********************************
Na Woinde Shizza , ARUSHA
CHAMA cha Waandishi wa Habari Mkoa wa Arusha (APC), kimempongeza,kwa dhati kabisa,Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania,Samia Suluhu Hassan kwa hatua yake ya kuagiza kufunguliwa mara moja kwa vyombo vya habari vilivyokuwa vimefungiwa na vingine kufutiwa usajili kwa nyakati tofauti.
Akiongea na waandishi wa habari mwenyekiti wa chama cha waandishi wa habari mkoa wa Arusha (APC)Claud Gwandu alisema kuwa uamuzi wa Rais umeleta furaha, faraja na matumaini
yaliyokuwa yanafifia kila kukicha kwa wanahabari,vyombo vyao na wadau wa
tasnia ya habari nchini, kutokana na matumizi ya sheria kandamizi zilizonyima fursa ya kutumia kikamilifu haki yetu ya kikatiba ya
kuhabarisha,kuelimisha na kuburudisha jamii bila vikwazo, kama ilivyoainishwa katika Ibara ya 18 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania ya mwaka 1977
“Hakika,uamuzi huu wa Rais unadhihirisha adhma yake ya kuhakikisha vyombo vya habari na wanahabari wanatekeleza majukumu yao
katika mazingira rafiki ambayo yanamwezesha kila mmoja wetu kutimiza wajibu wake bila hofu wala vikwazo vyovyote ” alibainisha Gwandu
Alisema zaidi ya hilo, Uamuzi wa Rais, utasaidia kurejesha ajira kwa mamia ya vijana walioathiriwa na maamuzi ya kufungiwavyombo vyao,kwa kuwa watakuwa huru kutafuta, kuchakata na kusambaza taarifa mbalimbali kwa jamii.
Alisema uamuzi huu pia utaisaidia serikali kupata kodi kutokana na mchango
wa vyombo vya habari na wanahabari mmoja mmoja, ikizingatiwa kuwa hiyo
ndiyo kazi inayowaletea mapato halali yanayostahili kulipiwa kodi.
“APC inaamini kuwa maamuzi haya ya Mheshimiwa Rais yametolewa wakati
sahihi, na kwamba yataendana na marekebisho ya sheria kandamizi ambazo
zimetumika kuviumiza vyombo vya habari, wanahabari na wadau wengine
bila sababu yoyote ya msingi”alisema
Alisema siku zote,vyombo vya habari na wanahabari wanapokuwa huru, mnufaika
mkubwa huwa ni Serikali na jamii ambayo sote tunapaswa kuitumikia kwa
mustakabali wa maendeleo ya taifa letu.
Alibainisha kuwa jamii yenye ufahamu wa kutosha juu ya wajibu wake katika utawala bora, demokrasia na haki za binadamu, ni jamii inayowajibika na inayoshiriki
kikamilifu, na kwa hiari katika masuala mbalimbali ya ujenzi wa taifa.
Alisema kuwa wakati tunampongeza Rais kwa maamuzi yake, alitoa wito
kwa vyombo vya habari na wanahabari kuzingatia misingi ya uandishi wa
habari ambayo imejikita katika uzalendo kwa nchi yetu,kufuata sheria,
kanuni na taratibu mbalimbali zilizopo ili kuitumikia jamii yetu kwa weledi
zaidi
Alibainisha kuwa APC inaahidi kuendeleza ushirikiano mzuri uliopo baina yao na wadau
ikiwamo Serikali, na kwamba daima watatimiza majukumu yao kwa kufuata sheria ,kanuni zilizoekwa.