Mkuu wa Wilaya ya Nyasa Isabela Chilumba akimtwisha maji Mary Ndembeka mkazi wa kijiji cha Chimate baada ya kuweka jiwe la msingi kwenye mradi wa maji unaosimamiwiwa na RUWASA NA unaogharimu milioni 390
…………………………………………………………………………….
SERIKALI imewatua ndoo kichwani wananchi wa kijiji cha Chimate wilaya ya Nyasa mkoani Ruvuma baada ya kutekeleza mradi wa maji uliogharimu shilingi milioni 390.
Akisoma taarifa ya mradi huo,Meneja RUWASA Wilaya ya Nyasa Mhandisi Jeremia Maduhu amesema mradi huo ambao umekamilika kwa zaidi ya asilimia 85 unatekelezwa kupitia force account.
Amesema mradi huo utakapokamilika unatarajia kuhudumia wananchi wa kijiji cha Chimate wapatao 2798 na kwamba maandalizi ya mradi huo yalianza Juni 2020 ambapo kazi rasmi ya ujenzi wa mradi ilianza Julai Mosi,2020.
“Kazi zilizopangwa kutekeleza kwenye mradi huu ni ujenzi wa chanzo kipya cha maji,ujenzi wa tanki la kuhifadhia maji lenye ujazo wa meta 75,000,ujenzi wa vituo vya kuchotea maji 15,ujenzi wa mtandao wa bomba wenye urefu wa kilometa 15’’,alisema Maduhu.
Hata hivyo amesema mradi huo hadi sasa zimetumika zaidi ya shilingi milioni 356 kutekeleza mradi huu ambao unatarajia kukamilika kwa asilimia 100 Aprili mwaka huu.
Amezitaja kazi zilizokamilika kwa asilimia 100 kuwa ni ujenzi wa chanzo kipya cha maji,tanki la kuhifadhia maji na ujenzi wa vituo 18 vya kuchotea maji.
Akizungumza baada ya kuweka jiwe la msingi kwenye mradi huo,Mkuu wa wilaya ya Nyasa Isabela Chilumba amesema ni jambo la kufuraisha kwamba ameweka jiwe la msingi kwenye mradi huo wakati vituo 10 kati 18 vinatoa maji ambapo amewataka wananchi hao kutunza mradi huo.
Chilumba amewapongeza RUWASA kwa kusimamia kikamilifu mradi huo kuanzia ujenzi hadi kukamilika hali ambayo sasa itawawezesha wananchi wa Chimate kupata maji safi na salama.
Kwa upande wake Meneja wa RUWASA Mkoa wa Ruvuma Mhandisi Rebman Ganshonga ametoa rai kwa wananchi wa kijiji cha Chimate kuhakikisha kuwa wanasimamia,kutunza na kukilinda chanzo cha maji ili mradi huo uwe endelevu.
“Wananchi wa Chimate,hiki chanzo tunachotumia kwenye mradi huu ni chanzo cha mtiririko,kwa hiyo tafadhali sana msifanye kazi za kibinadamu juu ya chanzo hiki,mkiharibu hiki chanzo mtambue kuwa tutakuwa tumepoteza fedha za serikali bure,maji yatakauka’’,alisisitiza Ganshonga.
Akizungumza kwa niaba ya wanawake wenzake,Mary Ndembeka mkazi wa Chimate amesema,kabla ya mradi huu,baadhi ya akinamama ndoa zao zilikuwa njia panda,huku wengine wakipigwa mara kwa mara na waume zao kwa kuchelewa kutoka kuchota maji mbali ambapo sasa amefurahi neema imewafikia kwa kupata maji bombani.