Wakulima wa Misiti ya Misaji (Teak) kutoka kijiji cha Mkali A wakishiriki kupanda miti hiyo kibiashara katika shamba la moja wapo.
Ofisa Misitu na Mratibu wa FORVAC Wilaya ya Nyasa, Bugingo Bugingo akitoa maelezo kuhusu faida za Miti ya Misaji (Teak), ambayo inapandwa katika vijiji vya Liuli, Lipingo, Mkali A na Mkali B wilayani hapo.
Mratibu wa FORVAC Kongani ya Ruvuma, Marcel Mutunda akieleza waandishi wa habari ni sababu gani imewasukuma kubuni program hiyo.
Wakulima wa Miti ya Misaji (Teak), kutoka Kijiji cha Mkali A wakiwa katika picha ya pamoja na wafadhili wa miti hiyo baada ya kupanda miti.
Muonekano wa Miti ya Misaji (Teak) ambayo imepandwa katika mashamba mbalimbali ya wakulima wa vijiji.
…………………………………………………………………………………
NA SULEIMAN MSUYA, NYASA
SHUGHULI za upandaji miti kibiashara ambazo zinafadhiliwa na Program ya Mnyororo wa Thamani wa Mazao ya Misitu (FORVAC) katika vijiji vinne vya Liuli, Lipingo, Mkali A na Mkali B inatarajiwa kuzalisha mamilionea 599 wilayani Nyasa mkoani Ruvuma.
FORVAC inatekelezwa na Idara ya Misitu na Nyuki kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS).
Program inatekelezwa katika Kongani tatu za Tanga (Handeni, Kilindi, Mpwapwa na Kiteto); Kongani ya Lindi (Wilaya za Liwale, Ruangwa na Nachingwea) na Kongani ya Ruvuma (katika Wilaya za Tunduru, Namtumbo, Songea, Mbinga na Nyasa) na inafadhiliwa na Serikali mbili za Tanzania na Finland.
Akizungumza na mwandishi wa habari hii Mwenyekiti wa Chama cha Wapandaji Miti Kibiashara (TGA) Kata ya Liuli Samwel Mawanja, amesema program ya FORVAC ambayo inawapa fursa ya kupanda miti imeanza kuleta matumaini makubwa.
Mawanja amesema katika kata ya Liuli vijiji vinne ambavyo vipo kwenye program ya FORVAC zaidi ya wanavijiji 500 wamepanda miti ya Misaji (Teak) ambapo baada ya miaka 20 watavuna na kuanza kuuza.
Mwenyekiti huyo amesema mwitikio wa wananchi wa vijiji hivyo vya Lipingo, Liuli, Mkali A na Mkali B kupanda miti umekuwa mkubwa hasa baada ya kupata elimu hali ambayo inavutia wengine.
“Tumeamua kushiriki katika mradi huu baada ya kupata elimu ya faida ya Misaji. Hadi sasa tupo zaidi ya 500 ambapo kila mmoja ana hekari mbili za kupanda hivyo zaidi ya hekari 1,000 zimepandwa misaji na hekari moja inaweza kumpatia mkulima zaidi ya shilingi milioni 300 baada ya miaka 20,” amesema Mawanja.
Mwenyekiti huyo amesema kwa sasa kuna wakulima 599 ambapo kijiji cha Liuli kina wakulima 296 wa Miti ya Misaji, Lipingo zaidi 150, Mkali A 116 na Mkali B 37 ila wanatarajia wataongezeka kwa kuwa elimu imeendelea kutolewa.
Amesema wanashuruku FORVAC kuwawezesha mbegu ya Misaji na kuahidi kuwa watahakikisha hawawaangushi.
Mwenyekiti wa TGA ya Mkali B, Magreth Ngonyani, amesema ujio wa program hiyo umefungua kurasa mpya ya maisha yao kwani wanaamini miaka michache ijayo watatambulika kama mamilionea.
Ngonyani amesema wanashiriki program hiyo wakiwa na amani kwa kuwa haiwabani kufanya shughuli nyingine za uzalishaji huku wakiwa na matumaini ya kunufaika.
