Home Mchanganyiko BILLIONEA MADINI YA RUBY TUNASIKITIKA HAYATI RAIS DKT MAGUFULI ALITUTHAMINI WACHIMBAJI WADOGO.

BILLIONEA MADINI YA RUBY TUNASIKITIKA HAYATI RAIS DKT MAGUFULI ALITUTHAMINI WACHIMBAJI WADOGO.

0

Bilionea wa madini ya Ruby Sendeu Laizer akiwa ameshikilia madini ya hayo

*******************************
NA NAMNYAK KIVUYO, ARUSHA.
Billionea wa madini ya Ruby Sendeu Laizer amesema wamepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za kifo cha Hayati Rais Dkt John Magufuli kwani aliwathamini wachimbaji wadogo na kuwapatia haki ya kumiliki migodi.
Sendeu Laizer aliyasema hayo wakati akiongea na waandishi wa habari ambapo alisema kuwa kwa aliyowatendea hawakutegemea kuwa watakuwa nae kwa muda mfupi lakini wanamuhimidi Mungu kwakuwa kila mmoja wao ataonja mauti.
Alisema kuwa Hayati Rais Dkt Magufuli watamkumbuka daima kwani aliwathamini wao wachimbaji wadogo ambao ni wazawa wa Tanzania na kuwapa haki zote za kumiliki migodi na kuendelea kufanya kazi za madini  bila kuwadharau kwamba hawataweza kufanya.
“Kwa kutumia ujasiri aliotupatia na nguvu zetu sisi wenyewe hatujamuangusha kwani tumefanya kazi kwa bidii na tunaendelea kufanya ili kuendeleza taifa letu na kufikia uchumi wa kati ulioimarika,”Alisema Sendeu. 
Alifafanua kuwa wachimbaji wengi wadogo kutokana na jitihada za Hayati Rais Dkt Magufuli wachimbaji wazawa hivi sasa wanamiliki migodi na kufanya ya uchimbaji bila woga wowote tofauti na awali ambapo wageni ndio walikuwa wanaonekana kuwa wanaweza zaidi.
“Kwakweli  kifo chake kimetusononesha sana kwasababu bado tulikuwa tunamuhitaji kwa mengi mapya na kuendeleza aliyokwisha kuyaanzisha kwani alikuwa ni mtu mwenye maono makubwa kwa nchi yake,” Alieleza.
Aliendelea kusema kuwa hakuna mgodi wa wazawa ulisimama bila kufanya kazi, kazi zinaendelea na ndio mana pato la wizara ya madini limepanda kuliko wakati mwingine wowote ambapo kwa eneo la Mundara kata ya Longido yalipo machimbo ya madini ya Ruby kuna leseni zaidi ya 100 ambazo awali ilikuwa ni leseni moja ya iliyokuwa inashughukiwa na wageni.
“Kupitia uongozi wake leseni ile ilikatwakatwa na wazawa kupewa fursa ya kumiliki jambo ambalo ilikuwa ni changamoto kubwa kwao lakini yeye aliweza kulitatua, kiukweli tunamshukuru sana japo hatupo naye tena, tunamuombea kwa Mungu ampe pumziko la amani,” Alisema.