Kushoto Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dk. Dorothy Gwajima alipokuwa mkoani Katavi kwa ziara ya kikazi akiwa na Mkuu wa mkoa wa Katavi Juma Homera
Watoto wakipatiwa chanjo na Mratibu wa Afya ya mama na Mtoto Sista Elida Machungwa katika Kituo cha Afya Mamba halmashauri ya Mpimbwe mkoani Katavi
……………………………………………………………………………………….
NA Zillipa Joseph, Katavi
Waziri wa Afya maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto Dakta Dorothy Gwajima amewataka maafisa lishe wa mkoa na wilaya za mkoa wa Katavi kuandaa kalenda maalum zitakazokuwa zinafundisha namna ya kumlisha mtoto ili kuondokana na tatizo la udumavu
Dakta Gwajima ametoa agizo hilo alipofanya ziara ya kikazi mkoani hapa ambapo amesema kalenda hizo zitasaidia kuongeza uelewa kwa wananchi hasa waishio maeneo ya vijijini
‘Tengeneza kalenda lenye picha za vyakula vyote sambaza kwenye ofisi za kata, zahanati na maeneo mengine wakienda kuhudumiwa huko wanapata na elimu’. alisema Dk. Gwajima
Ameongeza kuwa kalenda hizo zitabeba orodha ya makundi ya vyakula kulingana na asili ya vyakula vinavyopatikana katika kila Halmashauri na itaje vyakula gani vinafaa kwa mlo wa asubuhi, mchana na jioni
Akizungumzia changamoto hiyo mkuu wa mkoa wa Katavi Juma Homera amesema tatizo kubwa ni uelewa duni wa wananchi wa namna ya kula mlo kamili wakati Katavi ina vyakula vya kutosha
‘Hii ni nchi ya asali na maziwa, tunaposema hivyo si kwamba tunajisifia bali ni kwa sababu vyakula vya aina yote vinastawi hapa. Tuna karanga, viazi, ufuta, mahindi, mchele, kunde, maharage, choroko, ni vyakula vingi kwa kweli’ alisema Homera
Homera ameongeza kuwa licha ya kuwa na mifugo mingi maziwa yanayopatikana kutokana na mifugo hiyo yanaishia kwenye biashara huku familia ikiachwa bila maziwa ya kunywa
Amesema kuwa familia zilizo nyingi mkoani hapa zinatumia wali kama chakula kikuu bila kufuata mchanganyiko wa vyakula hali inayopelekea udumavu kwa watoto
Akizungumzia tatizo la udumavu Mganga Mkuu wa mkoa wa Katavi Dk. Omari Sukari amesema mpaka mwaka 2020 asilimia 33 ya watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano waligundulika na tatizo la udumavu
Dk. Sukari amesema watoto hao ni wale waliofikishwa katika zahanati na vituo vya afya ambapo walipata huduma ikiwemo ya kinamama kufundishwa jinsi ya kumlisha mtoto
Aidha emeongeza kuwa mzazi mwenye kumjali mtoto wake licha ya vyakula pia anatakiwa alinde afya ya mtoto kwa kuhakikisha mtoto anapata chanjo zote ili kumkinga na maradhi mbalimbali