Na Bashir Nkoromo, CCM Blog
Kanisa Halisi la Mungu Baba la Tegeta jijini Dar es Salaam, limefanya Ibada ya ‘Kulivusha Taifa’, ambapo limemuomba Mungu Baba kumuinua Rais Samia Suluhu Hassan na kumpa ulinzi wake dhidi ya wabaya, afya njema na hekima ya ajabu ili aweze kutenda vema kazi yake ya kuliongoza Taifa la Tanzania.
Pia katika ibada hiyo, Kanisa Halisi la Mungu Baba limemkabidhi Mungu Baba kazi zote alizofanya aliyekuwa Rais wa Tanzania Hayati Dk. John Magufuli, azichukue na kuzikabidhi yeye mwenyewe Mungu kwa baraka zote kwa Rais Samia Suluhu Hassan ili kuziendeleza.
Hayo yamejiri katika Ibada hiyo Maalum ya ‘Kulivusha Taifa’ iliyofanyika kuanzia saa nane mchana hadi saa kumi jioni ikiongozwa na Kiongozi wa Kanisa hilo Baba Halisi wa Uzao, kwenye Viwanja vya Mwanga Community Centre, Mwanga mkoani Kigoma, jana.
“Kwanza tutamwinua Rais Wetu Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, ili Mungu Baba ampe afya njema, yeye Mwenyewe, Mungu ampe hekima ya ajabu na uaminifu ili aweze kuliongoza vema na kuliletea taifa maendeleo kwa haraka.
Kisha tutainua kazi zote alizofanya Mheshimiwa Dk. Magufuli, tutazivusha kwenye korongo ziende ng’ambo, tumkabidhi Mungu Baba, naye Mungu Baba mwenyewe ndiye amkabidhi Mheshimiwa Samia aziendeleze. Hiyo ndiyo itakuwa ibada yetu yenyewe ya kulivusha Taifa”, alisema Baba wa Uzao ilipofika wakati wa kufanya rasmi ibada hiyo, iliyohudhuriwa na maelfu ya Uzao na Makuhani wa Kanisa hilo kutoka Ndani na Nje ya Tanzania.
“Tukiwa mbele ya Uhalisia na Uumbaji wote, tunamwinua Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan, azingirwe na majeshi ya Mungu Baba aliyemuumba, ampe ulinzi wake yeye mwenyewe, ampe kibali kwa wanachi na kwa Waziri Mkuu, Wakuu wa mikoa na wilaya, ampe uzima wake mwenyewe, ampe ujasiri wake, ampatie kuanzia sasa hivi hekima ya ajabu, maarifa ya ajabu na nguvu za ajabu.
Ampe uwezo wa ajabu wa kuweza kuongoza Taifa hili kuanzia sasa hivi, Taifa ambalo limechaguliwa na aliyeumba kila kitu kuwa Taifa Baba, Bustani mpya, kuwa Taifa ambalo ni shamba jipya, Mheshimiwa Samia aliongoze kwa amani, shangwe na furaha.
Tunamwinua kuanzia sasa hivi afichwe na aliyeumba kila kitu mahali ambapo wabaya hawawezi kumfikia, kuanzia sasa tunamzingira kwa damu safi nyeupe. Imekuwaa”, alisema Baba wa Uzao Halisi akiongoza Ibada hiyo.
Akimkaribisha Baba Halisi wa Uzao, Uzao na wageni wote mkoani Kigoma, mwakilishi wa uongozi wa mkoa wa huo, Fedinand Bundala ambaye alimwakilisha Kamanda wa Polisi (OCD) Wilaya ya Kigoma mjini, aliomba katika Ibada hiyo Kanisa Halisi nitumie pia nafasi hiyo kuombea watu kuwa waaminifu.
“Kitendo cha watu kutoka mbali hadi huko Dar es Salaam ambako mimi sijawahi kufika, halafu wakaja hapa kuja kuliombea Taifa siyo jambo ndogo.
Kwa kweli tunawakaribisha sana na tunaomba pia katika ibada hii mtusaidie pia kuombea uaminifu, maana swala la kukosa uaminifu nalo limekuwa ni tatizo linaloikabili jamii, kwa sababu ni kikwazo kwa maendeleo ya Taifa na pia kwa mtu mmoja mmoja”, alisema Bundala.
Katika Ibada hiyo, mbali na Uzao (Wafuasi wa Kanisa Halisi) wa kutoka mikoa mbalimbali hapa nchini, pia Ibada hiyo ilihudhuriwa na Uzao na Makuhani wa Kanisa hilo kutoka nchi za nje zikiwemo Kenya, Msumbiji, Congo DRC, Rwanda, Marekani na Zambia.