Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Bi. Mary G. Makondo akiikaribisha Kamati ya kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii Mkoani Iringa wakati wa uwasilishaji wa taarifa na ukaguzi wa mradi wa Kupanga, Kupima na Kumilikisha ardhi wa Igumbilo.
Mhe. Angelina Mabula, Naibu Waziri wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi akitoa taarifa fupi ya mradi wa Kupanga, Kupima na Kumilikisha ardhi wa Igumbilo kwa Kamati ya kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kabla ya kwenda uwandani kukagua mradi huo.
Wajumbe wa kamati ya kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii wakisoma nakufuatilia taarifa ya utekelezaji wa mradi wa Kupanga, Kupima na Kumilikisha ardhi wa Igumbilo Manispaa ya Iringa kabla ya kwenda kukagua mradi huo.
Mjumbe wa kamati ya kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii Mhe. Fratei Massay (wa tatu kutoka kushoto) akisisitiza jambo baada ya kamati kukagua mradi wa Kupanga, Kupima na Kumilikisha ardhi wa Igumbilo Manispaa ya Iringa.
…………………………………………………………………………………………
Na Eliafile Solla
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii imezitaka Halmashauri zote nchini ambazo zilikopeshwa fedha na Wizara ya Ardhi kwa ajili ya mradi wa Kupanga, Kupima na Kumilikisha ardhi kurejesha fedha hizo kabla ya tarehe 25 Machi, 2021 ili fedha hizo ziweze kukopeshwa kwa Halmashauri nyingine ambazo bado hazijapanga, wala kupima maeneo yao.
Agizo hilo limetolewa Mkoani Iringa jana na Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii Mhe. Aloyce A. Kwezi wakati kamati hiyo ilipotembelea na kukagua mradi wa Kupanga, Kupima na Kumilikisha ardhi wa Igumbilo ambao umetekelezwa na Manipsaa ya Iringa kwa kutumia fedha hizo za mkopo walizopewa na Wizara ya Ardhi.
‘‘Kimsingi kazi ya upangaji miji ni jukumu la kila Halmashauri na siyo Wizara hivyo ni lazima mtambue kwamba Wizara iliwasaidia katika kutekeleza majukumu yenu ya msingi kuwakopesha fedha na ndiyo maana mkopo huo haukuwa na riba ili mkapange, mpime na mmlikishe wananchi ardhi kwenye Halmashauri zenu’’ alisema Kwezi.
Kwa upande wake Mhe. Angelina Mabula Naibu Waziri Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, aliishukuru Kamati hiyo ya Bunge na kusema nia ya Serikali kupitia Wizara ni kuona kila kipande cha ardhi nchini kinapimwa na hivyo Wizara iliamua kuziwezesha Halmashauri zenye dhamana ya upangaji miji katika maeneo yao kwa kuzikopesha kiasi cha fedha ili zitumike katika utekelezaji wa kazi hizo za upangaji,upimaji na umilikishaji ardhi na kisha kuzirejesha.
Mabula aliongeza kwamba, Wizara kwa kuanzia ilitoa mikopo ambayo haina riba kwa Halmashauri 24 nchini kwa lengo la kupunguza migogoro kwa kuwapimia wananchi maeneo yao na kuzisaidia Halmashauri kuongeza kipato ambapo walikuwa na uwezo wa kupima maeneo na kuyauza ila hadi sasa ni Halmashauri saba tuu zimerejesha fedha hizo za Wizara kitu kinachokwamisha mradi kutekelezwa na Halmashauri nyingine kwani mradi ulitakiwa kuwa endelevu.
Mradi wa Kupanga, Kupima na Kumilikisha ardhi wa Igumbilo Manispaa ya Iringa, ulianza kutekelezwa kuanzia 2019/2020 kwa fedha ya mkopo kutoka Wizara ya Ardhi, ambapo jumla ya viwanja 375 vilipimwa na kati ya hivyo viwanja 253 vilikuwa na sifa ya kuuzwa na 122 havikuwa na sifa ya kkuza kutokana na sababu mbalimbali.
————————————-MWISHO——————————————————-