Mkurugenzi mtendaji wa Asasi ya kilele inayojishughulisha na kilimo cha Horticulture (TAHA) Dkt Jackline Mkindi akiongea na waandishi wa habari.
Mkurugenzi mtendaji wa Asasi ya kilele inayojishughulisha na kilimo cha Horticulture(TAHA) Dkt Jackline Mkindi akisaini kitabu cha maombolezo ya Hayati Rais Dkt Magufuli.
Antony Chamanga Meneja mkuu wa maendeleo ya Asasi kilele inajishughulisha na Kilimo cha horticulture akisaini kitabu cha maombolezo.
Kelvin Remen Meneja Mazingira ya Biashara wa Taha akisaini kitabu cha maombolezo.
*****************************************
NA NAMNYAK KIVUYO, ARUSHA.
Mkurugenzi mtendaji wa Asasi ya kilele inayojishughulisha na kilimo cha Horticulture yaani mboga, matunda na mimea itokanayo na mizizi pamoja na viungo(TAHA) Dkt Jackline Mkindi ambaye pia ni mwenyekiti wa baraza la kilimo Tanzania amesema asasi hiyo itamkumbuka Hayati Rais Dkt John Magufuli kwa nia yake ya dhati ya kukiinua kilimo Tanzania.
Dkt Mkindi aliyasema hayo baada ya kusaini kitabu cha maombolezo cha Hayati Rais Dkt Magufuli katika ofisi ya mkuu wa mkoa wa Arusha ambapo alisema kuwa walipokea kea masikitiko makubwa taarifa za kifo chake na watamkumbuka kwa utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo iliyokua na lengo ya kuongeza tija kwe kilimo hapa nchini.
“Katika uongozi wake Rais Magufuli alizindua rasmi programu ya kuendeleza sekta ya kilimo(ASDP II) iliyokuwa imeainisha maeneo ya vipaumbele katika kuendeleza sekta ya kilimo hapa nchini ambapo utekelezaji wake umeendelea kwa sehemu kubwa tangu 2018,” Alisema Dkt Mkindi.
Alifafanua kuwa baadhi ya mafanikio yaliyopatikana katika sekta ya kilimo kwa kipindi cha uongozi wake ni pamoja na maboresho ya kisera yaliyopelekea upatikanaji wa pembejeo na zana bora za kilimo kwa gharama nafuu ikiwemo mbegu, mbolea, viuatilifu na teknolojia mbalimbali za uzalishaji.
“Tutamkumbuka pia kwa nia yake ya dhati ya kuendeleza sekta ya Horticulture kupitia mikakati mbalimbali kama alivyoainisha katika hotuba yake ya ufunguzi wa bunge la 12 ikiwemo ununuzi wa ndege ya mizigo ili kurahisisha usafirishaji wa mazao ya mboga mboga na matunda,”Alieleza Dkt Mkindi.
“Aliongeza mkazo katika kuendeleza tasnia ya horticulture kutokana na ukuaji wake wa kasi hapa nchini, hakika tuataendelea kumkumbuka na kuenzi maono yake thabiti, uzalendo, uthububutu, na moyo wa kujituma aliokuwa nao Hayati Rais Dkt Magufuli,”Aliendelea kusema.
Alieleza kuwa aliwatengenezea mazingira wezeshi ili kuruhusu biashara ya kilimo kuendelea kwa kuboresha miundombinu kwa kuwekeza kwa kina katika maeneo mbalimbali na kuweza kuhamasisha uwekezaji katika kilimo kama vile miradi mikubwa ya umeme, barabara katika maeneo yaliyokuwa na uwekezaji wa kilimo, ujenzi wa bandari, ujenzi wa reli na viwanja vya ndege.
“Yote haya katika kilimo tunayaona kama ni fursa ya kutuwezesha kuwekeza zaidi kwenye kilimo pamoja na kufanya biashara na wenzetu ndani na nje ya mipaka yetu na kama viongozi wa sekta binafsi tutayaendeleza kwa kumuenzi kwa vitendo na ufanisi mkubwa huku tukilinda heshima ya Tanzania na kutumia kwa uangalifu na uadilifu mkubwa rasilimali zetu tulizonazo kwani ndiyo iliyokuwa kiu yake kuona kwamba tunafanya maendeleo, tunachapa kazi na kutunza rasilimali zetu,”Alisema.
Aliongeza kuwa wataendelea kufanya kazi kwa ukaribu na serikali na kumsapoti kwa hali na mali Rais wa sita wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu katika kuhakikisha kwamba yale ambayo aliyaacha yanaendelea na kuendelea kuyatekekeleza kwa manufaa ya taifa na watanzania wote.
Aidha kwa niaba ya sekta ya kilimo na kwa niaba ya wanawake waliopo katika sekta hiyo Dkt Jackline Mkindi amempongeza Rais Mheshimiwa Samia Suluhu kwa kuwa Rais na kusema kuwa wako bega kwa bega na watafanya kazi kwa ukaribu ikiwa ni pamoja na kumwamini na kuwa na uhakika nae kutokana na akili na busara ya hali ya juu ambayo Mungu amemjalia.