Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu,akizungumza na viongozi mbalimbali waliohudhuria hafla ya kitaifa ya kumuaga aliyekuwa Rais wa Tanzania Hayati Dkt.John Magufuli iliyofanyika leo Machi 22,2021 jijini Dodoma katika uwanja wa Jamhuri Dodoma
………………………………………………………………………………………
Na.Alex Sonna,Dodoma
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu amewahakikishia Watanzania kuwa hakuna jambo litakaloharibika kufuatia kifo cha aliyekuwa Rais wa Tanzania Hayati Dkt. John Pombe Magufuli amewatoa hofu baadhi ya watu wanaosema kuwa mwanamke anaweza kweli kuongoza nchi au la.
Mhe. Samia Suluhu Hassan ameyasema hayo leo Machi 22,2021 jijini Dodoma wakati akiongoza viongozi mbalimbali na wananchi kuaga mwili wa aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli katika uwanja wa Jamhuri Dodoma.
Mhe.Samia amesema kuwa ni siku nyingine ngumu katika historia ya nchi yetu na kwangu ni siku ngumu zaidi, tarehe 17 ilikuwa ni siku ngumu nilipotakiwa kutangaza kifo cha Rais haikuwa rahisi kwangu nilihisi nafanya makosa kumtangaza Rais wangu amefariki, lakini nikaambiwa hakuna wakulitangaza hili ispokuwa wewe.
“Hayati Dkt. Magufuli alikuwa ni kipenzi cha wengi hii inadhihirishwa na uwepo wa viongozi wakuu wa nchi na serikali na mashirika ya kikanda na kimataifa waliofika kumuaga hasa ukizingatia majukumu mazito waliyonayo lakini nyakati hizi tulizonazo ambapo kusafiri nje ya nchi si jambo jepesi”
“Na hapa nataka niseme kidogo kwa wale ambao wanamashaka kuwa Mwanamke huyu ataweza kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nataka niwaambie kuwa aliyesimama hapa ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye maumbile yake ni mwanamke”,amesema Rais Samia.
“Daima Nitamshukuru Rais Magufuli kwa imani yake kubwa kwangu na kwa wanawake wa Tanzania, Tukiandika historia ya usawa au uwiano wa kijinsia kwenye nyanja za siasa nchini lazima Magufuli jina lake litakuwemo .Na kupitia yeye Tanzania ilipata Mwanamke wa kwanza Makamu wa Rais na sasa ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
“Nafarijika alinipa fursa ya kuonesha uwezo wangu na kuwa wanawake tunaweza tukijengewa mazingira ya kufanya kazi kisawa sawa leo inanipa faraja kuwa kwa takribani miaka sita nilihudumu kama msaidizi wake wa kwanza na wa karibu”
“Hakuna jambo litakaloharibika nchi yetu ipo salama, tutaendeleza alipoishia na tutafika alipopatamani tufike”,amesisitiza
Hafla ya kumuaga Hayati Dkt.John Magufuli kitaifa imefanyika katika uwanja wa Jamhuri Dodoma na kuhudhuriwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Samia Suluhu Hassana pamoja na Marais wa nchi zaidi ya 10 na viongozi mbalimbali kutoka nje ya Tanzania wamehudhuria tukio la kutoa heshima za mwisho.