kuiomba serikali chumba cha kutolea huduma za tiba asili ndani ya eneo la hospitali ya wilaya kwa sababu wanao uwezo wa kutibu kwa dawa asili na kusaidia jamii.
Mkuu wa Wilaya alisema kinachosubiriwa ni waraka baada ya sheria ili waganga wa tiba asili waruhusiwe kutoa huduma ya tiba hizo ndani ya hospitali tofauti na ilivyo sasa.