*****************************
Na,Said Hauni, Lindi.
April 03:Wakala wa Misitu Tanzania (TFS) na Shirika la kuhifadhi Mipingo na Maendeleo (MCDI) chini ya uwezeshaji Program kuongeza mnyororo wa thamani mazao ya Misitu (FORVAC) umeandaa mpango maalum wa usimamizi na uvunaji mazao ya Misitu kwa vijiji (14) vya wilaya za Nachingwea na Ruangwa,Mkoani Lindi.
Vijiji hivyo ni,Ngunichile,Namatura-Mbondo,Kilimanjaro,Kiegei ‘A’ na ‘B’ katika Wilaya ya Nachingwea, Nandenje, Lichwachwa, Nahanga, Mchichira, Ng’au,Mnawa na Malolo,Wilaya ya Ruangwa.
Hayo yameelezwa na mwenyekiti wa kijiji cha Ngunichile,wilaya ya Nachingwea,Seif Ngwangwa,alipokuwa anazungumza na waandishi wa vyombo mbalimbali vya Habari vilivyotembelea kijijini hapo, kuona shughuli za kimaendeleo zinazofanywa na wananchi.
Ngwangwa amesema mpango huo ni mzuri kwani utasaidia kwa kiasi kikbwa jamii kufahamu thamani ya utunaji Misitu,baada ya kufanikiwa kuvuna,kuuza na kujipatia fedha zinazowezesha shughuli za maendeleo za vijiji vilivyo kwenye mpango huo.
Alisema kabla ya huo mpango,kijiji cha Ngunichile kilikuwa kikikusanya malipo ya ushuru yanayotokana na zao la ufuta pekee, ambayo hayakuwa yanakidhi haja,lakini kutokana na mpango huo utaweza kusaidia kuongeza mapato kupitia mazao mengine ikiwemo Misitu.
“Zamani kijiji chetu ninachokiongoza kilikuwa kinategemea mapato ya ushuru kupitia zao la ufuta,lakini baada ya huu mpango utasaidia kuongeza mapato yetu”Alisema Ngwangwa.
Kauli ya kiongozi huyo wa Kijiji hicho,imeungwa mkono na Habiba Salum, Yusufu Issa na Hemedi Kindamba,waliposema ni mpango mzuri,kwani utakuwa ni mkombozi kwa wananchi wa vijiji husika, ambavyo havina mapato m’badala yanayotokana na rasilimali Misitu.