……………………………………………………………………………………………………..
Na. Zillipa Joseph, Katavi
Mimba za utotoni zinazotokana na ndoa za utotoni au wakati mwingine utovu wa maadili unaopelekea wanafunzi wa kike kukatiza masomo kwa kupata mimba kumeelezwa kusababishia watoto wanaozaliwa kupata utapiamlo ama udumavu kutokana na lishe duni
Hayo yamesemwa na Mganga Mkuu wa mkoa wa Katavi Dk. Omari Sukari ambaye amefafanua kuwa mimba za utotoni zinawapa majukumu ya malezi ya watoto ambao nao wanahitaji kulelewa
Amesema hali hiyo inapelekea watoto kupata udumavu kutokana na sababu mbalimbali kama wazazi kutokuwa na uelewa wa kutosha juu ya lishe bora na wakati mwingine umaskini
Dk Sukari amefafanua kuwa uwezekani wa mtoto kupata udumavu ni kati ya siku moja tangu kutungwa mimba hadi siku 1,000 ambapo hata mjamzito asipofuatilia suala la lishe bora anaweza kujifungua mtoto mwenye utapiamlo
Aidha wazazi kujikita katika shughuli za utafutaji wa riziki kwa muda mrefu pia kunapelekea watoto kupata udumavu
Bwana Ignas Kikwala ni Kaimu Afisa maendeleo ya jamii mkoa wa Katavi amesema kwa kipindi cha miezi mitatu kuanzia Oktoba 2020 hadi Januari 2021 jumla ya watoto wa kike 155 wenye umri wa kati ya miaka 12 hadi 16 wamepata mimba
‘Na hawa ni kwa mujibu wa wale walioripoti katika vituo vya afya na hospitali zetu, sasa utaona tuna tatizo kubwa kwa kiasi gani!’ Alisema Kikwala
Amesema kwa mujibu wa takwimu za kitaifa Katavi inaongoza kwa kuwa na asilimia 45 ya mimba za utotoni
Mwandishi wa habari hii amepata nafasi ya kuzungumza na Sabina Kisari (16) mkazi wa Mpanda ambaye anakiri mwanae kupata udumavu aakiwa na mwaka mmoja na nusu
Sabina anasema alikuwa akisoma kidato cha pili wakati anapata ujauzito hali iliyopelekea kukatiza masomo, na baadae kufukuzwa nyumbani kwao
Anaeleza kuwa alikwenda kuishi na mzazi mwenzie aliyekuwa akifanya kazi ya bodaboda lakini hakudumu baada ya kijana huyo kumfukuza na akalazimika kujipangia chumba na kuanza kuuza matango ili apate hela ya kujikimu
‘Niliteseka, na mimba yangu nimeuza matango badae nikajifungua nikaenda kwa shangazi lakini shangazi yangu nae ni mstaafu kwa hiyo hali ilikuwa ngumu sana’ alisema
‘Mtoto wangu alikuwa haongezeki uzito na ngozi yake ilikuwa inasinyaa ikabidi niache kumpeleka kliniki kwa kuepuka kugombezwa’ alisema
Sabina anaeleza kuwa mtoto wake alibainika kuwa ana udumavu baada ya kuugua na kumpeleka hospitali ambapo alilazwa kwa muda mrefu.
Anasema kwa sasa mtoto amekuwa na afya njema na kutoa wito kwa wanafunzi kutopenda starehe
Kwa upande wake Mkuu wa mkoa wa Katavi Juma Homera ametaka kila kata kutengeneza mabalozi wa siri watakaokuwa wakifuatilia watu wenye malengo hasi na watoto wa kike sanjari na kuripoti na kufuatilia wanafunzi watakaobainika wana mimba
Homera amesema hatua hiyo inaweza kutokomeza mimba za utotoni na ndoa za utotoni ambapo amekemea jamii inayoozesha watoto wadogo