Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja (katikati) akiiomba kamati ya Bunge ya Ardhi Maliasili na Utalii isaidie kuhamasisha Utalii wa ndani wakati wa Kikao kifupi cha Majadiliano, Mapendekezo na Maelekezo kilichofanywa na Kamati hiyo katika ukumbi wa mikutano wa Sao- Hill mkoani Iringa.
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi ,Maliasili na Utalii imeipongeza Wizara ya Maliasili na Utalii kupitia Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) kwa kupunguza tatizo la ujangili hapa nchini .
Mwenyekiti wa Kamati hiyo Dkt. Aloyce Kwezi ametoa pongezi wakati wa ziara ya Kamati hiyo katika Hifadhi ya Taifa ya Ruaha na maeneo yanayosimamiwa na Wakala wa Hudma za Misitu Tanzania (TFS) ambapo amesema hatua hiyo imesaidia kwa kiasi kikubwa kuongezeka kwa idadi ya wanyama.
“Napongeza kazi kubwa iliyofanywa na Wizara, TANAPA wamefanya kazi kubwa sana ya kupunguza ujangili, hili limesaidia kuongezeka kwa idadi ya wanyamapori hapa nchini, pia nawapongeza TFS kwa kazi kubwa ambayo wameifanya” Amesema Dkt Kwezi
Kuhusu uboreshaji wa miundombinu maeneo ya Hifadhi, Kamati hiyo imeishauri Wizara katika kipindi hiki cha Bajeti kufuatilia kwa karibu ujenzi wa Barabara inayotoka Iringa kuelekea katika Hifadhi ya Taifa ya Ruaha .
“Tunaomba suala hili lifuatiliwe kwa ukaribu katika kipindi hiki cha bajeti, barabara ya kuingia katika Hifadhi ya Taifa ya Ruaha bado ina changamoto, lazima iwekewe nguvu na sisi tuko pamoja na kwenye jambo hili kuhakikisha limefanikiwa kwa sababu hifadhi hii ina vivutio vizuri sana . Amesisitiza Dkt. Kwezi
Mwenyekiti huyo amepongeza hatua ya ununuzi wa mitambo iliopatikana chini ya Mradi wa REGROW ya kufanya marekebisho na matengenezo ya barabara zilizoko ndani ya hifadhi akieleza kuwa hatua hiyo inapunguza gharama na kufanya ukarabati uwe endelevu.
“Nawapongeza kwa hatua hii, mnapokuwa na mitambo yenu wenyewe mnapunguza gharama na kufanya utengenezaji wa barabara za ndani ya hifadhi uwe endelevu” Amesema.
Kuhusu utengenezaji wa bidhaa zitokanazo na mazao ya misitu amesema kuwa Kamati ingependa kuona tekinolojia ya ubunifu ya kutengeza mkaa mbadala inasambazwa kwenye maeneo mengi hapa nchini ili wananchi waweze kuitumia kukailiana na tatizo la matumizi ya mkaa ambao umekua chanzo cha uharibifu wa Mazingira.
Mbali na hilo amesema takribani hekta 662 zimepotea kwa moto kichaa na kuisababishia Serikali hasara jambo lililoifanya Kamati hiyo kutoa maagizo kwa Kamati ya Ulinzi na Usalama mkoani humo idhibiti matukio hayo kwa kuweka Sheria ambazo zitasaidia kuondoa hasara hiyo.
Kwa upande wake Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Damas Ndumbaro ameiambia Kamati hiyo kuwa Wizara itayafanyia kazi maelekezo na ushauri uliotolewa na kamati hiyo.
“Ninawashukuru kwa ziara hii pamoja na maelekezo mliyoyatoa , kama mnavyofahamu Hifadhi ya ya Ruaha ina ukubwa wa Kilometa za Mraba 22,000, eneo eneo hili ni kubwa kuliko hata baadhi ya nchi pia ni kubwa kuliko Mkoa wa Mtwara, na kwa kiasi kikubwa miundombinu yake sio mizuri hasa upande wa Ruaha kusini, hili tutalifanyia kazi “Amesema Dkt. Ndumbaro
Naye Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja amesema amepokea ushauri uliotolewa na kamati hiyo na kuahidi kuufanyia kazi huku akieleza kuwa barabara inayotoka Iringa kwenda Hifadhi ya Taifa ya Ruaha imeshaanza kufanyiwa kazi na ipo katika hatua ya upembuzi yakinifu .
“Kwa kuwa tunaelekea kwenye bajeti, barabara hii tutaipa kipaumbele Ili iweze kutengenezwa na kupitika vizuri “