Kaimu Kamanda wa Kikosi cha Jeshi la Kujenga Taifa cha 841 KJ, Mafinga, mkoani Iringa, Luteni Kanali Issa Chalamila,akizungumza na waandishi wa habari leo March 14,2021 kabla ya kuanza ziara ya utekelezaji wa miradi ya JKT, ambapo Kikosi hicho ni mahsusi katika ufugaji wa ng’ombe wa maziwa na wakuzalisha mitamba pamoja na mbuzi na kondoo.
Ng’ombe wa maziwa wanaofungwa katika Kikosi cha Jeshi la Kujenga Taifa cha 841 KJ, Mafinga, mkoani Iringa.
Mbuzi na Kondoo ambao wanapatikana katika Kikosi cha Jeshi la Kujenga Taifa cha 841 KJ, Mafinga, mkoani Iringa.
Kaimu Kamanda wa Kikosi cha Jeshi la Kujenga Taifa cha 841 KJ, Mafinga, mkoani Iringa, Luteni Kanali Issa Chalamila,akiwaelezea waandishi wa habari jinsi kikosi hicho kilivyojipanga kuongeza eneo la kilimo kutoka ekari 200 hadi 500 na kuongeza uzalishaji wa ng’ombe, mbuzi na kondoo mara baada ya kujionea utekelezaji wa miradi ya JKT,katika ziara iliyofanyika leo March 14,2021 Mafinga Mkoani Iringa.
Bwana mifugo na shamba wa kikosi cha 841 KJ Mafinga Luteni Francis Breck,akizungumza na waandishi wa habari kuwa kuna ekari 22 za malisho ya kupanda yanayosaidia kulisha ng’ombe wakati wa kiangazi na mpango uliopo ni kuongeza hekari 50 katika ziara ya utekelezaji wa miradi ya JKT,iliyofanyika leo March 14,2021 Mafinga Mkoani Iringa.
Mkufunzi Mkuu 841 kikosi cha Jeshi Meja Victor Nkya,akiwaelezea waandishi wa habari jinsi kikosi hicho kimekuwa kikitoa vijana bora katika mafunzo ya ufugaji pamoja na kilimo wanayopatiwa kikosini hapo wakati wa ziara ya utekelezaji wa miradi ya JKT,iliyofanyika leo March 14,2021 Mafinga Mkoani Iringa.
Matrone Kikosi wa Vijana AKH 6612 SG Lucy Malema,akielezea jinsi wanavyofurahia mafunzo wanayoyapata na kuwajengea uwezo katika Ufugaji pamoja na Kilimo na yatawasaidia pindi watakapokuwa uraiani katika ziara ya utekelezaji wa miradi ya JKT,iliyofanyika leo March 14,2021 Mafinga Mkoani Iringa.
…………………………………………………………………………………………………
Na Alex Sonna, Mafinga
KIKOSI cha Jeshi la Kujenga Taifa cha 841 KJ, Mafinga, mkoani Iringa kimejipanga kuhakikisha kinaboresha ufugaji na kilimo ili kuweza kinajitosheleza kwa asilimia 100 na kuondokana utegemezi kutoka Serikali Kuu.
Miongoni mwa mikakati iliyowekwa ni kuanzisha kilimo cha parachichi, kuongeza eneo la kilimo kutoka ekari 200 hadi 500 na kuongeza uzalishaji wa ng’ombe, mbuzi na kondoo.
Akizungumza leo March 14,2021 katika ziara ya kuangalia utekelezaji wa mikakati na miradi ya JKT, Kaimu Kamanda wa Kikosi hicho, Luteni Kanali Issa Chalamila, amesema hatua hiyo ni katika kutekeleza azma ya Mkuu wa JKT, Meja Jenerali Charles Mbuge ya kutaka vikosi vyote vihakikishe vinajitosheleza kwa chakula.
Amesema kuwa kikosi hicho ni mahsusi katika ufugaji wa ng’ombe ambapo wanafuga ng’ombe wa maziwa na wakuzalisha mitamba.
“Katika kutekeleza azma ya Mkuu wa JKT tuna mikakati tumeiweka katika kuendeleza mifugo ikiwamo kuongeza uzalishaji wa ng’ombe wa maziwa ili kuwa na uzalishaji wa kutosha na kusambaza sehemu mbalimbali,”amesema.
Kuhusu mitamba, amesema katika mkakati wa kutosheleza kwa chakula ni kuwa na ng’ombe zaidi wa nyama ili kusambaza kwenye vikosi vya JKT, na kuuza nje ya kikosi na nje ya nchi.
Pia amesema kwasasa kuna mbuzi 192 na kuwa mikakati no kuwa na mbuzi 300 na kuongeza uzalishaji wa maziwa kutoka lita 200 hadi 250 kwa siku hadi kufikia lita 1,000 kwa siku.
“Kikosi pia kinajishughulisha na kilimo, kikosi mara ya kwanza kilikuwa kinalima heka 200 tu za mahindi ya chakula katika kutekeleza azma ya Mkuu wa JKT kwasasa kikosi kimelima hekari 500 za mahindi, alizeti na maharage,”amesema.
Ameeleza hatua hiyo inalenga kuhakikisha JKT inajitosheleza kwa chakula na kuipunguzia mzigo serikali na kutakuwa kwa asilimia 100 bila kutegemea fedha kutoka Serikali Kuu.
Kuhusu parachichi, Kamanda huyo amesema zao hilo lina soko la kutosha ndani na nje ya nchi hivyo kwa mwaka huu kikosi kimejipanga kuanza kulima.
“Pia kule Ruaha Mbuyuni tuna mpango wa kuanza kilimo cha vitunguu, itasaidia kutekeleza azma ya kujilisha na tunategemea tutaweza,”amesema.
Kwa upande wake Luteni Francis Breck,ambaye pia ni Bwana mifugo na shamba wa kikosi hicho, amesema ili kuendana na mabadiliko ya kuimarisha ufugaji, kikosi kinaongeza ekari 50 mbali na ekari 22 za malishao ya kupandwa ambayo tayasaida mifugo kuwa na chakula cha kutosha wakati wa kiangazi
Naye Mkufunzi Mkuu wa kikosi hicho, Meja Victor Nkya amesema kuwa kupitia miradi inayotekelezwa kikosini hapo imekuwa fursa kwa vijana wa kujitolea na wale wa mujibu wa Sheria kujifunza stadi.
“ mrejesho tunaoupata kutoka kwa vijana wetu pindi wanapomaliza mafunzo na kwenda kuajiriwa na kujiajiri inaonesha Mafinga JKT tuko vizuri.”