Kampeni iliyopewa jina la ‘Kijana Ni Usafi’ ambayo inalenga kuhamasisha tabia ya usafi miongoni mwa vijana nchini Tanzania imezinduliwa leo Jumatano mkoani Morogoro. Kampeni hiyo ya miezi sita inayotekelezwa na Shirika la Msaada la Uingereza (UKAID) inalenga wanawake na wanaume wenye umri wa miaka 15-35. Kampeni hiyo inatarajia kuwafikia vijana 48,000 katika mikoa minne ambayo ni Iringa, Dodoma, Dar es Salaam na Morogoro.
Kampeni hiyo inakusudia kuhamasisha vijana kuzingatia tabia chanya za usafi kama vile kunawa mikono, kutumia maji salama, udhibiti wa taka na usafi binafsi. Ili kufikia malengo ya kampeni ya Kijana Ni Usafi, Raleigh Tanzania ambao ndio waratibu wa kampeni hiyo imechagua na kuwajengea uwezo juu ya elimu ya usafi vijana 2500 wenye ushawishi katika jamii. Vijana hao kutoka katika mikoa minne iliyochaguliwa watatumika kuwajengea uwezo vijana wengine katika jamii zao ili kuhakikisha wanazingatia usafi.
Kampeni ya Kijana Ni Usafi imeundwa kwa kuzingatia mahitaji mahsusi ya usafi kwa kila mkoa. Kwa mfano, mkoani Dar es Salaam, kampeni inalenga kuhamasisha udhibiti wa taka. Kwa Dar es Salaam kampeni imepewa jina la “Vunja Urafiki na Uchafu; Acha Mazoea. Kampeni inalenga kuhamasisha vijana mkoani Dar es Salaam kuchukua hatua kudhibiti taka. Hii ni kwa sababu Dar es Salaam ni moja ya mikoa ambayo inakabiliwa na changamoto kubwa ya udhibiti wa taka.
Mkoani Iringa kampeni imelenga pia kuhamasisha udhibiti wa taka lakini kwa njia tofauti. Iringa wamechukulia taka kuwa fursa ya biashara. Kampeni imepewa jina la “Taka ni Mchongo; Kamata Utajiri” Vijana mkoani Iringa wanafundishwa namna wanavyoweza kugeuza taka kuwa fursa.
Mkoani Dodoma, kampeni ya Kijana Ni Usafi imelenga kuhamasisha usafi binafsi kwa vijana. Kampeni imepewa jina “Uchafu Sio Dili, Ng’aa Kijanja” ikilenga kuwashawishi vijana wa Dodoma kuimarisha usafi binafsi.
Mkoani Morogoro, lengo kuu la kampeni ni kuhimiza matumizi ya maji salama katika jamii. Sababu kubwa ni kwamba mkoa wa Morogoro umeathiriwa na magonjwa kama vile homa ya matumbo, kuhara na mlipuko wa kipindupindu mara kwa mara. Wanajamii wanaathirika kutokana na tabia ya kutumia maji yasiyo salama. Kampeni imepewa jina la “Tumia Maji Salama, Okoa Mkwanja” kuonesha vijana namna ambavyo matumizi ya maji salama yatawaepusha na gharama za kutibu magonjwa.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa kampeni hiyo, Mratibu wa Mradi, Augustino Dickson amesema kampeni ya ‘Kijana Ni Usafi’ inalenga kundi la vijana kwa sababu vijana ni kundi lenye idadi kubwa ya watu nchini Tanzania. Bwana Augustino ameongeza kuwa vijana wanaweza kuwa wakala wa mabadiliko chanya katika jamii endapo watajengewa uwezo kuhusu mambo muhimu ikiwemo elimu ya usafi.
“Vijana wa Tanzania wanahitaji kuelimishwa juu ya masuala mbalimbali ili kuweza kuchangia maendeleo ya nchi yao. Raleigh Tanzania imekuwa ikifanya kazi ya kuwapa vijana ujuzi katika maeneo mbalimbali ikiwa ni pamoja na ujuzi wa ujasiriamali. Kupitia kampeni hii tumejikita katika kuwaelimisha vijana kuhusu usafi ili waweze kutawala mazingira yao.” Amesema Augustino.
Augustino pia amesema kuwa vijana ndio watekelezaji wa ajenda ya maendeleo nchini Tanzania kama ilivyoainishwa katika Dira ya Maendeleo ya 2025 ya Tanzania na Malengo ya Maendeleo Endelevu ya 2030. Augustino alisisitiza kuwa kuelimisha vijana juu ya usafi ni muhimu sana katika kuweka mustakabali endelevu kwa jamii yoyote.
“Malengo ya kampeni hii yanaakisi Dira ya Maendeleo ya Tanzania ya 2025 na Ajenda 2030 (Malengo ya Maendeleo Endelevu) kwa sababu inaandaa vijana ili sio tu kufahamu umuhimu wa usafi lakini pia kuwa waangalizi wa mazingira yao. Hii ni muhimu sana kwa sababu ikiwa, watu ambao wana jukumu la kulea mustakabali wa taifa letu na ulimwengu wetu hawawajibiki kwa usafi wao binafsi na ustawi wa mazingira yao kuna uwezekano wa kutokuwa na maandalizi mazungi wa mazingira ya baadae.” Amesema Bwana Augustino
Akimalizia hotuba yake Augustino amesema kuwa kampeni hiyo inachagiza mipango ya Raleigh Tanzania na washirika wengine inayolenga kuwawezesha vijana.
“Sisi [Raleigh Tanzania] tunaamini kuwa kampeni hii itachochea juhudi zinazofanyika na wadau mbalimbali kuwawezesha vijana wa Tanzania kupata ujuzi wa masuala mbalimbali. Natoa wito kwa vijana wote watakaofikiwa na mradi huu kuwa tayari kupokea maarifa ambayo watapata kupitia kampeni hii na kutumia maarifa hayo katika kuchochea mabadiliko chanya katika jamii zao. ” Alihitimisha Augustino.
Vijana katika mikoa yote iliyochaguliwa watawezeshwa kupitia semina za mafunzo, kampeni kwenye vyombo vya habari na kupitia vipeperushi.