****************************************
Waziri Bashungwa ameongoza mazungumzo hayo machi 17 jijini Dar es Salaam akiwa na Wakuu wa Taasisi zilizochini ya wizara hiyo walipo kutana na Balozi wa Qatar nchini Tanzania Mhe. Hussain Ahmad Al – Homaid.
Kikao hicho kilikua na lengo la kuona namna Qatar itakavyoweza kusaidia tasnia ya Filamu nchini, Masoko kwa Sanaa za Ufundi, uendelezaji wa viwanja vya michezo pamoja na kubadilishana uzoefu katika sekta ya Habari.
“Kutokana na Ilani ya Chama chetu Tawala CCM tuna nia yakuongeza sana ajira kwa vijana na vijana wengi wapo katika sanaa na michezo, naomba ikiwezekana kupata library ya vifaa vya kutengenezea Filamu kutokana na kuwa na uhaba wa vifaa vya kisasa na wasanii wengi vijana hawa mudu gharama ya vifaa hivyo hivyo”alisema Mhe. Waziri Bashungwa.
Pia Mhe.Waziri Bashungwa ameomba ubalozi huo kuisaidia timu ya Taifa katika maandalizi yake ya michuano ya kushiriki kombe la Dunia ambapo timu hiyo ina mechi tatu wanazotarajia kucheza ili kufuzu kucheza kombe hilo.
Aidha Mhe. Bashungwa ameomba ushirikiano na Qatar katika kujenga Maktaba ya vifaa vya kuzalisha filamu ambayo Serikali imedhamiria kuijenga kwa lengo la kukuza tasnia hiyo na kuongeza ubora kwa kazi za filamu zinazozalishwa nchini.
Kwa upande wake, Balozi wa Qatar ameahidi kushirikiana na Serikali ili timu ya Taifa iweze kupata nafasi kushiriki katika kombe la Dunia linaloandaliwa na nchi hiyo mwaka 2022.
Vilevile Mkuu wa Taasisi ya Chuo cha Sanaa Bagamoyo (TaSUBa) Dkt. Herbet Makoye ameomba ubalozi huo kushirikiana na Taasisi hiyo katika kubadilishana washiriki katika Tamasha la kimataifa la Bagamoyo international festival na Qatar Art Festival ili kujijengea ujuzi zaidi katika tamaduni na sanaa za nchi zote mbili.