MGOMBEA Uwakilishi Jimbo la Pandani kwa Tiketi ya CCM Mohamed Juma Ali(kulia) akieleza vipaumbele vyake na kuomba kura kwa wananchi, akiwa na Mwenyekiti wa UVCCM Taifa Kheir James (kushoto) mara baada ya kumnadi katika mkutano wa hadhara wa CCM wa uchaguzi mdogo wa jimbo hilo uliofanyika katika viwanja vya Shenge juu Pemba.
Mwenyekiti wa UVCCM Taifa Kheir James akiwahutubia wananchi katika mkutano wa hadhara wa kumnadi Mgombea Uwakilishi kwa tiketi ya CCM Mohamed Juma Ali, mkutano huo umefanyika katika viwanja vya Shenge juu Pemba.
******************************************
NA IS-HAKA OMR, ZANZIBAR.
Mwenyekiti wa UVCCM Taifa ambaye pia Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM Kheri James (MCC), amewasihi wananchi wa jimbo la Pandani kuchagua kiongozi mwenye fikra,maono na kiu ya kuwaletea maendeleo bila kujadi tofauti za kisiasa na kidini.
Amesema kiongozi mwenye sifa hizo anatokana na Chama Cha Mapinduzi ambaye ni Mohamed Juma Ali, anayegombea nafasi ya Uwakilishi kwani ni mtu mchapa kazi na mwenye nia ya dhati ya kuwatumia kwa uadilifu mkubwa.
Nasaha hizo alizitoa wakati jana akimnadi mgombea huyo katika kampeni za CCM za Uchaguzi mdogo wa jimbo hilo zilizofanyika katika viwanja vya Shenge juu Pandani, Pemba.
Alisema mgombea huyo ni mtu wa watu anayejua changamoto za wananchi na hivyo itakuwa rahisi kuzitatua kwani amekuwa ni miongoni mwa wananchi wazalendo.
Kheir , ambaye pia ni mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM, alisema jimbo hilo linahitaji kiongozi makini anayetokana na chama chenye uzoefu wa muda mrefu katika kuwatumikia wananchi.
“Nakuombeni msipote bahari hii fanyeni maamuzi ya kumpa ridhaa mgombea wa CCM ambaye ni Mohamed Juma Ali bado ni kijana anayeweza kufanya kazi kwa muda mrefu, anashaurika, hana majivuno, anapenda na kuheshimu watu wa rika zote”. , alisema Kheir katika mkutano huo.
Aliwaomba wananchi wa makundi mbalimbali ndani ya jimbo hilo kujitathimini kwa kina kwa kupima miaka mingi ambayo jimbo hilo lilikuwa mikononi mwa wapinzani nini kilifanyika kasha wafanye maamuzi sahihi ya kumpigia kura nyingi mgombea huyo ili aweze kufanya mapinduzi ya kimaendeleo kwa haraka.
Alisema endapo watamchagua mgombea huyo watakuwa wamechagua kiongozi sahihi wa kusaidiana na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi, katika utekelezaji wa shughuli za maendeleo.
Katika maelezo yake Kheir, alisisitiza kulinda na kuheshimu maridhiano ya kisiasa yaliyofanywa na viongozi wakuu ambayo yanatakiwa kutekelezwa kwa vitendo ili Pemba iendelee kuwa na amani na utulivu mkubwa.
“Wananchi na Wanachama wa CCM endeleeni kuiamini CCM ili kuhakikisha Utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi uendelee kutekelezwa kwa Kasi ya hali ya juu chini ya kiongozi makini Mohamed Juma Ali.
Mgombea ambaye yeye mwenyewe ni mpambanaji anayepambania nafsi yake na anayepambania kundi la wapambanaji wenzake ambaye anafahamu changamoto nyingi za kijamii.” ,alisema Kheir.
Alisema mgombea ambaye anaumwa na uchungu wa Zanzibar yote bali anawatizama wapiga kura wa Pandani sio kwa Upemba bali uzanzibar wao.
Alisema Mgombea anawakilisha kundi la vijana,wafanyabiasha na kundi la vijana waangaikaji na asiyejivunia kuwa na majumba pemba bali anajivunia kuishi na wenzake.
Kwa upande wa Mgombea uwakilishi kwa tiketi ya CCM Mohamed Juma Ali, aliahidi kutatua changamoto mbalimbali zikiwemo za ukosefu wa shule ya msingi,ujenzi wa kituo cha afya chenye vifaa tiba vya kisasa.
Alisema ataongeza uzalishaji wa chumvi kupitia mabwawa,kuwezesha vikundi vya ujasiriamali vya akina mama, kuimarisha michezo kwa kuibua vipaji vya vijana sambamba na kutengeneza daraja linalounganisha shehia ya Shenge juu na Maziwani.
Kampeni hizo za uchaguzi mdogo zinafanyika kufuatia kufariki kwa aliyekuwa Mwakilishi mteule wa Chama Cha ACT-Wazalendo katika Jimbo hilo Abubakari Khamis Bakar.