………………………………………………………………………….
Na.Alex Sonna,Chato
Mkuu wa Majeshi nchini Tanzania (CDF) Venance Mabeyo amesema kuwa ulinzi wa nchi na mipaka yake ni salama na vyombo vitaendelea kukulinda kama Rais, kukutii kama amiri jeshi mkuu na kutekeleza majukumu yetu kama ilivyoainishwa kwenye Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Hayo ameyasema leo Machi 26,2021 wilayani Chato Mkoani Geita kwa niaba ya Wakuuu wa vyombo vya ulinzi na usalama wakati wa Ibada ya Mazishi ya Hayati Dkt.John Magufuli,Mabeyo amesema kuwa hali ya nchi ni shwari na wataendelea kuimarisha ulinzi.
CDF Mabeyo amesema kuwa vyombo hivyo vitaendelea kuonyesha uadilifu, utiifu na uaminifu kwake kama ilivyokuwa kwa awamu za uongozi zilizopita.
“Vyombo vya ulinzi na usalama vinapenda kukuhakikishia kuwa ulinzi wa nchi na mipaka yake ni salama na vitaendelea kukulinda wewe, kukutii na kutekeleza majukumu yake aidha vinakuhakikishia utiifu, uadilifu na uaminifu mkubwa kwako” amesema CDF Mabeyo
Aidha Mabeyo amemuomba Rais Samia kuwatunuku nishani askari wanafunzi waliotakiwa kutunikiwa nishani hizo Machi 10, 2021 na Hayati Rais Magufuli
”Hayati Magufuli alitakiwa awatunuku nishani Februari 20 lakini kutokana na kazi zake tukasogeza mbele hadi Machi 6,alipomaliza ziara yake Dar es Salaam akaniambia hajisikii vizuri hivyo akaomba tusogeze hadi Machi 10 ili ajitazamie afya yake,” amesema Mabeyo
Mwili wa Hayati Dkt.John Magufuli unatarajiwa kupumzishwa leo katika nyumba ya milele alipozikwa Baba yake Mzazi.