Home Mchanganyiko WILAYA YA NYASA YAFANYA MAOMBI YA KUMUOMBEA HAYATI DKT.JOHN MAGUFULI

WILAYA YA NYASA YAFANYA MAOMBI YA KUMUOMBEA HAYATI DKT.JOHN MAGUFULI

0

…………………………………………………………………………………

Wilaya ya Nyasa Mkoani Ruvuma  imefanya maombi maalum, ya Kumuombea aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Hayati  Dkt John Pombe Magufuli, maombi yaliyofanyika katika Viwanja vya Fisheries, Mbamba bay Wilayani Nyasa .

Maombi hayo yamewakutanisha wananchi wa Wilaya ya Nyasa, Waamini wa Dini zote  na Mgeni Rasmi alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Nyasa Mh. Isabela Chilumba.

Akihutubia mamia ya wananchi waliohudhuria katika Maombi Maalum,  ya kumuombea Hayati Dkt Magufuli, Mkuu wa Wilaya ya Nyasa amewataka wananchi wa Wilaya ya Nyasa,  kumuombea kwa sala  Hayati Dkt Magufuli ambaye atazikwa Kesho Wilayani Chato na kumuenzi kwa kuyatekeleza yale yote,  ambayo alikuwa akiyasisitiza yakiwepo kufanya kazi kwa bidii, kwa kuwa hayati magufuli alikuwa ni mchapakazi, na Msimamizi makini wa Shughuli zote, kuanzia Ngazi ya chini ya Kitongoji ,Kijiji hadi Taifa. Hivyo kila mtu amuenzi Hayati Dkt Magufuli  kwa kufanya kazi kazi kwa juhudi na maarifa, na kila mtu kwa nafasi yake ahakikishe anatimiza majukumu yake ipasavyo.

Mh Mkuu wa  Wilaya ameeleza kuwa  wananchi wa Wilaya ya Nyasa wamepokea Taarifa ya kifo cha Hayati Dkt Magufuli kwa Majonzi Makubwa,  kwa kuwa Rais  Magufuli  aliwaahidi wananchi kuja Nyasa,  Kufungua Barabara ya Mbinga Mbamba bay,  iliyojengwa kwa kiwango cha Lami, ambayo Imekamilika na aliahidi kuja kufungua barabara hiyo mwenyewe, alipoweka jiwe la msingi la Barabara  Wilayani Mbinga, na kwa msisitizo Januari 5 mwaka huu, alimtuma Waziri Mkuu Mh. Kassim Majaliwa kuja kukagua Ujenzi ikiwa ni maandalizi ya yeye kuja kufungua barabara hiyo.

Aidha mh. Chilumba amewataka Wananchi wa Wilaya ya Nyasa kuongeza Mshikamano na Kumuombea Hayati Dkt Magufuli kwa Kuwa Kazi ya Mungu haina makosa, naye kampenda zaidi.

“Ndugu zangu kwa niaba ya wananchi wa Wilaya ya Nyasa, Tumepokea Taarifa ya Kifo cha Hayati Dkt Magufuli kwa Majonzi makubwa, kiasi kwamba mara baada ya kupokea Taarifa Hizi sikuweza kulala kwa kwa kuwa ametutendea mambo makubwa Wilayani Nyasa, na Kuiweka Nyasa katika Ramani ya maendeleo na tulikuwa tukimsubiri aje kutufungulia barabara ya Mbinga Mbamba bay,  iliyojengwa kwa kiwango cha Lami na Imekamilika na kutufanya wakazi wa Nyasa tupate maendeleo Makubwa”.

Mh. Chilumba ameitaja Miradi   Mikubwa  ambayo wananchi wa wilaya ya Nyasa wanamkumbuka Hayati Dkt Magufuli kuwa ni Ujenzi wa Meli za mizigo na Abiria za Ziwa Nyasa,Bandari ya Ndumbi, Hospitali ya Wilaya ya Nyasa,Chuo cha Ufundi Stadi VETA NYASA, Vituo vya afya Mkili, Kingerikiti, Kihagara, Utoaji Elimu Bure na Miradi ya mingine ambayo hawezi kuitaja yote, Umeme,maji na ujenzi wa madarasa katika shule za Msingi na Sekondari Wilayani hapa na kusema kuwa Magufuli aliipenda sana Wilaya ya Nyasa.

Kwa upande wao Viongozi wa Dini ya Kiislam na Kikristo Wilaya ya Nyasa  wamesema wanamuombea Kwa Mungu Hayati   Dkt Magufuli  kwa kuwa alikuwa ni zawadi kutoka kwa Mungu kwa Tanzania na Afrika,  na alifanya kazi kwa nguvu zote na kupiga Vita Rushwa, na ubinafsi na kutumia raslimali za Tanzania kwa manufaa ya Watanzania. Pia wanamuombea Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan hasa katika Kipindi hiki kigumu ili aweze kutekeleza vema majukumu yake ya kulijenga Taifa la Tanzania.