Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya Mfuko Misitu Tanzania (TaFF) Profesa Romanus Ishengoma akizungumza
*****************************************
Na Richard Mrusha kutoka Bukombe Geita
MWENYEKITI wa Bodi ya Wadhamini ya Mfuko Misitu Tanzania (TaFF) Profesa Romanus Ishengoma na timu yake imefanya kazi ya kukagua mradi wa ujenzi wa kiwanda cha kuchakata na kufungasha mazao ya nyuki uliopatiwa ruzuku na Mfuko wa Misitu Tanzania unaotekelezwa na Halmashauri ya Wilaya ya Bukombe mkoani Geita.
Mfuko wa Misitu Tanzania unagharamia asilimia 95 na Halmashauri ya Wilaya ya Bukombe inachangia kwa asilimia 5 za ujenzi wa kiwanda hicho kitakachoendeshwa na Halmashauri ya Bukombe kwa mfumo wa Kampuni Tanzu (SPC).
Akizungumza wakati wa wa ukaguzi huo, Mwenyekiti wa Bodi hiyo Profesa Ishengoma amesifu ujenzi unaoendelea na kuitaka Halmashauri kushirikiana kwa karibu zaidi na TaFF.
Profesa Ishengoma amesema wanataka uwazi ushirikishwaji na uwajibikaji kwani ndio msingi wa utawala bora katika kila hatua kwa yale yote yanayofanyika.
“Kwa kawaida tunapokuwa tumedhamini milioni 500 katika ujenzi wa kiwanda kwa shughuli za nyuki moja ya changamoto ni upatikanaji wa malighafi hivyo utajiuliza je asali ipo tunaweza kuweka hapa kiwanda cha milioni 500, fedha ya serikali tumeitumia.
Nakuongeza kuwa “tumejiandaje kupata asali, nakumbuka kuwa tumewezesha vikundi vya ufugaji nyuki lengo ni kufanya kiwanda hiki kama chachu, tunategemea sasa wilaya hii iibue vikundi vingi zaidi.”amesema Profesa Ishengoma
Naye katibu Tawala wa Mfuko wa Misitu Tanzania (TaFF) Dkt Tuli Msuya amesema ni vema mchakato wa kuanzisha kampuni tanzu uanze kama ilivyosainiwa kwenye mkataba wa ujenzi wa kiwanda hicho.
Amefafanua kuwa kuhusu kampuni Tanzu siyo hiari kwa sababu walisaini mkataba na kukubaliana kwamba tutaanzisha kampuni tanzu ya kusimamia kiwanda, ni vema tukaanza mchakato tutakapokamilisha ujenzi wa kiwanda kampuni inakuwa tayari ipo na inaanza kufanya kazi.
Kwa upande wa kamishna Mhifadhi Mkuu wa Misitu (TFS), Profesa Dos Santos Silayo amesema wilaya hiyo inasifika kwa kuzalisha asali nzuri na taarifa zinaonyesha kuwa asali nyingi inayozalishwa eneo hilo inapelekwa nje na wafanyabiashara, si jambo baya kwa sababu ni mmonyororo mzima wa biashara.
“Tujipange kupambana kibiashara tunatakiwa kuangalia mazingira ya kibiashara ya kuifanya asali isiende nje ikiwa ghafi bila ya kupita katika kiwanda hiki, hatuwezi kusema asali ya Tanzania isiuzwe nje, lakini tunapambana nayo kibiashara.”amesema
Profesa Silayo ameongeza kuwa anaamini tutaanzisha kampuni tanzu itakayosimamia ufanyaji wa biashara wenye uwezo wa kubadilika na kushindana na wengine, kwa sababu huwezi kumlazimisha mtu kuuza bidhaa yake kwako kwa kuweka sheria za serikali.
“Tutakaponunua vifaa kwa ajili ya kiwanda tuangalie vile ambavyo vitakuwa na uwezo wa kuchakata mazao mbalimbali ya asali, tunatakiwa kuwa makini na kutazama mbali,”amesisitiza Profesa Silayo.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Bukombe, Said Nkumba amesema kutokana na maeneo yetu haya kuzungukwa na hifadhi tumekuwa na mazingira bora na salama ya kufuga nyuki wanaozalisha asali bora kwa sababu ya kutokuwa na mwingiliano na shughuli za kibinadamu.
“Ujio wa kiwanda hiki umekuja sehemu sahihi kwa sababu kitakuwa kiwanda endelevu kwa kuwa wakazi hapa ni wafugaji nyuki hivyo kurahisisha upatikanaji wa malighafi.