Mkurugenzi wa Shirika la Mpingo na Maendeleo (MCDI), Gaspar Makala akitoa maelezo kwa Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk.Damas Ndumbaro kuhusu mashine ya kuchakata mazao ya misitu iliyonunuliwa na MCDI kwa ufadhili wa Program ya Mnyororo wa Thamani wa Mazao ya Misitu (FORVAC).
Mtaalam wa Mashine ya Norwood ya kuchakata mbao, Paul Kuiranga alielezea namna mashine hiyo inafanya kazi.
*************************************
NA SULEIMAN MSUYA, SONGEA
MSHAURI Mkuu wa Kiufundi wa Program ya Mnyororo wa Thamani wa Mazao ya Misitu (FORVAC), Juhan Harkonen amesema matumizi ya teknolojia katika uvunaji na uchakataji mazao ya misitu utachochea uendelevu wa misitu na ukuaji wa uchumi nchini.
Aidha amesema watahakikisha changamoto ya soko katika bidhaa za misitu linapatiwa jibu ili dhana ya mnyororo wa thamani ionekane kwa haraka.
Harkonen amesema hayo wakati akizungumza na mwandishi wa habari hii hivi karibuni wilayani Songea mkoani Ruvuma.
Amesema sekta ya misitu ni muhimu kwa maendeleo ya nchi iwapo uvunaji wake utafuata njia sahihi za teknolojia kama matuzimi ya mashine za kuchakata.
Mshauri huyo amesema nchini Finland wanatumia teknolojia katika uvunaji wa rasilimali misitu hali ambayo imechangia kuwa endelevu.
“Sisi tumewekeza kwenye teknolojia ya uvunaji kwa kutumia mashine za kuchakata mazao ya misitu hivyo FORVAC itahakikisha hili linafanyika hapa nchini.
Tumenunua mashine hizo mbili moja itatumika hapa Songea na Namtumbo na nyingine Ruangwa ila hadi mwisho wa mwaka tunatarajia kununua mashine nyingine tatu ambapo moja ikuwa Ruvuma, Lindi na Tanga,” amesema Harkonen.
Amesema kwa ujumla mradi huo ambao unatekelezwa chini ya Idara ya Nyuki na kufadhiliwa na Serikali ya Tanzania na Finland umeonesha mafanikio katika ngazi zote jambo ambalo linawapa nguvu ya kuendelea.
Kuhusu changamoto ya soko amesema eneo hilo linahitaji nguvu ya ziada ili tafsiri sahihi ya mnyororo wa thamani ionekane kwa kila mtu.
Harkonen amesema mbinu moja wapo ya kupata solo ni Tanzania kutangaza bidhaa zinazopatikana kwenye misitu kwa soko la ndani na nnje.
Amesema Serikali ya Finland itaendelea kushirikiana na Tanzania kuhakikisha rasilimali misitu inakuwa na mchango mkubwa kwa maendeleo, mazingira na uchumi.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Misitu na Nyuki Wizara ya Maliasili na Utalii Dk.Ezekiel Mwakalukwa amesema kinachofanywa na FORVAC na Shirika la Mpingo na Maendeleo (MCDI) ni utekelezaji wa Sera ya Misitu ya 1998 na Sheria ya Misitu ya 2002.
Amesema program ya FORVAC itaweza kufikia lengo iwapo kila mdau atashiriki kwa kufuata Sheria na miongozo inaliyoandaliwa na Idara ya Misitu na Nyuki.
“Mashine hii ambayo inatolewa katika wilaya ya Songea na Namtumbo ni moja ya nyenzo muhimu kwenye kuonesha mnyororo wa thamani wa mazao ya misitu hivyo tuitumie vizuri kwa maslahi yetu,” amesema.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Nyasa Isabela Chillumba amesema mashine hiyo ni mkombozi mkubwa kwenye sekta ya misitu mkoani hapo.
Amesema imani yao ni kutumia mazao ya misitu kuinua uchumi wa wananchi, wilaya, mkoa na nchi kwa ujumla.
“FORVAC imekuja kutuletea mabadiliko makubwa kwenye sekta ya misitu ambapo sasa wananchi wanaanza kunufaika na rasilimali za zao hivyo wanazilinda na sisi kama Serikali tupo nyuma yao
Mashine hii ya kuchakata mazao ya misitu itakuwa kichocheo kikubwa zaidi katika kuboresha maisha yao,” amesema.