Home Mchanganyiko BCI WAMLILIA HAYATI DKT.JOHN POMBE MAGUFULI, TUMEPOTEZA MTETEZI

BCI WAMLILIA HAYATI DKT.JOHN POMBE MAGUFULI, TUMEPOTEZA MTETEZI

0

rais wa BCI Godefroid Mukendi

*****************************************

UMOJA wa wafanyabiashara kutoka nchini Congo ‘Business Congolese International’ (BCI) umesikitishwa na kifo cha aliyekuwa Rais wa awamu ya tano ya Tanzania Hayati Dk John Magufuli na kudai kuwa atakumbukwa na wafanyabiashara na wananchi wote wa Congo kwa uchapakazi wake.

Wakizungumza Jijini Dar es Salaam viongozi wa umoja huo walisema kifo cha Dk Magufuli siyo pengo kwa watanzania bali wananchi wote wa Bara la Afrika na Dunia nzima kutokana na ushupavu wake katika kuiongoza nchi na kuiletea maendeleo mbalimbali.

Hata hivyo rais wa umoja huo Mukendi Godefroid, alisema Taifa limempoteza shujuaa na mchapakazi hodari aliyejitolea kuiongoza Tanzania akisimamia haki za wanyonge na kuweka kando maslahi yake binafsi akisisitiza kuwa kifo chake ni pigo pia kwa wafanyabiashara wa Congo wanaofanya shughuli zao kati ya Congo na Tanzania.

“Tunatoa pole kwa Rais Samia Suluhu Hassan, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, viongozi wote wa mihilimi mitatu ya Serikali na wananchi kwa ujumla kwa kuondokewa kiongozi huyu aliyeondoka wakati taifa likiwa bado linamuhitaji, hakuna zaidi ya kumauombea kwa Mungu ampumzishe kwa amani” alisema Mukendi

Alisema Dk Magufuli ameondoka akiwa ameacha alama kubwa kwa watanzania na hata dunia kutokana na mambo mengi aliyoyafanya katika taifa hili enzi wa uhai wake na zaidi umoja wa wafanyabiashara hao waliopo hapa nchini na Congo wakimkumbuka kwa namna alivyosimamia mambo mbalimbali yanayohusu biashara zao.

“Tunaamini mambo yote mazuri na mengine bado yataendelea kufanyika katika Taifa hili chini ya Rais wa sasa Mama yetu Samia Suluhu Hassan kwa kuwa chini ya uongozi wake alipikwa vyema pamoja na viongozi wengine waliopo chini yake kuliongoza taifa hili” aliongeza Mukendi.

Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti wa umoja huo John Kapeta, mbali na kutoa pole kwa wananchi pamoja na Serikali kupitia mihili yake yote mitatu juu ya kifo cha Dk Magufuli, alimpongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kupewa nafasi hiyo huku akiwataka watanzania kumuamini na kwamba anatosha katika nafasi hiyo.

“Mama Samia amefanya kazi na Dk Magufuli kwa zaidi ya miaka sita akiwa Makamu wa Rais, kila kitu alichokuwa akikifanya Hayati Magufuli alikuwa anaona, tunaamini moto wake utaendelea kuwa ule ule kama ilivyokuwa hapo nyuma na taifa litazidi kusonga mbele” alisema Kapeta

Alisema wao kama wafanyabiashara wa Congo, walikoshwa na ushirikiano na urafiki uliokuwepo baina ya Dk Magufuli na Rais wa Congo Felix Tshisekedi kiasi cha kuitana kaka, jambo ambalo pia limewafanya wananchi wa nchi hizo mbili kwenda na upendo huo.

Aidha wamewatoa hofu wafanyabiashara wan chi hiyo na kuwaambia kuwa kazi inaendelea kama kawaida kutokana na uhimara wa viongozi wa Serikali katika kushughulikia changamoto na kero mbalimbali endapo zitajitokeza kama ambavyo Hayati Dk Magufuli alikuwa akipambana nazo.