……………………………………………………………………………..
NA NAMNYAK KIVUYO, ARUSHA
Wadau wa sekta ya Asasi za kiraia kanda ya Kaskazini wametaja baadhi ya maeneo muhimu ambayo wanatarajia kuendelea kuboresha na kufanya kazi karibu zaidi na serikali ili kuhakikisha wanachangia katika mafanikio ya Mhe. Rais wa jamhuri ya muungano wa Tanzania Samia Suluhu.
Wakiongea na waandishi wa Habari baadhi ya wawakilishi wa asasi 206 wakati wakitoa salamu za pole kutokana na kifo cha aliyekuwa Rais wa jamuhuri ya muungano wa Tanzania,Dkt.Magufuli kilichotokea mnamo machi 17 na pongezi kwa kwa Rais aliyeko madarakani hivi sasa walisema kuwa wamepata tumaini na nguvu kubwa ya kuimarisha utoaji wa huduma mbalimbali kwa jamii.
Mmoja wa wawakilishi hao kutoka shirika la kifugaji jamii ya kimasai Amani Laizer alisema kuwa moja ya maeneo hayo ni kuendelea kuchangia katika kukuza uchumi wa nchi kwa fedha zinazotumika katika miradi mbalimbali, kuboresha utendaji kazi wa Asasi za kiraia ili kuongeza tija katika utoaji wa huduma, kuongeza miradi ya kibunifu yenye tija kwa jamii na makundi mbalimbali pamoja na kuongeza uwezo wa kifikra na kiuchumi miongoni mwa wanajamii kupitia elimu na miradi.
Alisema eneo jingine ni kuchangia ongezeko la utawala bora katika taasisi za kiserikali kutokana na ufuatiliaji unaoemdelea kufanywa na Asasi hizo, kuchangia kutokomeza umasikini nchini, kushirikiana na serikali kutoa huduma,kuweka mikakati na serikali ya kutoa ajira Kwa maelfu ya vijana kulinda katiba,haki za binadamu na utawala bora pamoja na kutoa msaada wa kisheria.
“Nyingine ni kuendelea kuwa walipa kodi wazuri, kufanya kazi zetu Kwa uwazi na Kwa weledi,kuishauri serikali katika mambo ya msingi, kumshauri Mhe. Rais,kushauri maboresho ya sheria,kushauri vyama vya siasa, kushauri serikali na wadau juu ya usawa wa kijinsia na kuboresha amami ya Taifa letu,” Alieleza Laizer.
Aidha kuhusiana na utoaji pole Mratibu wa Asasi za kiraia kanda ya kaskazini ambaye ni mwakilishi kutoka Asasi ya Hakadini Erick Luwongo alisema kuwa wao kama asasi za kiraia watamkumbuka ,Dkt. Magufuli kwa jitihada zake alizofanya katika kuleta maendeleo ikiwemo kupiga vita rushwa na ufisadi,kuboresha miundombinu,huduma za kijamii pamoja na kuweka nidhamu ya utumishi wa umma.
“Tunatambua kuwa tangu mwaka1995 alipochaguliwa kuwa mbunge na baadaye kuwa naibu waziri pamoja na waziri wa katika wizara tofauti tofauti hadi kufikia nafasi ya Rais,Hayati,Dkt.Magufuli alikuwa mstari wa mbele katika kupinga rushwa na kuleta uwajibikaji katika idara za umma pamoja na kupiga vita dhidi ya umaskini na uboreshaji wa miundo mbinu,”alisema Luwongo
Mwakilishi kutoka asasi ya jumuiko la maliasili(TNRF), Magreth Mollel alisema kabla ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 kulikuwa na kilio kikubwa cha wadau wa asasi za kiraia kuhusu mambo kadhaa ikiwemo kukosekana kwa uadilifu katika sekta ya umma,utawala wa sheria,katiba mpya,haki za kibinadamu,umaskini miongoni mwa jamii pamoja na changamoto katika sekta mbalimbali kama elimu,afya,miundombinu na nishati.
“Hayati Rais Magufuli alijitahidi sana kupunguza kwa kiasi kikubwa changamoto ambazo zilikuwa zinaendelea kufanyiwa kazi hadi umauti unamkuta,lakini kuna mambo muhimu yaliyofanyika au kukamilika katika kipindi cha uongozi wake kama vile kukuza uchumi wa Kitaifa pamoja na mikutano ya kila mwaka ya wakurugenzi wa Azaki ambapo wageni rasmi wamekuwa ni mawaziri pamoja na viongozi wengine wa serikali,” Alisema mollel
Kwa upande wake Mkurugenzi wa asasi ya kirai ya utetezi wa haki za kibinadamu(CILAO) Charles Odero Charles alisema wanampongeza Rais.Suluhu Hassan kwa kupata nafasi ya kuongoza nchi na wanaimani naye kwa utendaji wa kazi katika kipindi chote cha uongozi wake kutokana nafasi mbalimbali za uongozi alizowai kushika katika kipindi cha nyuma.
“Katika nafasi mbalimbali alizoshika Rais.Samia Suluhu Hassan amekua mstari wa mbele kufanya kazi na wadau wa asasi za kiraia katika kuhakikisha mambo mbalimbali muhimu kwa jamii yanatekelezwa miongoni mwa maeneo muhimu aliyosimamia moja kwa moja ni pamoja na uboreshaji wa vituo vya afya na huduma muhimu,huduma ya maji maarufu kampeni ya kumtua mama ndoo,kuboresha hali ya lishe kwa akina mama wajawazito na watoto waliochini ya umri wa miaka mitano,”alisema Odero.
Alisema amekuwa mstari wa mbele pia kwa vijana walio katika umri wa balehe , wazee na kuzindua mradi wa kutokomeza unyanyasaji wa wanawake na watoto masokoni pamoja na kupambania kumuinua mwanamke kiuchumi na kuwa mlezi wa mabaraza yao.
Mkurugenzi mtendaji wa taaasisi ya utetezi jamii za pembezoni kupitia vyombo vya habari (Maipac)Mussa Juma alisema wanamuomba Rais,Samia Suluhu kuwa kupata fursa ya kukutana na mashirika yasiyo ya kiserikali kwa muda atakayeupanga ili kuweza kuwapa mwelekeo wake kwa lengo la kuboresha tasnia ya Utendaji kazi wa NGOs mbalimbali.