Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi, anayeshughulikia Sekta ya Uvuvi, Dkt. Rashid Tamatamah akiwasilisha Taarifa za Utekelezaji wa Mpango na Bajeti kwa mwaka wa fedha 2020/21 na Makadirio ya Bajeti ijayo ya mwaka 2021/22 ya Sekta ya Uvuvi mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji iliyokutana leo Machi 29,2021 bungeni Dodoma.
Baadhi ya Viongozi katika Sekta ya Uvuvi wakifatilia uwasilishwaji wa Taarifa za Utekelezaji wa Mpango na Bajeti kwa Mwaka wa fedha 2020/2021 na Makadirio ya Bajeti ijayo ya 2021/22 ya Sekta ya Uvuvi mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji iliyokutana leo Machi 29,2021 bungeni Dodoma.
………………………………………………………………………….
Na.Alex Sonna,Dodoma
Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia sekta ya uvuvi Dk. Rashid Tamatama,amesema kuwa katika bajeti ya sekta ya uvuvi ya mwaka 2021/22 imepanga kuboresha shughuli za uvuvi wa bahari kuu nchini ili iweze kuongeza mapato yataokanayo na mazao ya uvuvi.
Hayo aliyasema jijini Dodoma wakati akiwasilisha bajeti ya wizara hiyo mbele ya kamati ya bunge ya mifugo, maji na kilimo.
Aidha, katika bajeti hiyo kiasi cha Sh. Bilioni 50 kimetengwa kwa ajili ya ujenzi wa bandari hiyo ya uvuvi.
Dk.Tamatama amesema kuwa katika bajeti hiyo maeneo ya vipaumbele ni pamoja na ujenzi wa bandari ya uvuvi itakayo jengwa ili kuongeza ufanisi katika sekta hiyo nchini.
Amesema kuwa hivi sasa mchakato wa kujenga bandari hiyo ya uvuvi upo katika hatua za kuandaaji wa michoro na mara baada ya kukamilika hatua nyingine itafuata.
“Ili kuboresha shughuli hizi za uvuvi kuwa na tija na kuongeza pato la taifa kupitia sekta hii lazima tujenge bandari ya uvuvi itakayo saidia kuongeza uvunaji wa samaki tofauti na ilivyosasa na katika bajeti yetu hii tumetenga Sh. bilioni 50, kwa ajili ya ujenzi huo”amesema Dk. Tamatama
“Lakini pia tunapanga kununua meli za uvuvi ambazo zitakuwa chini ya shilirika hilo la uvuvi na tunatarajia hadi Desemba mwaka huu au Januari mwakani tutakuwa tumenunua meli ya uvuvi ya kisasa yenye vifaa vyote”amesisitiza
Aidha Dk.Tamatama amesema kuwa kupitia ufadhiri wa nchi ya Japani tayari meli hiyo imeshaanza kujengwa katika nchi ya Sirilanka na hadi Januari mwakani wanatarajia kuwa iwe imefika nchini na kuanza kazi.
Amesema kuwa Hayati Rais wa awamu ya Tano John Magufuli, alikuwa amepanga serikali kununua meli za uvuvi nane kwa ajili ya Zanzibar na Tanzania bara.
Dk.Tamatama amesema kuwa wizara itasimamia kuhakiisha zinanunuliwa meli hizo nane mpya na zenye vifaa vyote kwa ajili ya uvuvi wa bahari kuu ili kuongeza uzalishaji wa mazao ya uvuvi na kusafirisha nje ya nchi.
Kwa upande wake Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki amesema kuwa wameanzisha kamapeni ya kuhamasisha jamii kuhusu ufugaji wa samaki na wanatarajia kuweka mashamba darasa katika kila wilaya nchini.
“Lakini pia tunatarajia kufanya upembuzi yakinifu katika maeneo ya bahari na maziwa ili kubainia maeneo ambayo tunaweza kuwapatia wananchi wanaohitaji kufuga samaki katika vizimba kando ya maeneo hayo”amesema Ndaki