Mnufaika wa mpango wa kunusuru Kaya Masikini kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) wilayani Iramba mkoani Singida, Magreth Peter akiswaga ng’ombe wake aliowapata baada ya kuwezeshwa na mpango huo..
Mnufaika wa mpango wa kunusuru Kaya Masikini kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) Magreth Peter (kushoto) mkazi wa Kijiji cha Kengege akizungumza na viongozi wa kijiji hicho pamoja na maafisa habari kutoka TASAF makao makuu waliomtembelea kujua mafanikio yake na changamoto alizo nazo.
Mnufaika wa mpango huo, Ukende Kidyusi akiwa na wajukuu zake mbele ya nyumba yake ya kisasa aliyoijenga baada ya kuwezeshwa na TASAF.
Mnufaika wa mpango huo, Joyce Mpugi akiwa na mume wake mbele ya nyumba yao ya kisasa waliyoijenga baada ya kuwezeshwa na TASAF huku wakiwa na kuku ambao ni zao lililotokana na mpango huo..
Nyumba ya tembe iliyo kuwa ikitumiwa na Mariam Danford na wazazi wake kabla ya kujengwa nyumba yao ya kisasa.
Hii ni nyumba ya kisasa ya wazazi wake Mariam Danford baada ya kuwezeshwa ma TASAF.
Mariam Danford (kulia) akizungumzia mafanikio waliyopata kutoka TASAF.
Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Kijiji cha Kengege, Edward Mdende akizungumzia jinsi TASAF ilivyo wawezesha kulifanyia matengezo lambo la maji ambalo linawasaidia katika shughuli mbalimbali za kijamii.
Betha Simon akizungumzia faida za lambo hilo.
Mratibu wa TASAF wilayani humo, Adamu Msangi akizungumzia utekeleza wa mpango huo.
Na Dotto Mwaibale, Iramba
WANUFAIKA wa mpango wa kunusuru Kaya Masikini kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) wilayani Iramba mkoani hapa wameomba kutembelewa mara kwa mara na wataalamu wa kilimo, mifugo na biashara ili waweze kuwasaidia kupata faida badala ya hasara.
Maombi hayo yametolewa jana kwa nyakati tofauti na wanufaika hao wa Kijiji cha Kengege wakati wakizungumza na waandishi wa habari na maofisa wa mfuko huo ambao wapo katika ziara ya kuwatembelea ili kujua mafanikio na changamoto walizo nazo.
Mnufaika wa mpango huo Magreth Peter ambaye hujishughulisha na kilimo pamoja na ufugaji wa nguruwe na ng”ombe alisema changamoto kubwa waliyonayo ni kukosa wataalamu wa kuwapa elimu ya ufugaji na kilimo pamoja na biashara.
“Tunashindwa kupiga hatua kutokana na kupata matunda kidogo yatokanayo na kazi zetu kwa sababu ya kukosa wataalamu hao ambao hapa kwangu walifika mwaka juzi na hawajarudi tena” alisema Peter.
Aidha Peter alisema kutokuwa na elimu ya biashara kumechangia kwa kiwango kikubwa kuuza mifugo yao kwa bei ya chini kupitia walanguzi na madalali akitolea mfano alipouza nguruwe wake 11 kwa sh.milioni 1.8 tu.
Mnufaika mwingine Ukende Kidyusi anaye jishughulisha na kilimo na ufugaji kazi zilizo msaidia kujenga nyumba ya kisasa baada ya kuwezeshwa na TASAF anasema elimu ndogo wanayopata kutoka kwa wataalamu hao wanayoitoa kwenye mikutano ya hadhara bila ya kufika zilipo shughuli hizo zina warudisha nyuma licha ya TASAF kuwa na maono mazuri ya kuziinua kaya Masikini.
Mratibu wa TASAF wilaya hiyo Adamu Msangi alisema mara kwa mara wanapokutana na wataalamu hao katika mikutano ya kiutendaji wamekuwa wakihimiza kuwatembelea walengwa wa mradi huo kwa ajili ya kujua changamoto zao za kilimo na ufugaji ili kuzipatia ufumbuzi haraka.
Akizungumzia utekeleza wa mpango huo alisema halmashauri hiyo ilipokea kiasi cha sh. 7,716,971,481 kutoka Serikali kuu ambapo kwa mwaka 2014/ 2020 wametumia sh.5,049,115,890 kwa ajili ya uhaulishaji fedha za ruzuku na utimizaji wa masharti ya afya na elimu.
Alisema kwa mwaka 2016/2020 walitumia sh.2,032,809,000 kwa ajira ya muda mfupi.
Aidha Msangi aliongeza kuwa mwaka 2018/2020 walitumia sh.300,750,000 kwa ajili ya kinga dhidi ya maambukizi ya virusi vya ulimi na athari za ukimwi kwa wasichana balehe na wanawake vijana walio ndani ya mfumo wa shule (Timiza malengo)
Alisema mwaka 2018/2020 walitumia sh.23,963,500 kwa ajili ya kuwawesha wananchi kiuchumi na kuwa mwaka huo huo walitumia sh.170,304,091 kutoa kinga dhidi ya maambukizi ya virusi vya ukimwi kwa vijana walio nje ya mfumo wa shule (Timiza male ngo)
Wanufaika wengine wa mpango huo ni Joyce Mpugi ambaye anajishughulisha na kilimo, ufugaji wa kuku, mbuzi na ng’ombe, Ukende Kidyusi na Mariam Danford ambapo wote kwa pamoja wamefanikiwa kuondoka kwenye nyumba za matembe walizokuwa wakiishi baada ya kujenga za kisasa.