Home Mchanganyiko WAZIRI NDUGULILE ATOA MAAGIZO KWA WATAALAM WA TEHAMA

WAZIRI NDUGULILE ATOA MAAGIZO KWA WATAALAM WA TEHAMA

0
Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dkt. Faustine Ndugulile akizungumza na waandishi wa habari leo Machi 30,2021  katika ukumbi wa Bunge Jijini Dodoma. Kushoto ni Mulembwa Munaku, Mkurugenzi wa TEHAMA wa Wizara hiyo na kulia ni Prosper Minja, Afisa Habari wa Bunge
………………………………………………………………………………………………………
Na.Alex Sonna,Dodoma
Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Dkt. Faustine Ndugulile ametoa maagizo kwa Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dkt. Zainab Chaula kuitisha  kikao cha wataalam wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano(TEHAMA), ili kuzishughulikia hoja za ukaguzi zilizobainishwa na Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali(CAG).
Akizungumza  na waandishi wa habari leo Machi 30,2021 bungeni , Dk.Ndugulile alimtaka Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dk.Zainabu Chaula kuratibu kikao cha Makatibu Wakuu wa Wizara zinazohusika na mifumo ya TEHAMA pamoja na kuitisha kikao cha Wakurugenzi wanaosimamia TEHAMA wa Wizara na taasisi za serikali ili kujadili matatizo yaliyojitokeza na kushauri namna ya kuzitatua
“Nimemuelekeza Katibu Mkuu wangu kuchukua hatua za haraka kwa kuitisha kikao cha wadau wataalamu ili kufanya tathmini ya mifumo hiyo, idadi yake, changamoto za utengenezaji, uendeshaji na uendelezaji wa mifumo hiyo hapa nchini pamoja na  changamoto ya mifumo hiyo kutosomana na kutobadilishana taarifa”, alieleza Dkt. Ndugulile
Aidha, alisisitiza kikao hicho kuwahusisha wataalamu kutoka Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi na Utawala Bora, Ofisi ya Rais TAMISEMI, Wizara ya Fedha, Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) ,Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL), Kituo cha Kuhifadhia Data cha Taifa (NIDC), Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA) 
“Natoa wiki moja kwa wataalamu hawa kufanyia kazi jambo kubwa lililogusiwa na Mhe. Rais Samia la uwezekano wa mifumo hiyo kuruhusu mianya ya upotevu wa mapato na usalama wa mifumo hii na kutoa mapendekezo ya maboresho ya nini kifanyike ili kuhakikisha mianya hiyo inazibwa, usalama wa mitandao unakuwepo na kunakuwa na mifumo inayosomana ambayo haitaruhusu kupoteza mapato ya nchi”, alizungumza Dkt. Ndugulile
Aidha Dk.Ndugulile ameongeza kuwa Wizara yake itafanyia kazi mapendekezo hayo ikiwa ni pamoja na kuchukua hatua za kuboresha na yale ambayo yatahitaji yatahitajika kushughulikiwa na  mamlaka ya juu yatachukuliwa na kupelekwa haya kwa hatua nyingine zaidi.
“Jukumu kubwa la wizara hii ni kutoa miongozo, usimamizi wa mifumo , uendelezaji na kuhakikisha nchi inakuwa na matumizi sahihi ya mifumo ya TEHAMA na salama wake, mifumo mingi iliyokuwa inatumiwa na Serikali ilikuwa inatoka nje ya nchi na fedha nyingi zilitumika kwa uendeshaji na kulipia leseni  lakini kwa sasa zaidi ya asilimia 80 ya mifumo inayotumika nchini na ndani ya serikali imetengenezwa na wataalamu wetu  wazalendo”, alisisitiza Dkt. Ndugulile
Amesema kuwa jukumu kubwa alilonalo katika wizara hiyo ni kuhakikisha inajenga uwezo wa wataalamu wa ndani ya nchi kuhakikisha mifumo mingi inaweza kutengenezwa hapa hapa nchini katika ubora unaouhitaji kwa mahitaji ya nchi na usalama dhidi ya udukuzi ambao unaweza kufanyika kwa kutumia mifumo ya iliyotengenezwa mahali pengine.
Dk.Ndugulile akizungumzia kuhusu siku 100 baada ya kuundwa kwa Wizara hiyo, Waziri Ndugulile alisema kumekuwa na ongezeko la miamala ya fedha inayoipita mtandaoni kwa mwezi kutoka wastani wa Sh. Milioni 310 kwa Disemba 2020 mpaka Sh.Milioni 340 hadi Machi 5 mwaka huu.