Home Mchanganyiko ZAIDI YA WANANCHI 3000 KIJIJI CHA KATETE MKOANI RUKWA KUNUFAIKA NA HUDUMA...

ZAIDI YA WANANCHI 3000 KIJIJI CHA KATETE MKOANI RUKWA KUNUFAIKA NA HUDUMA YA MAJI

0

Mkuu wa Wilaya ya Kalambo, Karolius Misungwi (kuhoto) akiweka Jiwe la Msingi la mradi wa maji wa maji wa mserereko wa kijiji cha Katete.

Baadhi ya wananchi wa kijiji cha Katete na watendaji watendaji wa Sekta ya Maji waliofika kwenye hafla ya uwekaji wa jiwe la msingi mradi wa maji wa Katete.

Meneja wa RUWASA Wilaya ya Kalambo, Mhandisi Patrick Ndimbo akiwasilisha taarifa ya mradi wa maji wa Katete kwa Mkuu wa Wilaya ya Kalambo (hayupo pichani) wakati wa hafla ya uwekaji wa jiwe la msingi.

Meneja wa RUWASA Mkoa wa Rukwa, Mhandisi Boaz Pius akipanda mti wakati wa hafla ya utiaji saini mradi wa maji wa Katete Wilayani Kalambo, Mkoa wa Rukwa.

**************************************

Na Mohamed Saif

Zaidi ya wananchi 3,000 kutoka kijiji cha Katete Wilayani Kalambo Mkoani Rukwa watanufaika na mradi wa maji wa mserereko unaotekelezwa na Wakala wa Majisafi na Usafi wa Mazingira  Vijijini (RUWASA) Wilaya Kalambo.

Meneja wa RUWASA Wilaya ya Kalambo Mhandisi Patrick Ndimbo amesema hayo kijijini Katete alipokuwa akiwasilisha taarifa ya mradi kwa Mkuu wa Wilaya ya Kalambo, Karolius Misungwi wakati wa hafla ya uwekaji wa Jiwe la Msingi Machi 16, 2021,

Mhandisi Ndimbo alisema mradi unatekelezwa na Kampuni ya Safari General Business ya Sumbawanga kwa ufadhili wa fedha za Mfuko wa Taifa wa Maji (NWF) kwa gharama ya shilingi milioni 382.

Alibainisha kwamba kijiji hicho hakikuwa na huduma ya maji na badala yake wananchi walilazimika kutumia muda mwingi kutembea umbali mrefu kufuata huduma ya maji.

Akizungumza na wananchi wakati wa hafla hiyo Mkuu wa Wilaya ya Kalambo, Karolius Misungwi aliipongeza Wizara ya Maji kwa kutambua kero iliyokuwa ikiwasumbua wakazi wa kijiji hicho na kuitafutia ufumbuzi.

“Wizara ya Maji inafanya kazi kubwa sana, tumeshuhudia miradi mingi ikijengwa, ninaamini maeneo mengine pia ya jirani nayo yatapata huduma ya maji ni suala la muda tu,” alisema Misungwi.

Aliwasihi wananchi kuhakikisha wanatumia vyema fursa zitokanazo na mradi ili kujiletea maendeleo na pia aliwataka kuhakikisha wanatunza mradi na wanalinda miundombinu.

“Huu mradi unajengwa kwa fedha nyingi, mmeteseka kwa muda mrefu kufuata huduma mbali na hapa hivyo ni lazima muwe na uchungu wa kuhakikisha mradi unadumu, msikubali mtu auchezee,” alisisitiza Misungwi.

Aliitaka Jumuiya ya Watumiaji Maji Ngazi ya Jamii (CBWSO) ambayo inasimamia shughuli za uendeshaji na matengenezo ya mradi wa Katete kuhakikisha inatekeleza majukumu yake kwa weledi.

Hafla hiyo ya uwekaji wa jiwe la msingi la mradi wa maji wa Katete unakwenda sambamba na uzinduzi wa miradi na uwekaji wa jiwe la msingi maeneo mbalimbali kote nchini ikiwa ni kuadhimisha Wiki ya Maji mwaka 2021.