*****************************
March 13
BAADHI ya wakazi wa mtaa wa Kitende na Kwamfipa wilayani Kibaha ,mkoani Pwani ,wameondokana na kero ya kutembea wakati mwingine kutumia gharama za usafiri ,kufuata huduma ya afya mbali, baada ya kujengwa kituo cha afya cha Kibaha specialized polyclinic (KSP),ambacho kimekuwa mkombozi kwao.
Katika kipindi cha nyuma wakazi hao walikuwa wakitaabika kwenda kituo cha Mwendapole ,na wakati mwingine hospital ya rufaa ya Tumbi kutokana na ukosefu wa zahanati na kituo cha afya katika eneo hilo hususan vya serikali.
Akizungumzia changamoto za kiafya wakati wa ufunguzi wa kituo cha afya cha KSP ,mkazi wa Kwamfipa bibi Mariam Shomari (77),yeye alisema ,wazee na watoto walipata shida nyakati hasa za usiku kufuata huduma ya afya Mwendapole ambapo ni umbali wa km mbili kwenda na kurudi ama kutumia mabasi madogo ya abiria na pikipiki.
“Tunapata shida ,mimi ni mzee,nasumbuliwa na ugonjwa wa moyo ,moyo wangu ni mkubwa ,nalazimika nauli kila wiki kufuata huduma Tumbi ambako zaidi ,pesa sina na watoto wangu wanagharamika sana ,nadhani kungekuwepo hospital ya serikali tungepata ahueni”
Bibi Mariam aliiomba serikali, iangalie namna ya kusogeza huduma kwa kuwajengea zahanati huku wakiendelea kutumia vituo vya watu binafsi ambavyo kwasasa ndio mkombozi kwao.
Mwenyekiti wa mtaa wa Kitende, Mchello Mintanga alieleza ,awali kulikuwa na changamoto ya ukosefu wa dawa kwenye zahanati zilizo karibu nao na kufuata huduma za kiafya umbali mrefu ambazo kwasasa zimebakia historia licha ya mahitaji ya zahanati ama kituo cha afya cha serikali.
Kwa upande wake ,mkurugenzi mkuu wa kituo cha afya cha KSP ,mphamasia Stephen Stephen alisema ,ameguswa kujenga kituo hicho ili kuwakomboa wananchi wa maeneo hayo na kuunga mkono juhudi za serikali katika sekta ya afya ya kusogeza huduma karibu na wananchi.
“Rais wetu John Magufuli anaipambania sekta ya afya kupunguza changamoto za miundombinu ,dawa,vifaa tiba hivyo wadau ni wajibu wetu kushirikiana nae kutatua changamoto hizo ” alielezea Stephen.
Stephen anasema, kituo cha afya KSP ,kinatoa huduma masaa 24 ambapo katika ufunguzi huo wametoa huduma bure ya kupima shinikizo la damu,uwiano wa uzito na urefu,uchunguzi wa saratani ya matiti,upimaji wa virusi vya ukimwi,upimaji wa tezi dume,homa ya ini ,na wametoa elimu ya kujikinga na magonjwa ya mlipuko.
Mganga mfawidhi wa KSP Dokta Emmanuel Mniko aliongeza kwamba,kwa siku wanapokea wagonjwa mbalimbali kutoka maeneo jirani ,wanapokea wenye majanga ya ajali ,magonjwa ya dharura na kwa mwezi wanapokea wagonjwa zaidi ya 1,500.