“Sisi hapa tumeelimishwa na wataalam wa FORVAC na Serikali kuhusu faida ya miti ya Misaji hivyo tuna imani kuwa siku chache tutabadilishwa majina kwa kuitwa mamilionea,” amesema.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa TGA ya Mkali A, Alphonce Sangana amesema wanakijiji wamepokea program hiyo kwa moyo wote jambo ambalo linarahisisha utekelezaji na usimamizi wake.
Sangana amesema wamepanda miche zaidi 50,000 kwenye hekari zaidi ya 100 hivyo matumaini yao ni kuwa baada ya miaka 20 watakuwa na mamilionea wengi.
Mwenyekiti huyo ambaye pia Katibu Mwenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), amesema program hiyo imeanza kuonesha matumaini ila changamoto kubwa ni kukosekana miundombinu ya uhakika ya kuwafikisha shambani.
“FORVAC imekuja kutekeleza Ilani ya CCM, inayotaka mazao ya misitu kuongezewa thamani mimi nikiwa muenezi nitaendelea kupigania hili kwa nguvu zote,” amesema.
Menedora Haule Mwekahazina wa TGA ya Mkali A, amesema yeye amefanikiwa kupanda miche 520 ambapo anaamini siku chache zijazo zitabadilisha maisha yake.
Haule amesema amekuwa akitoa elimu kwa wakina mama wenzake ili washiriki program hiyo kwa kuwa itabadilisha maisha yao.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Mkali A, Barnabas Mbele amesema program hiyo ya FORVAC ni mkombozi wa wanakijiji na kuwa watakuwa bega kwa bega kuhakikisha inafanikiwa.
Amesema program hiyo imeweza kuajiri vijana wengi kijiji kwake hivyo hawana budi kuiunga mkono ili iwe endelevu.
“Mimi kama Mwenyekiti wa kijiji ninayetokana na CCM nadiriki kusema program ya FORVAC inatekeleza Ilani ya chama hivyo tutaiunga mkono bila shaka,” amesema.
Kwa upande wake Ofisa Misitu na Mratibu wa FORVAC Wilaya ya Nyasa Bugingo Bugingo, amesema program hiyo itakuwa na matokeo chanya kwa wanavijiji siku chache zijazo.
“Nikizungumza kama mtaalam niseme kuwa baada ya miaka 20 hapa Liuli kutakuwa na mamilionea wengi ambao watatokana na kilimo cha Misaji.
Kwa mujibu wa taarifa za sasa ujazo wa mita moja ya Mti wa Msaji unauzwa hadi shilingi laki 8 hivyo kwa mtu mwenye miti 350 akivuna kwa pamoja anaweza pata zaidi ya shilingi milioni 350 kwa hekari moja,” amesema.
Amesema Misaji ni miti ambayo inatumika kutengeneza vya thamani kama meli, jahazi na vitu vingine.
Bugingo amewashauri wanavijiji kuhamasishana kupanda miti ya Misaji kwa kuwa ni fursa kubwa ya kiuchumi.
Mratibu wa FORVAC Kongani ya Ruvuma, Marcel Mutunda amesema wametoa miche ya Misaji 450,000 ambayo imegharimu zaidi ya shilingi milioni 225 lengo likiwa ni kuinua maisha ya wanavijiji nakuonesha kwa vitendo dhana nzima ya mnyororo wa thamani wa mazao ya misitu.
Mutunda amesema FORVAC inaaamini iwapo kila mwanakijiji atatambua dhana ya mnyororo wa thamani wa mazao ya misitu ni wazi kuwa wataitunza na kuilinda misitu.
“Sisi tunataka Tanzania iwe na mamilionea wengi kupitia rasilimali zao na misitu ni moja wapo hivyo tutatoa ushirikiano na yoyote ambaye ataonesha kuhitaji,” amesema.
Mkuu wa Wilaya ya Nyasa Isabela Chillumba amesema wao kama wilaya wataungana na mdau yeyote ambaye atakuwa amekuwa na wazo la kumkomboa mwananchi kiuchumi, maendeleo na huduma za kijamii.
Aidha, amesema wilaya kupitia Wakala wa Barabara Mjini na Vijijini (TARURA), watajitahidi kutatua changamoto ya miundombinu katika vijiji vyote ili shughuli za maendeleo zitekelezwe.
“Tunawakaribisha wadau wote ambao wana mitazamo kama ya FORVAC ili kuchochea maendeleo wilayani kwetu,” amesema.