Home Mchanganyiko TASAF KUJENGA WODI YA AKINA MAMA NA MAABARA KIJIJI CHA MKAMBARANI

TASAF KUJENGA WODI YA AKINA MAMA NA MAABARA KIJIJI CHA MKAMBARANI

0

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa, Mhe. Humphrey Polepole (Mb) akitoa maelekezo kwa Serikali kuhusu ujenzi wa wodi ya kuwahudumia akina mama wajawazito na maabara katika zahanati ya Kijiji cha Mkambarani.

Baadhi ya wananchi wa Kijiji cha Mkambarani-Morogoro wakimsikiliza Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa, Mhe. Humphrey Polepole (hayupo pichani) wakati wa ziara ya kikazi ya kamati hiyo iliyolenga kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF kijijini hapo.

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa, Mhe. Humphrey Polepole (Mb) na baadhi ya wajumbe wa kamati yake pamoja na watendaji wa Serikali wakikagua zahanati ya Mkambarani wakati wa ziara ya kikazi ya kamati hiyo iliyolenga kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF kijijini hapo.

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi akizungumza kuhusu utekelezaji wa maelekezo ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa wakati wa ziara ya kikazi ya kamati hiyo iliyolenga kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF katika Kijiji cha Mkambarani – Morogoro.

Mmoja wa wanufaika wa TASAF wa Kijiji cha Mkambarani Mzee Abdallah J. Kinyaku akitoa ushuhuda wa namna alivyonufaika na TASAF kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa wakati wa ziara ya kikazi ya kamati hiyo iliyolenga kukagua utekelezaji wa mpiradi ya TASAF kijijini hapo.

*******************************************

Na. James K. Mwanamyoto-Morogoro

Tarehe 15 Machi, 2021

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi ameiahidi Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa kupitia TASAF kujenga wodi ya kuwahudumia akina mama wajawazito na maabara katika zahanati ya Kijiji cha Mkambarani ili wananchi wa kijiji hicho wapate huduma bora za afya.

Mhe. Ndejembi ametoa ahadi hiyo ikiwa ni utekelezaji wa maelekezo ya kamati hiyo ya kudumu iliyoelekeza Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) kujenga jengo la kina mama kwa ajili ya kuwapatia huduma stahiki, ikiwa ni pamoja na kujenga maabara itakayotoa huduma bora ya vipimo kwa wananchi wa Kijiji cha Mkambarani.

Mhe. Ndejembi amesema, kutokana na maelekezo yaliyotolewa na kamati ofisi yake itajenga wodi ya akina mama ili kuwe na faragha wakati wa kuwahudumia akina mama wajawazito.

Kuhusu maelekezo ya ujenzi wa maabara, Mhe. Ndejembi ameihakikishia kamati na wananchi wa Kijiji cha Mkambarani kujenga maabara ili kuwaondolea adha wananchi hao ya kusafiri umbali mrefu kufuata huduma ya maabara ambapo pia hulazimika kuingia gharama kubwa.

Mhe. Ndejembi ameongeza kuwa, lengo la Serikali kujenga zahanati ya Mkambarani ni kuwasogezea karibu huduma za afya wananchi wa eneo hilo ikizingatiwa kuwa, walengwa wa TASAF watanufaika pia na huduma zinazotolewa na zahanati hiyo na hatimaye kuwa na afya bora itakayowawezesha kupambana na umaskini kupitia ruzuku ya TASAF wanayoipata.

Awali, akitoa maelekezo kwa Serikali kwa niaba ya kamati yake, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa, Mhe. Humphrey Polepole (Mb) amesema Kamati imelazimika kutoa maelekezo ya ujenzi wa Wodi ya akina mama na maabara kama sehemu ya kulinda utu wa wananchi hususani akina mama wanaofuata huduma ya uzazi katika zahanati ya Mkambarani.  

Mhe. Polepole amesema, wodi ya akina mama ikijengwa itaongeza usiri na faragha wakati wa kuwahudumia wajawazito tofauti la ilivyo sasa ambapo hakuna usiri wa kutosha wala faragha pindi akina mama wanapohudumiwa.

Kuhusiana na maelekezo ya ujenzi wa maabara, Mhe. Polepole ameeleza kuwa, kamati yake imepata fursa ya kuitembelea zahanati ya Mkambarani na kubaini kuwa hakuna maabara inayokidhi mahitaji ndio maana kamati yake imeielekeza Serikali kujenga maabara itakayokidhi kutoa huduma stahiki kwa wananchi wa Kijiji cha Mkambarani.

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa imemaliza ziara ya kikazi ya siku tatu mkoani Dar es Salaam, Pwani na Morogoro iliyolenga kukagua utekelezaji wa miradi inayotekelezwa na taasisi zilizo chini ya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora.